Thursday, August 4, 2016

WANAHARAKATI WAENDELEA KUIKOMALIA SHERIA YA NDOA ZA UTOTONI TANZANIA,

Valeria Msoka Mwenyekiti wa Mtandao wa kupinga ndoa za utotoni Tanzania katikati akizungumza na wanahabari kuhusu sheria hiyo na hatua wanazochukua,Kulia ni Mkutugenzi wa kituo cha sheria na haki za binadamu nchini LHRC Bi Hellen Kijo Bisimba

Mtandao wa mashirika yanayopinga ndoa za utotoni ni mtandao unaoundwa na asasi zisizokuwa za kiselikali zipatazo 32 hapa nchini. Mtandao huu umekuwa ukifanya kazi mbalimbali katika ngazi ya kijamii mpaka ngazi ya kitaifa ili kuondokana na ukatili wa watoto ikiwemo  ndoa za utotoni.

Mwanzoni mwa mwaka huu taasisi ya mwanamke initiative ambayo ni mwanachama wa mtandao huu  ulifungua  kesi ya kikatiba katika mahakama kuu ya Tanzania, shauri namba 5 la mwaka huu 2016 ikiwa ni kati ya Rebeca Gymu (Mkurugenzi mtendaji wa taasisi hiyo)  na mwanasheria mkuu wa serikali.katika kesi hii mlalamikaji alikuwa akihoji  uhalali wa kikatiba wa vifungu namba 13 na 17 vya sheria ya ndoa ya mwaka 1997 iliyokuwa ikieleza kuwa mtoto wa kike anaruhusiwa kuolewa akiwa na umri wa miaka 14 au 15 kwa ridhaa ya wazazi au mahakama.
Rebeca Gymu mwanaharakati aliyefungua kesi hiyo mapema mwaka huu juu ya sheria mbovu ya Mtoto hapa akizngumza na wanahabari kuhusu maswala mbalimbali,Pembeni ni Hellen Kijo Bisimba Mkurugenzi mtendaji wa kituo cha sheria na haki za Binadamu LHRC
Valeria Msoka mwenyekiti wa Mtandao wa kupinga ndoa za utotoni Tanzania alisema wao wakiwa kama watetezi wa haki za watoto na wanaopinga ndoa za utotoni walifurahishwa na hukumu iliyotolewa mapema Julai 8,2016 chini ya jaji mkuu Shabani Lila ambapo alisema vifungu hivyo sio halali kwa mujibu wa katiba na kuitaka serikali kubadilisha ndani ya muda wa mwaka mmoja.
Alisema wao kama Taasisi inayopinga ndoa za utotoni walishangazwa na walishtushwa na tamko la mwanasheria mkuu wa selikali kuwa amekata rufani katika mahakama ya rufani ili kupinga uamuzi uliotolewa na mahakama kuu kwenye kesi hiyo.

Aidha aliendelea kusema kuwa wao wameshindwa kuelewa rufaa hii inabebwa na misingi gani na je ni kweli selikali ya Tanzania inataka kuendelea kuwa na vifungu hivi vinavyosema kuwa mtoto  wa kike aweze kuolewa chini ya miaka 18.

April 27 waziri wa katiba na sheria alizungumza bungeni kuhusu dhamira ya selikali kupeleka mswaada bungeni kupinga ndoa za utotoni akijibu swali la mbunge wa ileje aliyetaka kujua ni lini selikali itafanya marekebisho ya sheria ya ndoa nchini, wao wakiwa kama wanamtandao na wanaopinga ndoa za utotoni walitegemea kwenye hili selikali ingeamua kuchukua shauri la mahakama kuu na kuboresha sheria hiyo lakini matokeo yake selikali yenyewe ndio inaenda kukata rufaa kupinga  hukumu hiyo.

Aliendelea  kusema ikumbukwe kuwa Tanzania ni nchi mwanachama wa umoja wa mataifa na umoja wa afrika na iliridha  mikataba mbalimbali  ya kikanda na ya kimataifa ya kulinda haki na ustawi wa mtoto na kupinga aina zote za ukatili na ubaguzi dhidi ya mwanamke.mikataba hiyo ni pamoja na mkataba wa haki za  mtoto wa kimataifa wa mwaka 1989 pamoja na mkataba wa afrika wa haki na ustawi wa mtoto pia wa mwaka 1990,hivyo kama selikali ina haki ya kutunga sheria kama wajibu wa utekelezaji wa sheria hii kwani ndoa za utotoni ni ukiukwaji wa haki za binadamu na ni ukatili wa wanawake na watoto wa kike.

Tafiti mabailmbali zilizofanyika zinaonyesha kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye idadi kubwa  ya ndoa za utotoni  kwa takribani 35% ndoa za utototoni ni janga la kitaifa na zinamadhara  makubwa kwa mtoto mwenyewe hata jamii nzima.

Ndoa za utotoni husababisha mimba za utotoni zenye kumuathiri mtoto wa kike kwa mfano tarehe 2 julai 2012 taasisi ya Tanzania life Improvement Association (TALIA) ilitoa taarifa kwamba kulingana na takwimu za wizara ya elimu, mafunzo ya ufundi, kila mwaka wasichana 8,000 huacha masomo kutokana na mimba za utotoni.  Aidha kila mwaka 24% ya wanawake wajawazito hufa kutokana na matatizo ya mimba za utotoni na aslilimia 5 mpaka 6 ni watoto wa kike wenye umri chini ya miaka 18.

Inapozungumziwa nafasi ya mwanamke hapa nchini Tanzania na changamoto anazokutana nazo kiuchumi ,kisiasa na kijamii msingi wake pia hutokanana na mambo kama haya ya ndoa chini ya miaka 18. Mtoto wa kike ananyimwa fursa ya kukua na kufurahia utoto wake, fursa ya kupata elimu , fursa ya kujitambua na hata ya kujiinua kiuchumi kwani ndoa za utotoni huua kabisa ndoto za mtoto huyo.

Madhara mengine yatokanayo na ndoa za utotoni ni ukatili wa kijinsia kwani watoto hawa uozeshwa kwa watu waliowazidi sana umri. Ndoa za utotoni zina madhara kiafya ikiwemo kupoteza maisha, kupata shida wakati wa uzazi, maambukizi ya magonjwa ikiwemo ukimwi na hata malezi duni kwa watoto wanaozaliwa na mama huyo kwa kuwa na yeye bado ni mtoto hivyo basi kwa kuzingatia yote haya tunashangazwa sana na selikali inapinga maamuzi ya kubadilishwa kwa sheria kama vile walioko selikalini hawatambui madhara haya au wanayafurahia

 Wao kama wana mtandao wanapenda kuikumbusha selikali kuwa ni jukumu lao na ni wajibu kulinda haki za Raia na makundi  mbalimbali katika  jamii. Ulinzi huu unaweza kufanyika pale tu panapokuwa na misingi imara ya kisheria hata kiutawala na kimfumo ili kuhakikisha sheria zinasimamiwa ipasavyo.

Anasema kuwa Ni aibu kubwa sana taifa kuwa na sheria katika karne hii inayotamka wazi mtoto mwenye umri chini ya miaka 18 anaweza kuolewa. pia selikali ikumbuke kuwa imeridhia utekelezaji wa mipango endelevu ya maendeleo 2030 pamoja na ajenda ya umoja wa afrika 2063 vya kuondokana na vitendo vyote vya ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto ,kiuchumi, na kisiasa.ili kuweza kutekeleza mipango na mikakati hii selikali inawajibu wa kuhakikisha kuwa inaweka misingi thabiti ya sheria na usimamizi wa sheria hizo. Wanamtandao wanaishauri selikali iondoe kusudio hilo la kukata rufaa na ijipange kutekeleza amri ya Mahakam kuu.

No comments: