Sunday, July 17, 2016

MAANA YA PAROLE, MADHUMUNI YAKE NA SHERIA ZA BODI YA PAROLE HAPA NCHINI

IMA
Mh Agustino Lyatonga Mrema Mwenyekiti wa Bodi ya Parole
……………………………………………………………………………………………………………..
Na; Lucas Mboje – Jeshi la Magereza,
PAROLE ni utaratibu wa kisheria unaompa fursa mfungwa aliyehukumiwa kutumikia kifungo Gerezani cha miaka minne na kuendelea kutumikia sehemu ya kifungo chake katika jamii kwa masharti maalum baada ya kukidhi vigezo vifuatavyo:-
i).    Awe ametumikia theluthi (1/3) ya kifungo chake na kuonesha mwenendo wa kurekebika kurudi katika jamii kumalizia sehemu ya kifungo chake kwa masharti maalum. Masharti hayo ni  kuwa chini ya uangalizi maalum kuhakikisha kuwa hatendi kosa lolote mpaka atakapomaliza kifungo chake, kuzingatia masharti ya Parole anayopewa kikamilifu pamoja na kuwa raia mwema na kuishi kwa kujipatia kipato halali katika jamii;

ii).    Awe ameonesha kujutia kosa, kurekebika tabia na kuonesha mwenendo mzuri gerezani na;
iii).    Mamlaka husika kujiridhisha kuwa hatahatarisha usalama wa jamii.
 
Parole ni moja kati ya adhabu mbadala na imeonesha mafanikio makubwa katika nchi nyingi duniani.  Utaratibu huu ni wa kipekee kwa kuwa unawagusa wafungwa wa vifungo virefu ambao ndio wengi waliopo magerezani. Aidha, ni utaratibu unaoshirikisha jamii katika urekebishaji kwa kuzingatia usalama wa jamii na dhana kwamba uhalifu ni zao katika jamii.

Madhumuni ya kuanzishwa kwa utaratibu wa Parole  nchini hayatofautiani na madhumuni ya kuanzishwa kwa utaratibu huu kwenye nchi nyingine Duniani zikiwepo nchi za Afrika kama vile: Afrika kusini, Zambia na Namibia.  Mfumo wa Parole ulioainishwa hapa nchini unatokana na uzoefu wa Parole unaotumika nchini Canada.  Sababu zilizopelekea kuanzishwa kwa Parole hapa Nchini ni:-

i.    Kuhusisha jamii katika suala zima la urekebishaji wa wafungwa badala ya kutegemea serikali peke yake kwani chanzo cha uhalifu ni mazingira yanayotokana na jamii yenyewe.

ii.    Kuwepo na kuendelea kuongezeka kwa idadi ya wafungwa wenye vifungo virefu magerezani ambao kutokana na urefu wa vifungo vyao hawawezi kufaidika na programu zilizopo za urekebishaji kwa sababu ama watatoka magerezani wakiwa wazee wasiojiweza, watakutana na mabadiliko makubwa kijamii, kiuchumi na kisera wasiyoweza kuyamudu haraka/ipasavyo kwenda na wakati au watafia gerezani.

Wafungwa wa aina hii hukata tamaa kwani hawaoni sababu ya kuwa na nidhamu wawapo gerezani, hivyo kusababisha usalama magerezani kuwa mashakani.  Parole ilikusudiwa kuwarejeshea matumaini ya kurejea katika jamii na kuishi maisha ya kawaida na kupunguza tishio la kiusalama magerezani na katika jamii kwa ujumla.
Jeshi la Magereza kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi liliwasilisha mapendekezo ya kutungwa Sheria ya Bodi za Parole nchini. Mapendekezo hayo yalijenga hoja ambayo hatimaye iliwasilishwa katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwezi Novemba, 1994 na kupitishwa rasmi kuwa Sheria ya Bodi za Parole Na. 25/1994. 

Sambamba na kutungwa kwa Sheria hiyo, kanuni za Bodi za Parole ziliandaliwa na kutangazwa kwenye Gazeti la Serikali tarehe 29 Agosti, 1997 (GN. 563/1997) hivyo kuwezesha Sheria hiyo kuanza kutumika rasmi. Hata hivyo Sheria iliyopitishwa haikuzingatia mapendekezo yaliyotolewa na Jeshi la Magereza ambayo yaliwalenga wafungwa wote kunufaika na Parole bila kujali aina na uzito wa makosa. Aidha, Sheria husika haikuanza kutumika mara moja kutokana na sababu zifuatazo:-
i.    Bodi ya Taifa ya Parole na Bodi za Parole za Mikoa zilizokuwa zimeundwa kwa mara ya kwanza zilivunjwa na kuundwa upya na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya kulalamikiwa kuwa uteuzi wa Wajumbe wake haukuzingatia uwiano wa jinsia na dini.

ii.    Kutokamilika kwa maandalizi ya nyaraka mbalimbali muhimu katika utekelezaji wa mpango wa Parole ikiwa ni pamoja na uendeshaji wa semina kwa wajumbe wa Bodi za Parole za Mikoa yote nchini ili kufanikisha uanzishwaji na utekelezaji wa Sheria hiyo.
Baada ya matukio hayo, kikao cha kwanza cha Bodi ya Taifa ya Parole kilifanyika tarehe 19 Agosti, 1999 ambacho kiliwajadili wafungwa watano (5) na kupitisha watatu(3) walioonekana kutimiza  masharti ya kuachiliwa kwa Parole nchi nzima. Idadi hiyo ni ndogo hasa ikizingatiwa kwamba wakati huo magereza yote nchini yalikadiriwa kuwa na wafungwa 27,000. Kutokana na Wafungwa  hao watano waliojadiliwa, ilidhihirisha kuwa Sheria yenyewe ilikuwa   haitekelezeki kama ilivyokusudiwa katika mapendekezo yaliyowasilishwa na Jeshi la Magereza hapo awali.
Matokeo haya yalisababisha Bodi ya Taifa ya Parole kuishauri  Serikali  kupanua wigo wa sheria hii ili wafungwa wengi zaidi waweze kunufaika. Mapendekezo haya yalilenga kifungu cha nne     cha sheria     ya Bodi za Parole vifungu vidogo (a),(b) na (c) ambavyo vinataja kuwa wafungwa wanaotumikia vifungo vya maisha, waliofungwa kwa makosa ya unyang’anyi wa kutumia silaha,     madawa ya kulevya, kujamiiana na adhabu ya kifo iliyobadilishwa  kuwa kifungo kwamba     hawawezi kupata msamaha wa Parole. Ilipendekezwa kwamba  kifungu hicho kirekebishwe ili     wafungwa wote wa makosa hayo nao wafikiriwe kunufaika na  utaratibu wa Parole bila kujali makosa waliyotenda.
Kutokana na mapendekezo yaliyotolewa na Bodi ya Taifa ya Parole, Sheria Na. 25/1994 ilifanyiwa marekebisho kwa Sheria Na. 5/2002 ambayo ilijihusisha na eneo dogo tu kwamba badala ya mfungwa anayestahili Parole kuwa amehukumiwa kifungo cha miaka nane (8) na kuendelea, ilirekebishwa na kuwa awe amehukumiwa kifungo cha miaka minne (4) na kuendelea.

Chini ya marekebisho hayo Wakili wa Serikali Mfawidhi wa kanda aliongezezwa kuwa mjumbe wa Bodi ya Parole ya Mkoa. Hata hivyo suala la aina ya makosa na urefu wa kifungo katika kufikiriwa kunufaika kwa mpango wa Parole lilibaki kama lilivyokuwa hapo awali. Baada ya marekebisho hayo ya Sheria ya Bodi za Parole, Bodi  za Parole za Taifa na Bodi za Mikoa zilizinduliwa upya mwaka 2003, na Bodi ya Taifa ya Parole ilifanya kikao chake cha kwanza mwezi Agosti, 2003  ambacho kilikuwa cha pili tangu Sheria hii ilipoanza kutumika rasmi nchini mwaka 1999.

Kwa mujibu wa Sheria na Sera za kitaifa kuhusu uboreshaji wa Magereza zinazotolewa kufuatia kuridhiwa kwa maazimio mbalimbali ya Kimataifa katika kuboresha hali za wafungwa magerezani, imeonekana kuwa vifungo siyo njia pekee ya kumrekebisha mhalifu. Adhabu mbadala zimeonekana ni bora zaidi kuliko kifungo kwa vile jamii huhusishwa katika suala zima la kumrekebisha mhalifu. 

Adhabu mbadala zinazotumika hapa nchini ni pamoja na kulipishwa faini, Kuachiliwa kwa masharti, Probation, Kuachiliwa kwa matazamio, Kifungo cha Nje (EML), Parole, Huduma kwa Jamii n.k. Aidha, katika adhabu mbadala   zilizoainishwa, Utaratibu wa Parole umeonekana unafaa zaidi kwa kuwa ndugu, uongozi wa mtaa/kijiji na mwathirika wa uhalifu hushirikishwa kutoa maoni kabla ya mfungwa husika kunufaika na mpango huu. Aidha, ni adhabu mbadala pekee inayohusika na wafungwa wanaotumikia vifungo virefu magerezani. Itaendelea …………wiki ijayo……!.
MWANDISHI WA MAKALA HII NI AFISA NGAZI YA JUU WA JESHI LA MAGEREZA, KWA MAONI NA USHAURI  – 0754 871084lucasmboje@yahoo.co.uk or mbojelucus@gmail.com

No comments: