.

WANANCHI NDANDA WAAMUA KUUNGANA KUTENGENEZA BARABARA YAO,WENGINE WAVUNJA NYUMBA ZAO NA KUKATA MITI KUPISHA BARABARA

Diwani Wa kata ya Ndanda CONSTANSIA BERNARD akishiriki kukata miti
Wananchi wa kijiji cha Mpowora kata ya Ndanda baada ya kukabiliwa na ukosefu wa barabara kwa miaka mingi wameamua kujitolea kwa kushirikiana na viongozi wao ili kuhakikisha wanapata barabara huku baadhi wakivunja nyumba zao na kukata mimea ili kupata huduma hiyo muhimu.
Kutokana na adha hiyo inaelezwa imekuwa ikipelekea baadhi ya wanawake kujifungulia majumbani na wengine njiani hasa wakati wa masika kutokana na kukosekana kwa usafiri.

Akizungumza diwani wa kata hiyo,Constansia Bernard alisema kutokana na ukosefu wa barabara katika kata hiyo,wananachi  wamekuwa wakipoteza maisha hasa wanawake kwa  kujifungulia njiani.

“Kata yangu ina changamoto nyingi hasa barabara zinazounganisha kijiji na kijiji hali ambayo imekuwa ikisababisha wajawazito wanapopata uchungu kuzalia njiani na wengine nyumbani kwasababu kipindi cha masika vyombo vya usafiri kama bodaboda zinakuwa hazifanyi kazi,”alisema Bernard

Akizungumza mwalimu mkuu wa shule ya msingi Mpora iliyo kijijini hapo,Patricia Edward alisema wageni mbalimbali wanapotaka kutembea shule hiyo kwa shughuli mbalimbai wamekuwa wakiishia njiani kutokana na kukosekana barabara.
“Barabara ni kero,mara nyingi hata wasimamizi walipotaka kuja wamekuwa wakishukia Ndanda na kutembea umbali mrefu karibu kilomita mbili,hata tunapoletewa msaada kama madawati  inabidi yashukie Ndanda tukafuate wenyewe kwahiyo inakuwa ni gharama na wakati mwingine kama ni vitabu inalazimika wanafunzi wakavifuate wagawane kidogo kidogo,”alisema mwalimu Edward
Akizungumza mbunge wa jimbo hilo,Cecil Mwambe aliwataka wananchi wote kujitolea kwaajili ya kuendelea kuchimba barabara na kushukuru wale waliojitolea kukata mimea yao.

“Wananchi tayari wamekubaliana tutengeneze barabara,na wapo wananchi ambao wamekubali kuvunja nyumba zao na kung’oa visiki na kukata mimea yao ili waweze kupata huduma hii muhimu niwashukuru kwa ujasiri,kikubwa niombe ushirikiano zaidi kutoka makundi yote,”alisema Mwambe

Mmoja wa wanakijiji hao Halima Liumbe alisema “Barabara ilikuwa kero sana lakini tunamshukuru mbunge wetu kwa kutuunganisha na sasa tumeanza kukata miti ili tupate barabara nina uhakika tukishapata barabara hakuna mwanamke atakayejifungulia tena njiani ama atakayeshindwa kumpeleka mwanaye kliniki kuhudhuria zile huduma muhimu za watoto kama chanjo.,”alisema Liumbe

About HABARI24 TV

Post a Comment
Powered by Blogger.