Friday, August 12, 2016

WAZIRI NDALICHAKO AWAPA AHADI KEMKEM WANASAYANSI CHIPUKIZI TANZANIA


Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi Prof. Joyce Ndalichako akiwakabidhi Tuzo washindi wa Jumla wa mashindano ya wanasayansi Chipukizi ambao ni wanafunzi kutoka Mtwara Jana katika mashindano yaliyohitimishwa Jijini Dar es salaam
Wakati serikali ya Tanzania ikijitahidi kuifanya elimu ya nchi kuwa bora na Rahisi kwa kila mtanzania kuipata naye Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi Prof. Joyce Ndalichako,amesema kuwa Serikali itahakikisha inawawezesha na kuwatengenezea mazingira mazuri Wanafunzi Chipukizi wanaosoma Masomo ya Sayansi kwa kuhakikisha wanaboresha maabara na kufanya sayansi ya vitendo kufundishwa zaidi mashuleni.

 Hayo yanakuja ikiwa Tanzania inajiandaa na kuingia katika mfumo wa viwanda ambapo serikali ya awamu ya tano imekuwa ikitangaza kuwa ndiyo mfumo mpya wa kuhakikisha kuwa nchi inasonga mbele ambapo imekuwa ikielezwa kuwa ili malengo hayo yatimie ni lazima nchi itengeneze wanasayansi wa kutosha.
Akizungumza Dar es Salaam jana katika kufunga  Mashindano ya wanasayansi chipukizi kutoka shule zaidi ya 300 za Sekondari yaliyoandaliwa na Taasisi ya YOUNG SCIENTIST TANZANIA alisema ni vema serikali ikaendelea kuimarisha uwekezaji wake katika masomo ya sayansi ili kuongeza idadi kubwa ya wanasayansi nchini.

Washindi wakifurajhia Tuzo yao 
Alisema kwa sasa masomo hayo yamekuwa yakitolewa kwa vitendo zaidi na kuwafanya  wanafunzi kufanya utafiti na kubuni vitu mbalimbali vya kisayansi ambavyo vinalenga kuja kusaidia jamii ya kitanzania.

“Vipaji vinavyoonyeshwa na wanafunzi hawa wanaosoma masomo ya sayansi ambao bado ni Chipukizi,ni vipaji ambavyo vinaubunifu wa hali ya juu ambavyo wamevitengeneza kwa hali ya juu kulinganisha na rika walilokuwa nao,”alisema Prof. Ndalichako
Alisema kuwa Serikali itahakikisha inaendeleza vipaji vya wanasayansi hao  Chipukizi pindi wanapokuwa shuleni kwa kuwapa nafasi walimu wao kuandaa mashindano mbalimbali ya ngazi ya Wilaya,Mkoa hadi Kitaifa ambayo yataongeza tija ya wanafunzi kusoma masoma ya sayansi zaidi.
Prof.Ndalichako aliongeza kuwa kwa sasa wizara yake inanunua vifaa  mbalimbali vya Maabara kwa lengo la kupeleka vifaa hivyo katika shule za vijiji ambazo bado hazina vifaa itakayosaidia wanafunzi wa shule hizo kusoma masomo ya sayansi kwa vitendo zaidi.


“Kwa sasa hali ya masomo ya Sayansi kufundishwa katika shule zetu sio mbaya kwani tumejionea katika mashindano haya,ushiriki wa shule mbalimbali hadi zile za vijijini kufanya vizuri hivyo ni juhudi ya serikali na wadau mbalimbali kuhakikisha Sayansi inakuwa na wadau wengi ambao baadae waendelezwa na Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTEC),”alisema Prof.Ndalichako

Waziri Ndalichako akikagua kazi mbalimbali za wanasayansi chipukizi wa Tanzania katika maonyesho ya Sayansi yaliyofanyika Ktika ukumbi wa mwalimu Nyerere Dar es salaam yaliyoandaliwa na Taasisi ya Young scientist Tanzania 
Kwa Upande wake Mkurugenzi na Mwanzilishi Mwenza wa Shirika la 
Wanasayansi Chipukizi Tanzania(YST),Dkt Gosbert Kamugisha alisema kuwa vijana wengi wanapenda kusoma masomo ya sayansi lakini mazingira wanayokutana nayo ndio yanasababisha wasiweze kusoma masomo hayo.


Alisema Mashindano wanayoyafanya vijana kuona sayansi inaweza kufanyika katika njia tofauti tofauti na ikafanyika kwa vitendo zaidi ambapo wanaona sayansi inafurahisha na inauwezo wa kusaidia jamii kujikwamua kiuchumi.

“Kijana anahitaji kuonyeshwa njia na mwalimu wake ili sayansi anayofanya isiishie kwenye exprementi tu kama inavyoonyeshwa katika vitabu vya fizikia,bioloji au chemistry bali wafundishwe kutumia sayansi katika kumaliza tatizo linalokabili jamii kwa kufanya utafiti na kugundua teknolojia ya kukabiliana na changamoto iliyopo,”alisema

Katika Mashindano hayo ambapo yalishirikisha wanafunzi zaidi ya 50 shule ya wasichana ya Mtwara ilichukua nafasi ya kwanza katika mashindano hayo huku nafasi ya pili ikichukuliwa na Shule ya Sekondari ya Mzumbe.





















No comments: