Wednesday, July 20, 2016

Wakazi wa kijiji cha Madimba kata ya Madimba mtwara walalamikia ubovu wa matank ya kuhifadhia maji


                             PICHA NA MAKTABA YETU

                Wakazi wa kijiji cha Madimba kata ya Madimba  baada ya kupata maji waliyoyakosa kwa zaidi ya miaka ishirini sasa wamelalamikia ubora wa matanki yanayohifadhia maji baada ya kuanza kupasuka.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kijijini hapo,wananchi hao walisema kuwa baada ya kufariki kwa mmoja wa mtoto aliyekuwa akitafuta maji waliweza kupatiwa huduma hiyo na kuwapunguzia machungu lakini sasa wanaingia katika gharama nyingine ya kukarabati matanki hayo.

Septemba 15 mwaka jana gazeti hili liliripoti ukosefu wa maji uliosababisha kifo cha mtoto Maliki Hamisi(11) mkazi wa kijiji hicho kuumwa na nyoka na kupelekea kifo wakati akitafuta maji kwenye visima vya kienyeji maporini hali ambayo iliwezesha kijiji hicho kupatiwa maji na Shirika la Maendeleo ya Petrol nchini (TPDC) ambao ni wajenzi wa mtambo wa kuchakata gesi asilia uliopo kijijini hapo ambapo gesi yake inakwenda jijini Dar es Salaam.

Akizungumza Mohamed Linangwa mkazi wa kijiji hicho, alisema wamekuwa wakiahidiwa maji kwa muda mrefu lakini baada ya kupatiwa maji matanki yake yamekuwa yakipasuka kutokana na kukosa uimara.
“Walikuja viongozi mpaka rais mstaafu Kikwete ,na mawaziri wakatuahidi maji kwa kipindi kirefu tukayapata lakini sio ya kukidhi mahitaji kwasababu ukienda yalipo maji matanki ni ya plastiki yametupasukia na kijiji ni kikubwa kina watu wengi ambao wanalazimika kutembea umbali mrefu kuja yalipo matanki,”alisema

Naye Amina Hamis alisema suala la maji bado ni changamoto kwasababu wamekuwa wakilazimika kutembea umbali mrefu kutafuta maji yaliyopo katika kijiji hicho lakini nayo yanauzwa.

“Maji yapo lakini tunauziwa tofauti na zamani tulikuwa tukiyatafuta kwenye mashimo maporini na kukutana na wadudu ila kero kubwa yale mapipa ni ya plasitiki yameshaanza kupasuka inalazimika tena uongozi wa kijiji uingie gharama kuyakarabati kwa zile pesa ambazo tulitegemea zingetusambazia mabomba sisi tulio mbali na yalipo matanki,”alisema Hamis
Akizungumza mwenyekiti wa kijiji hicho, Mohamed Madiza alisema kijiji hicho bado kinakabiliwa na tatizo la maji kutokana na kuwa na vitongoji 9 hivyo wanalazimika kutembea umbali mrefu.

“Maji kwa sasa yanapatikana lakini kijiji changu kina vitongoji tisa hivyo wale walio vitongoji vya mbali mfano Mahiva wanalazimika kutembea karibia kilomita 5 kuja kufuata maji tuliyowekewa na TPDC lakini na yenyewe mapipa ni ya plastiki yameanza kupasuka,”alisema Madiza
Aidha alisema maji hayo yamekuwa yakiuzwa Sh 50 kwa kila ndoo ya lita 20 ambapo pesa inayopatikana inakusanywa ili kuona kama kuna uwezekano wa kuyasambaza katika vitongoji vilivyopo mbali.

“Ni kweli moja ya pipa lilipasuka na tukatumia pesa za mradi zile tunazouzia maji kumlipa fundi arekebishe kwa thamani ya laki mbili nay ale mengine manne yako salama lakini sio ya kuaminika sana kwani linapopasuka italazimika tutumie pesa tulizokusudia kusambazia maji ili kukarabati,”alisema Madiza
Mwisho…………….
       

No comments: