Saturday, August 13, 2016

Chadema Yaanza Kugawa Vifaa vya Operesheni UKUTA


CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Pwani kimeanza kugawa vifaa zikiwemo bendera kwa ajili maandalazi ya Umoja wa Kupinga Udikteta ( Ukuta) ambayo yanatarajia kufanyika Septemba mosi mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Katibu wa Kanda ya Pwani wa Chadema, Casimir Mabina, alisema kuwa bendera hizo zitaanza kupeperushwa kuanzia kesho kutwa kwa ajili ya kuunga mkono azimio la Kamati Kuu ya kufanyika oparesheni Ukuta.
Alisema oparesheni Ukuta ni lazima ifanyike nchi nzima na kwamba hawako tayari kuona ukandamizaji wa demokrasia unaoendelea kufanywa na serikali ya awamu ya tano ambayo imeonyesha viashiria vya utawala wa kidikteta.
Alisema Rais John Magufuli, anajaribu kuua demokrasia ya vyama vingi kwa kukataza na kuzuia mikutano ya kisiasa ya vyama vya upinzani huku CCM ikiendelea na mikutano yake kama kawaida.
“Tumeona jinsi Rais alivyopiga marufuku wapinzani kukutana kwenye mikutano ya hadhara huku akiwatishia kuwa wakikaidi atawashughulikia na kweli amewaamuru polisi watekeleze amri hiyo ya kuwakamata viongozi wa Chadema na kuwafungulia mashtaka,” alisema
Aliongezea kuwa mbaya zaidi Jeshi la Polisi linazuia hata mikutano ya ndani ya vyama vya upinzani na makongamano na hata mahafali ya wanafunzi wenye itikadi za upinzani licha ya kutambua kuwa mikutano ya ndani haiwezi kuleta uvunjifu wa amani kwa walio ndani ya ukumbi.
Alisema licha ya kwamba Mwenyekiti wa CCM Rais Magufuli. amekataza mikutano hiyo kufanyika chama tawala, kinafanya mikutano ya hadhara katika maeneo mbalimbali kwa kisingizio cha shughuli za serikali.
Mabina alisema juzi CCM ilisema itakuwa na maandamano kutoka uwanja wa ndege wa Mwalimu Nyerere ya kumpokea Rais Magufuli hadi Makao Makuu ya CCM yaliyopo Lumumba.
“Tunahoji haki ya kufanya siasa ni kwa CCM tu na siyo kwa vyama vingine? Hili jambo hatuwezi kukubali Jeshi la Polisi lituambie inakuwaje vibali vinatolewa kwa CCM halafu upinzani tunyimwe tunasema lazima tufanye oparesheni Ukuta ya kupinga ukandamizaji wa demokrasia,” alisema Mabina
Naye Katibu wa Wabunge wa Upinzani Mkoa wa Dar es Salaam, Mbunge wa Viti Maalum, Anatropia Theonest, alisema lengo la oparesheni ya Ukuta ni kupinga ukandamizaji unaofanywa na serikali.
Alisema wana haki ya kikatiba ya kufanya mikutano bila kuzuiliwa kama ambayo wamefanyiwa na ndio maana wameanza kugawa bendera kwa ajili ya kujiandaa na oparesheni hiyo.

No comments: