Saturday, September 10, 2016

VIJANA ACT WAZALENDO WAUNGA MKONO MAAZIMIO YA KAMATI KUU YA CHAMA HICHO

Edna Sunga Katibu Vijana Taifa ACT-Wazalendo akizungumza na wanahabari makao makuu ya chama hicho Jijini Dar es salaam mapema leo ambapo vijana wa chama hicho wameunga mkono maazimio mbalimbali yaliyotolewa na kamati kuu ya chama Hicho
NGOME YA VIJANA ACT WAZALENDO
TAMKO LA KUUNGA MKONO MAAZIMIO YA KAMATI KUU YA CHAMA CHA ACT WAZALENDO CHA TAREHE 5/09/2016 

JUMATATU ya septemba 5 mwaka huu  kamati kuu ya chama chetu cha ACT Wazalendo, kilifanya kikao chake cha kawaida na kutoka na maazimio mbali mbali yenye manufaa kwa taifa letu, baada ya kuangalia kwa kina hali ya kisiasa nchini, hali ya kiuchumi na tishio la kusambaratika kwa umoja wa kitaifa kutokana na mwenendo usioridhisha wa serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na chama cha Mapinduzi chini ya Rais John Magufuli

Katika hali ya kisiasa kamati kuu ya Chama cha ACT Wazalendo ilitambua kuwa Kikatiba, nchi yetu inafuata mfumo wa demokrasia ya vyama vingi. Katiba na Sheria mbalimbali zimeainisha utaratibu wa kazi na shughuli za vyama vya siasa. Ili kuhakikisha kwamba kazi na shughuli za vyama vya siasa zinakuwa endelevu, vyama vyenye kukidhi vigezo hupewa ruzuku kupitia Bajeti ya Serikali inayopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano Tanzania.   

Hata hivyo, katika awamu hii ya tano, Serikali ya Chama cha Mapinduzi imeamua kuzuia shughuli za siasa kwa kutumia nguvu ya Jeshi la Polisi na hata Jeshi la Wananchi. Kwa mujibu wa serikali ya CCM, shughuli za kiuenezi za vyama vya siasa kama vile mikutano ya hadhara, maandamano, makongamano, mijadala na hata mikutano ya ndani inapaswa kukoma mapema baada ya uchaguzi. Kisheria, huu ni uvunjifu wa Katiba na Sheria za nchi. 

Kisiasa, tunatambua kwamba Viongozi wa CCM wamepoteza mvuto kwa wananchi na sasa wanamsukuma Mwenyekiti wao Rais Magufuli kutumia jeshi katika kuokoa taswira ya Chama cha Mapinduzi mbele ya umma.
Kwa kuzingatia hayo yaliyoelezwa juu   Kamati Kuu ya chama chetu iliazimia yafuatayo: 

i. Ililaani na kupinga kwa nguvu  zote hatua za Serikali ya Chama cha Mapinduzi za kuvunja Katiba na kujaribu kuweka pembeni utawala wa sheria.
ii. ilipinga vitendo vinavyozidi kushamiri katika serikali hii ya CCM ya kujaribu kuendesha nchi kwa ubabe na matamko ya viongozi badala ya utawala wa sheria. 

iii. Ilisisitiza Chama kusimama  imara, na hata  kuungana na vyama vingine vya siasa pamoja na taasisi zingine za kiraia katika kulinda mfumo wa demokrasia ya vyama vingi, uhuru wa maoni, na utawala wa sheria katika nchi yetu.
Kwa maazimio hayo ya kamati kuu ya Chama sisi ngome ya vijana wa ACT wazalendo, tunaunga mkono kwa nguvu zote tukiwa na sababu za msingi za kufanya hivyo
 Sisi vijana tunatambua juhudi zozote za kuminya demokrasia, kutokufuata katiba ya nchi na kuruhusu mtu mmoja kuamua kuongoza nchi atakavyo bila kufuata na kuheshimu taratibu tulizojiwekea kama Taifa kitatuathiri zaidi sisi ambao dhamana ya Tanzania iliyo bora na yenye amani ipo mikononi mwetu.
 Kwa sababu ya kuminya demokrasia tunaona dhamira ovu ya serikali ya awamu ya tano ya kuifanya nchi isiwe na  viongozi bora wa siku zijazo hali hii inakiuka misingi iliyoachwa na baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere  ambaye alitoa fursa kwa vijana wa enzi hizo kuwa sehemu ya wenye kuhoji masuala mbali mbali kupitia majukwaa tofauti hali iliyotupatia viongozi bora kama Mzee Joseph Warioba na Salim Ahmed Salim ambao hawa wote walitambuliwa uwezo wao wakiwa ni vijana waliopewa fursa ya kuwasilisha hoja zao katika majukwaa huru
 Sisi ngome ya vijana wa ACT Wazalendo, tunamtaka Rais Magufuli atambue kuwa sababu yoyote ya kuendelea kuminya demokrasia kwa maslahi ya chama chake haitakuwa sababu ya kupunguza ari na moyo wa vijana wa kitanzania kuhitaji mabadiliko yaliyoshindwa kupatikana chini ya serikali yake kwa muda wa miaka 50 iliyopita

2 Hali ya Kiuchumi 
  Kuhusu hali ya kiuchumi  Kamati kuu ya Chama chetu ilieleza kuwa katika miaka 10-15 iliyopita, nchi yetu ilijenga uchumi uliokuwa ukikua kwa kiwango cha asilimia 6-7 kwa mwaka katika kipindi chote hicho. Ilieleza kuwa ukuaji huo wa uchumi ulitokana na juhudi za nchi katika kuvutia wawekezaji na kuchochea shughuli za uzalishaji mali kwa wananchi wenye kipato cha chini. Ikaeleza kuwa serikali ya awamu ya tano  ya Chama cha Mapinduzi imerithi changamoto ya uchumi unaokua bila kuwafaidisha wananchi wa kawaida na kwamba   ilitegemea Serikali mpya ishughulike nalo. 

Kamati Kuu ikaeleza kuwa imeshtushwa na hali ya kuanza kudorora kwa shughuli za uchumi katika kipindi cha miezi kumi ya utawala wa awamu ya tano. Kwa kutolea mifano kadhaa kwamba taarifa za Benki Kuu zilizopo kwenye tovuti yake (Quarterly Economic Review na Monthly Economic Review) kwa robo ya mwisho ya mwaka 2015 (Oktoba - Desemba 2015) zinaonesha kuwa kasi ya ukuaji wa Pato la Taifa ilikuwa 9%. Katika robo ya kwanza ya mwaka 2016 (Januari - Machi 2016) kasi ya ukuaji wa Pato la Taifa ilishuka hadi kufikia 5.5%. Kiuchumi, hii inamaanisha kuwa ukuaji wa shughuli za kiuchumi katika kipindi cha miezi 6 ya mwanzo ya utawala wa awamu ya tano chini ya Rais Magufuli umepungua kwa 4%! 
a. Shughuli za uchumi zinazohusu wananchi masikini zimeshuka kutoka kasi ya ukuaji ya 10.20% katika robo ya mwisho ya mwaka 2015 mpaka 2.7% katika robo ya kwanza ya mwaka 2016, ikiwa ni punguzo la 8% ndani ya kipindi kisichozidi miezi sita. 

Hi inamaanisha kwamba Wananchi wetu wanazidi kudumbukia kwenye ufukara kwa kasi tangu awamu ya tano ya Serikali ya Chama Mapinduzi iingie madarakani.
b. Ukuaji wa sekta ya ujenzi katika robo ya mwisho ya mwaka 2015 ulikuwa ni 13.8% lakini ukuaji wa sekta hiyo katika robo ya kwanza ya mwaka 2016 ilikuwa ni 4.30%, ikiwa ni tofauti ya takribani -10%. Hii ni kwa sababu uwekezaji katika sekta hii umeanza kushuka.

c. Kasi ya ukuaji wa sekta ya usafirishaji imeporomoka kutoka kukua kwa 14.50% robo ya mwisho ya 2015 mpaka kukua kwa 7.9% robo ya kwanza ya 2016, ikiwa ni kuporoka kwa 7% katika kipindi cha miezi 6 tu ya kwanza ya utawala wa Rais Magufuli. Kuporomoka kwa sekta ya usafirishaji itaathiri watu wengi, wakiwemo madereva, matingo, pamoja na mama ntilie wanaowauzia chakula.
Kwa kuzingatia mwenendo wa hali ya uchumi katika nchi, Kamati Kuu iliazimia yafuatayo
a) Iliitaka serikali izingatie ‘’sayansi ya uchumi’’ katika kuendesha uchumi wa nchi. Uamuzi wa CCM wa kuitelekeza serikali yake kwa mwanasiasa mmoja anayedhani ndiye anayejua kila kitu na yeye kugeuka kuwa mshauri wa washauri wa uchumi badala ya washauri wa uchumi kumshauri yeye, itasambaratisha uwekezaji nchini na kuua kabisa juhudi za miaka 20 za kuvutia wawekezaji na kujenga uchumi shirikishi. 
b) Kamati kuu ilihimiza  wananchi kuzingatia kuwa msingi wa uchumi wetu ni uwekezaji kutoka ndani na nje ya nchi.

 Msingi wa kuvutia wawekezaji ni utawala wa sheria.ikaeleza kuwa juhudi za serikali ya CCM za kuua utawala wa sheria zitaua uwekezaji na kuangamiza uchumi wa nchi na kwamba wananchi wasiiruhusu CCM iue uchumi wa nchi kwa maslahi yake ya kisiasa na viongozi wake.
Sisi ngome ya Vijana wa Chama cha ACT Wazalendo tunaunga mkono maazimio haya tukiwa tunatambua kuwa
 Kuathirika kwa namna yoyote kwa uchumi wa nchi ni kuathirika kwa maisha ya vijana wa kitanzania wanaotegemea fursa  za kiuchumi kwa ajili ya kujipanga kimaisha
 Tunaunga mkono maazimio ya kamati kuu ya Chama chetu cha ACT Wazalendo na kumtaka Rais Magufuli, atambue umuhimu wa wataalamu wanaomshauri katika masuala mbali mbali ya kiuongozi kwa kuwa kutokufanya hivyo kutajenga dhana kwa vijana wa sasa kuona hakuna haja ya kuwa wataalam wa masuala mbali mbali kwa sababu ya mtu mmoja kuamua kuwadhalilisha wataalamu wetu waliosomeshwa kwa kodi mbali mbali zilizochangwa na wazazi wetu,. Tunatambua kuwa kuathirika kwa namna yoyote kwa uchumi wa nchi kutazalisha wimbi kubwa la ukosefu wa ajira huku vijana wakiwa ni waathirika wakubwa
 Kuathirika kwa vijana kwa sababu ya Uchumi kuyumba kutazalisha makundi ya kihalifu ndani ya nchi na walengwa wakuu wa uhalifu huo watakuwa ni vijana

3 Umoja wa Kitaifa
   Kamati kuu ya Chama cha ACT Wazalendo ilitambua kuwa nchi yetu imefanya juhudi kubwa katika miaka 50 iliyopita katika kujenga umoja na mshikamano wa kitaifa kwa kuhakikisha kuwa makabila, dini na baadaye vyama vya siasa tunaishi bila kukamiana wala kuhasimiana. Juhudi za dhati za kupambana na ubaguzi ndiyo umekuwa msingi imara wa kujenga Umoja wa Kitaifa na amani tunayojivunia. 

Hata hivyo, Kamati Kuu imezingatia kuwa utawala mpya wa Serikali ya CCM, kupitia Mwenyekiti wake mpya na Rais wa Jamhuri wa Muungano, umeanza kwa juhudi na kasi kubwa kuchokonoa na kumomonyoa misingi ya utaifa na umoja wetu.
Kamati kuu ilieleza kuwa sasa nchi yetu inaye  Rais asiyechagua maneno na asiyejua aongee nini na wapi na kwa wakati gani nah ii ilitokana na Rais kuwadhalilisha vijana waliosoma kwa bidii katika mazingira ya shule zilizotelekezwa na serikali ya CCM akaamua kuwaita  VILAZA.

Pia Kamati kuu ikaeleza kuwa serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Magufuli  Katikati ya uhasama mkubwa wa kisiasa na kijamii huko Zanzibar ikaamua kwenda kuongeza majeraha yaliyosababishwa na serikali ya chama chake badala ya kwenda  kujaribu kutibu majeraha  yaliyosababishwa na kuchezewa kwa sanduku la kura, bali kuchochea uhasama chini ya ulinzi wa vyombo vyetu vya dola vyenye jukumu la kulinda na kudumisha amani.

Ikaeleza kuwa  Rais, kupitia kauli zake, ameanza kuubomoa muungano wetu uliojengwa kwa unyenyekevu na katika mazingira magumu. Kila asimamapo kuhutubia, jambo moja la kutarajiwa kutoka katika kinywa cha Rais wetu ni matamshi yanayodhoofisha nguzo fulani ya umoja, mshikamano na undugu wetu kama taifa.

Ikaeleza kuwa yote hayo yakitokea chama chake cha CCM ama kimekaa kimya au kinachekelea.ikasisitiza kuwa  Inasikitikitisha kwamba Chama kilichoasisiwa na Mwalimu Nyerere kinamruhusu kiongozi wake kubomoa misingi ya umoja wa kitaifa na kuchochea chuki katika jamii ya watanzania.  

Kamati kuu ikaeleza kuwa kwa kuzingatia mtikisiko mkubwa katika umoja na mshikamano wa kitaifa unaoendelea nchini, Kamati Kuu:
1) ililaani juhudi zinazofanywa na Serikali ya CCM kupitia Mwenyekiti wao za kuchochea chuki katika jamii ya watanzania na kubomoa misingi ya umoja wa kitaifa na amani ya nchi .

2) ilitoa wito kwa watanzania wote waipendao nchi yao kusimama kidete katika kulinda misingi ya nchi yetu na kukataa chuki inayoanza kujengwa na utawala wa CCM.
3) iltoa wito wa kipekee kwa viongozi wetu wa dini na wakuu wa nchi waliopita, hususani Mzee Ali Hassan Mwinyi, Mzee Benjamin Mkapa na Mzee Jakaya Mrisho Kikwete, pamoja na wazee wengine wanaoheshimika katika nchi yetu wavae ujasiri wa kumuonya Mwenyekiti wa CCM kuwa juhudi zake za kuchochea chuki katika jamii yetu ya watanzania zitasambaratisha Taifa letu.  
.
Kwa kuzingatia hayo yaliyoelezwa na kamati kuu sisi Ngome ya vijana wa Chama tunaunga mkono maazimio hayo na tunamtaka Rais Magufuli atambue kuwa
 Tanzania ni ya watanzania wote pasipo kujali vyama vyao dini zao, makabila yao au mahali watokako
 Tunamtaka Rais Magufuli atambue kuwa njia yoyote ya kuwafanya watanzania wasiotokana na chama chake kama sehemu ya watu wasio na haki ndani ya nchi hakitavumiliwa na kijana yeyote wa kizalendo na mwenye kujitambua.

 Tunamtaka Rais Magufuli atambue kuwa Chuki anazozipanda katika mioyo ya watanzania zitakuwa na athari kubwa kwa Taifa na sisi kama vijana hatutamruhusu alitekeleze jambo hilo kwa nafasi yake ya ukuu wa dola
 Mwisho tunamtaka Rais Magufulia atambue kuwa vijana wa kitanzania hawatakubali kugawanywa kwa maslahi ya kichama kikanda wala kikabila katika kupigania maslahi ya nchi na yeyote atakayesimamia jambo hilo awe ndani ya serikali yake au nje ya serikali atakuwa ni adui wa kwanza wa vijana wa kitanzania
Edna Sunga
Katibu Vijana Taifa ACT-Wazalendo
10 Septemba,2016.

No comments: