Monday, October 17, 2016

ATCL YATOA OFA YA MWEZI MMOJA KWA SAFARI ZA MWANZA.

imageNa Daudi Manongi-MAELEZO
Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) imetoa ofa ya mwezi mmoja kwa abira wanaosafiri kutoka Dar es salaam kwenda Mwanza kulipa nauli ya shilingi 160,000/- kwa safari moja.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es salaam na na Kaimu Afisa Mawasiliano wa Kampuni Bi.Lily Fungamtama wakati akiongea na Idara ya Habari.
Amesema Ndege za Kampuni zimeanza kutoa huduma kuanzia Jumamosi ya wiki iliyopita ya tarehe 15 ya mwezi huu kama ilivyobainisha kupitia vyombo vya Habari.
Safari hizo zilianza kwa kutoa huduma ya kusafirisha abiria kuelekea nchini Comoro na hapa nchini itoa safari katika mikoa ya Mwanza, Arusha na Kigoma.
Bi.Fungamtama amesema kwa kuanzia walianza na mazoezi ya vitendo kwa marubani na wafanyakazi wa ndani ya Ndege ambapo hatimaye walianza safari za biashara ya kusafirisha abiria mnamo tarehe 15 Oktoba kama ilivyopangwa.
Ameongeza kuwa ATCL imeboresha huduma zake kwa kiasi kikubwa kwa kuwapatia wateja wake ofa ya kubeba kilo 20 za mizigo na kilo 7 za mzigo wa mkononi bure   pamoja na kutoa vinywaji na ubadilishaji wa tiketi ni bure ndani ya mwezi.
Aidha, Kaimu Afisa Mawasiliano wa Kampuni Bi.Lily amekanusha taarifa potofu kuwa zimekwama kuanza safari zilizopangwa.
Amesema kuwa habari hizo sio za kweli kwani hivi sasa wameshaanza huduma katika mikoa hiyo mitatu.
Kampuni ya Ndege ya ATCL kwa sasa ina ndege tatu,zikiwemo mbili aina ya Dash8-Q400 zenye uwezo wa kubeba abiria 76 kila moja na Dash8-Q300 moja yenye uwezo wa kubeba  abiria 50.

No comments: