Friday, July 29, 2016

U17 MADAGASCAR KUIJARIBU SERENGETI BOYS KESHO


Timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 ya Madagascar kesho Jumamosi Julai 30, 2016 itacheza mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Serengeti Boys ya Tanzania kwenye Uwanja wa Taifa wa Madagascar.

Serengeti Boys imepiga kambi jijini Antananarivo, Madagascar kujiandaa kucheza na Afrika Kusini katika mchezo wa awali kuwania nafasi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika utakaofanyika Agosti 6, 2016. Mchezo wa marudiano utafanyika Agosti 21, mwaka huu kwenye Uwanja wa Azam, ulioko Chamazi-Mbagala, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.

Taarifa kutoka kwa mkuu wa msafara Ayoub Shaibu Nyenzi ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Soka la Vijana, zinasema mchezo huo ni muhimu na Kocha Kocha Mkuu, Bakari Nyundo Shime au Mchawi Mweusi, amesema kwamba amefurahi kupata nafasi hiyo huku Daktari wa timu hiyo, Shecky Francis Mngazija akithibitisha kwmaba vijana hao wako salama.

Nyota walioko kambini ni pamoja na makipa, Ramadhani Awm Kabwili, Kelvin Deogratius Kayego na Samwel Edward Brazio wakati mabeki wako Kibwana Ally Shomari, Nickson Clement Kibabage, Israel Patrick Mwenda, Dickson Nickson Job, Ally Hussein Msengi, Issa Abdi Makamba na Enrick Vitalis Nkosi.
Viungo ni Kelvin Nashon Naftal, Ally Hamisi Ng’anzi, Asadi Ali Juma Ali, Syprian Benedictor Mtesigwa, Ibrahim Abdallah Ali, Shaban Zuberi Ada huku washambuliaji wakiwa ni Mohammed Abdallah Rashid, Yohana Oscar Mkomola na Muhsin Malima Makame.
Serengeti Boys inakwenda kucheza na Afrika Kusini baada ya kuwatoa Shelisheli kwa jumla ya mabao 9-0 katika mechi zake mbili za kimataifa. Mshindi wa jumla kati ya Serengeti Boys na Afrika Kusini, atacheza na timu mshindi kati ya Namibia na Congo-Brazaville.
Hivi karibuni Serengeti Boys ilifanya ziara India ambako walishiriki mashindano ya vijana ya Kimataifa yanayotambuliwa na FIFA (AIFF International Youth Tournament 2016) kabla ya kurudi na rekodi ya kupigiwa mfano si tu katika Tanzania na kwa nchi za Afrika Mashariki. Ilishika nafasi ya tutu nyuma ya Korea Kusini na Marekani.

No comments: