Hotuba ya Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo Ndugu Zitto Zuberi Kabwe kuhusu Hali ya Nchi iliyotolewa katika Mkutano wa Kwanza wa Kidemokrasia

   


Ndugu Mama Anna Elisha Mghwira, Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Wazalendo,
Ndugu Viongozi wote wa chama katika ngazi mbalimbali
Ndugu Wanachama
Ndugu wageni waalikwa
Ndugu wananchi
Mabibi na Mabwana

Karibuni Sana!


Ninayo furaha na heshima kubwa kusimama mbele yenu na kuhutubia kwa mara ya kwanza katika Mkutano wa Kwanza wa Kidemokrasia wa Chama chetu. Mkutano wa kidemokrasia ni kikao pekee rasmi cha kikatiba katika chama chetu ambapo viongozi na wanachama wanakutana ana kwa ana na kubadilisha mawazo kuhusu chama na maendeleo ya nchi yetu kwa ujumla. Aidha, katika mkutano huu tunawaalika wageni mbalimbali kutoka nchi na vyama marafiki kwa ajili ya kubadilisha uzoefu katika nyanja mbalimbali.

Mkutano wa Kidemokrasia ni kikao cha aina yake kwa kuwa wanachama na waalikwa wengine wanahudhuria kwa hiari yao na kwa gharama zao. Muhimu zaidi ni kwamba katika kikao hiki hata wananchi wasio wanachama wanakaribishwa kuhudhuria ili wasikilize na kushiriki kutoa maoni kuhusu mtazamo wa chama chetu kuhusu hali ya nchi yetu.
Tunajivunia muundo huu wa chama chenye kutoa fursa pana kwa wanachama na wananchi kushiriki kujenga na kuwa taswira sehemu ya chama. Ni chama pekee hapa nchini chenye muundo huu. Lengo la kuwa na muundo huu ni kutekeleza kwa vitendo imani yetu kwamba chama cha siasa ni mali ya wanachama na umma kwa ujumla.

Katika mkutano huu tutapata nafasi ya kusikia na kujadili mada mbalimbali zitakazowasilishwa na wadau wa maendeleo kutoka ndani na nje ya nchi yetu. Aidha Mwenyekiti wetu, mama Anna Mghwira, na mshauri wa chama chetu, Profesa Kitila Mkumbo, watatupitisha katika mambo ya msingi kuhusu chama chetu kuelekea mwaka 2020. Karibuni Sana tutafakari kwa pamoja.

Kwa mujibu wa Katiba ya Chama chetu, Kiongozi wa Chama anapaswa kutoa mtizamo wa chama chama kuhusu hali ya nchi na kutoa mwelekeo na msimamo wa kisera katika mambo mbalimbali yanayoikabili nchi kwa kipindi cha sasa na muda mrefu ujao. Ninatekeleza wajibu huu kupitia hotuba hii ya leo katika Mkutano huu.

Katika hotuba yangu, ninapitia historia ya maendeleo ya nchi yetu na kuelezea changamoto zinazotukabili na mtazamo wetu kisera ya namna ya kutatua changamoto hizo kupitia falsafa yetu ya Siasa ni Maendeleo.


Ujenzi wa Taifa ni Mradi Endelevu
Tanzania ina umri wa miaka 55 kama taifa lililo huru kutoka kwa wakoloni na miaka 52 kama Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Kufikia hatua ni matokeo ya mapambano dhidi ya ukoloni, ubaguzi, unyanyasaji, na unyonge (unaotokana na umaskini, ujinga na maradhi). Huu ni mradi wa ujenzi wa Taifa, ambao ni endelevu kutoka kizazi kimoja hadi kingine.

Katika miaka 52 ya mradi wa kujenga Taifa yapo mambo ya msingi ambayo tumejitambulisha nayo kama Taifa na ambayo viongozi, vyama vya siasa na kila mwananchi anawajibika kuvilinda na kuviendeleza. Haya ni mambo ambayo iliyokuwa Tume ya Mabadliko ya Katiba iliyaita TUNU.

TUNU hizi ni pamoja naUmoja wa wananchi na wa kitaifa uliojengwa katika msingi wa udugu bila kujadili dini, makabila wala eneo alilozaliwa mtu. Tunao Muungano wa Taifa moja linaloundwa na nchi mbili zilizoungana kwa hiari kwa maslahi mapana, na uliosimikwa katika misingi ya kisheria na kikatiba. Tuna Haki na Uhuru kama njia ya kulinda maslahi ya wanyonge ambao ni wengi. Tujitambulisha kwa Amani na Utulivu kama tunda la haki.

Pengine TUNU kubwa zaidi iliyotutambulisha, na inayoendelea kututambulisha, kama Taifa ni Maadili ya viongozi. Tulijitambulisha kuwa na viongozi walioishi maisha kama yetu na tukakaa nao mitaani na tukasoma na watoto wao katika shule, na tukapanga nao mstari tulipoenda kutibiwa katika hospitali za umma. Tulijitambulisha kwa kuwa na viongozi ambao waliogopa na kuikimbia rushwa. 

Tulijambulisha kwa Usawa, bila kujali nafasi ya mtu katika jamii. Tulithaminiana kwa UTUbadala ya mahali mtu alipozaliwa na mali alizokuwa nazo. Kipimo cha ubinadamu wa mtu ulikuwa ni UTU badala ya hali aliyo mtu na mahali atokoka. Kwa kifupi tulikuwa tunapambana kujenga na kuimarisha maendeleo ya binadamu (watu) badala ya maendeleo ya vitu. Roho ya TUNU zote hizi ilikuwa siasa ya Ujamaa na Kujitegemea.

Hata hivyo, katika miaka ya karibuni ya uhai wa Taifa letu tumeanza kuzimomonyoa baadhi ya TUNU za taifa letu. Kwanza, wengi wa viongozi waliofanya kazi na Mwalimu Nyerere walishindwa kuielewa au kuitafasiri falsafa ya Ujamaa na Kujitegemea. Badala yale, wasaidizi wa Mwalimu walijpanga kutelekeleza maelezo na maelekekezo yake bila tafakuri na bila kufuata taratibu ya kisera. Matokeo yake tukatengeza mazingira ya kuamini kwamba maono ya mwalimu ndiyo sera. Bahati pekee tuliyokuwa ni kwamba Mwalimu alikuwa na maono mapana na nchi iliweza kusimama hata kwa kutegemea mawazo pekee. Hata hivyo, imani potofu kwamba serikali ndiyo pekee iliyokuwa na uwezo kuendesha uchumi na nyanja zingine muhimu katika jamii ilikwaza sana maendeleo ya uchumi na kijamii.

Badala ya kurekebisha kasoro zilizojitokeza wakati wa utawala wa Mwalimu Nyerere, utawala uliofuata ulitelekeza kabisa falsafa ya Ujamaa na Kujitegemea. Mbaya zaidi ni kwamba baada ya kutelekeza falsafa hii hawakuja na mbadala. Matokeo yake sasa katika miongo zaidi ya mitatu Taifa letu limekuwa likiendeshwa bila falsafa. Ni kwa sababu hii tumeanza kushuhudia mmomonyoko wa tunu mama za Taifa. 

Tunashuhudia juhudi kubwa za kutafuta maendeleo ya vitu, badala ya maendeleo ya watu. Tunashuhudia ubaguzi wa dini, makabila na maeneo ukianza kuibuka, na katika siku za karibuni tunashuhudia ubaguzi wa ukabila wa kivyama vya siasa. Tumeanza kuamini na kuhubiri kwamba haiwezekani kujenga jamii iliyo sawa, na sasa tunaona ni jambo la kawaida kabisa kuwa na utengano katika utoaji wa huduma za jamii kati ya maskini na wenye kipato kikubwa. Kwa kifupi ule mradi wetu wa ujenzi wa taifa umetelekezwa na sasa tunaendesha nchi pasipo na dira ya muda mrefu. Tumeanza kuendesha nchi kama familia maskini inayoishi kutafuta chakula cha leo siku ipite bila kujali kesho itakuwaje.

Tumeanza kushuhudia, kuzoea na kukubaliana na viongozi wetu kuishi maisha tofauti na sisi. Tumeanza kushangaa tukiona kiongozi anatibiwa katika hospitali tunazitibiwa sisi, na tutamshangaa akipeleka mtoto wake katika shule tunazosoma sisi. Tukipanda daladala tutashtuka na kushangaa tukiona pembeni yetu yupo kiongozi tuliyemchagua wenyewe. Matokeo yake viongozi wetu wameanza kujibiidisha kuishi maisha yaliyo juu ya uwezo wao ili waonekane ni viongozi na kujikuta wanajitumbukiza katika maisha ya kutafuta mali kupitia nafasi zao za ungozi.

Hata tunu yetu ya UTU tumeanza kuimomonyoa. Tumeanza kujithamini mno wenyewe na kuacha ile dhana yetu kama kila binadamu ni ndugu yangu. Sasa imeanza kuwa kawaida kwa jirani yetu kushambuliwa na sisi tukabaki tunashangaa na kushindilia zaidi vitasa vya milango ili nasi tusivamiwe. Mwenzetu akivamiwa na vibaka barabarani badala ya kumsaidia tunapiga picha ili tuwe wa kwanza kusambaza katika mitandao ya kijamii. Inabidi tujiulize ilikuwaje ndugu yetu Said hata akapigwa na kutobolewa macho mchana kweupe huko Buguruni na sisi tuliokuwa naye tunamwangalia tu jambazi aliyemvamia? Iliwezekanaje kijiji kizima kinashuhudia na kushiriki kuchoma moto binadamu wenzao huko Chamwino? Walikuwa wapi walimu na wanafunzi huko Mbeya pale ambapo mwanafunzi alishushiwa kipigo na baadhi ya walimu? 

Imekuwaje tumeanza kuzoea vitendo vya kuchoma moto watu ambao tunawatuhumu kuwa vibaka? Haya ni maswali yanayohusu UTU ambayo sote tunapaswa kujiuliza na kuyajibu.
Katika hotuba aliyoitoa tarehe 16 Agosti 1990 wakati akizungumza na vijana Mjini Mwanza, pamoja na mambo mengine, Mwalimu Nyerere alisema maneno haya kuhusu kazi za chama cha siasa:

“Lengo [la chama chetu] lazima liendelee kuwa ni kuinua hali ya maisha ya kila mtu ili kila mtu aweze kupata huduma za msingi za elimu na matibabu. Kama watu wachache wanaishi maisha ya kifahari na watu walio wengi hawapati hata mahitaji yao ya lazima hatutaweza kamwe kudumisha utulivu nchini mwetu. Tanzania isikose kuacha kuchukua msimamo wake wa kuhakikisha uko usawa wa binadamu, kwa kuwa huu ni msingi muhimu katika hali ya maisha ya kila mtu na kwamba kuna heshima ya binadamu kwa kila raia wa Tanzania. Mimi siamini hata kidogo kwamba mnaweza kujenga amani na utulivu wa kudumu katika nchi maskini bila kuheshimu misingi ya haki na usawa. Na unyang’au kwa hulka yake hauheshimu misingi ya haki na uswa”.

Chama chetu kimeunda katika imani ya maneno haya ya Mwalimu. Ni kwa sababu hii tamko la awali kabisa katika kuanzishwa kwa chama chetu ilikuwa ni kurudisha nchi katika misingi ya kuasisiwa kwake. Misingi hii ni hiyo niliyoieleza hapo juu na ambayo tumeitafsiri na kuianisha katika katiba yetu kuwa ni misingi kumi ya chama. Wenzangu wataifafanua zaidi baadaye katika Mkutano huu.

Sisi katika chama chetu cha Wazalendo tunaaminini kwamba Siasa ni Maendeleo. Hii ndiyo falsafa inayoongoza sera na programu za chama. Tunaamini kwamba chama cha siasa lazima kijihusishe kikamilifu na kuinua hali za maisha ya watu, kikiwa ndani au nje ya serikali. Hapa chini ninafafanua baadhi ya maeneo muhimu yanayoanisha falsafa yetu ya siasa ni maendeleo. 

Siasa ni Maendeleo
Mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi
Katika kikao chake maalumu kilichofanyika mwezi Juni 2015 Mjini Tabora, Halmashauri Kuu ya Chama cha Wazalendo ilijadili na kupitisha Azimio la Tabora. Azimio hili linafafanua na kutoa mwongozo kuhusu utekelezaji wa Itikadi ya Ujamaa wa Kidemokrasia. Katika kikao hiki tulianisha changamoto nne kubwa zinalikabili taifa letu na ambazo zinahatarisha misingi ya taifa ambayo nimeieleza hapo juu.
Changamoto tulizozitaja katika kikao cha Halmashauri Kuu ni rushwa na ufisadi; uchumi usiozalisha ajira na kutokomeza umaskini; huduma duni za jamii hususani elimu, afya na maji; na kuanza kushamiri kwa vitendo vya kibaguzi wa kidini na kikabila. Ilani ya Uchaguzi wa mwaka 2015 ililenga kukabiliana na changamoto hizi.

Ni kwa sababu hii tuliweza kuunga mkono mara moja na bila kusita hatua za awali za Rais John Magufuli za kupambana na vitendo vya rushwa na ufisadi katika utumishi wa umma. Bado tunaendelea kumuunga mkono Rais katika juhudi zake za kuangamiza rushwa na ufisadi katika utumishi wa umma.
Hata hivyo tunasisitiza tena kwamba vita dhidi ya rushwa na ufisadi lazima ifanywe kwa kuzingatia misingi ya haki, utu na usawa. Tunasistiza kwamba hakuna mbadala katika kutafuta haki na kujenga utawala wa sheria. 

Ndiyo maana, tunamhimiza Rais na serikali yake wahakikishe kwamba watumishi wote wa umma 134 waliosimamishwa kazi hadi kufikia mwezi Agosti mwaka huu wanatendewa haki kwa kufikishwa katika vyombo husika vya kinidhamu na sheria ili ukweli kuhusu tuhuma zao ujulikane na hatua stahiki zichukuliwe. Lazima tujiepushe na vitendo vyovyote vya kuhukumu watu kwa vigezo vya tuhuma. Kuminya haki, usawa na utu huzaa jamii ya wakatili inayoweza kujichukulia sheria mkononi. Lazima kama taifa tuhakikishe kwamba tunadumisha utawala wa sheria katika nchi yetu.
Aidha, tunamkumbusha Rais kwamba kuna viporo vya ufisadi ambavyo anapaswa kuvishughulikia.

 Viporo hivi ni pamoja suala la Tegeta Escrow. Bado mtambo wa kufua umeme wa IPTL upo chini ya matapeli na kila mwezi Serikali inawalipa matapeli hao zaidi ya shilingi bilioni 8 (wazalishe au wasizalishe umeme).
Upo pia ufisadi mkubwa kuhusu HatiFungani ya dola za kimarekani 600 milioni (sawa na trilioni 1.3) uliotokea katika Benki ya Standard ya Uingereza.Tunatambua kuwa kuna watu tayari wamefikishwa mahakamani kwa rushwa ya dola 6 milioni (sawa na shilingi 13 bilioni). Lakini Serikali imefikisha mahakamani inaowaita madalali wa rushwa hiyo tu. Walioitoa rushwa hiyo - Benki ya Standard ya Uingereza haipo mahakamani. Waliopokea rushwa hiyo - maafisa waWizara ya Fedha na Uchumi hawapo mahakamani. HatiFungani hii ambayo Serikali imeanza kulipa riba yake ni ghali mno na imeongeza Deni la Taifa kwa kiwango cha shilingi 1.3 trilioni bila ya riba. Itakapofika mwaka 2020 ambapo tutakuwa tumemaliza kulipa deni hili, tutakuwa tumelipa zaidi ya shilingi 1.9 trilioni, shilingi bilioni 600 zaidi!

TunamshauriRais wetu atuongoze Watanzania kukataa mikopo ya namna hii ambayo inafukarisha nchi. Ni muhimu kabisa TAKUKURU wawachukulie hatua watu wote waliofaidika na bilioni 600 zaidi tutakazolipa katika deni hili.Kwa mifano hii miwili utaona kwamba, pamoja na nia na juhudi kubwa zinazoendelea katika kupambana na ufisadi, bado serikali inapapasa na haijagusa ufisadi ulioitesa nchi kwa muda mrefu, hasa katika kupambana na mafisadi wenyewe. Hadi sasa juhudi za Rais zimeishia kupambana na mawakala wa ufisadi waliopo serikalini lakini bado hajaanza kupambana na mafisadi wenyewe.


Uchumi shirikishi
Katika sera yetu ya uchumi shirikishi unaozalisha ajira nyingi na bora tulisisitiza haja ya kuchukua hatua mahususi kuhakikisha kwamba tunapanua wigo wa ajira bora katika maneneo ya viwanda na sekta ya huduma. Tulieleza na tunaendelea kueleza umuhimu wa kuharakisha miundo mbinu ya huduma mbalimbali vijijini ili kuwavuta vijana kushiriki shughuli za uzalishaji katika viwanda vidogo vidogo na sekta ya huduma. Kutokana na ufinyu wa viwanda na sekta ya huduma, watanzania wengi (75%) bado wamejiajiri katika sekta ya kilimo ambayo nayo inafanyika katika mazingira duni na uzalishaji hafifu. Ni kwa sababu hii, pamoja na uchumi kukua kitakwimu, bado wananchi wetu walio wengi wanaishi katika dimbwi la ufukara. Hili halikubaliki na lazima tutoke hapa tulipo.

Sisi wachumi tunaweza kubishana juu ya hali ya ukuaji wa uchumi nchini kwa kutumia takwimu za kitaalamu. Hatutarajii katika mazingira yetu ya kisiasa na utawala wa leo watalaamu wa serikali watoe takwimu zitakazoonyesha kwamba hali ya uchumi si njema. Hata hivyo, kwa mwananchi wa kawaida cha muhimu kwake sio takwimu za kiuchumi zilizopo katika nyaraka rasmi za serikali. Kilicho muhimu kwa mwananchi wa kawaida ni kipato na uwezo wa kipato hicho katika kumudu mahitaji muhimu ya kibinadamu na huduma nyingine muhimu za kijamii. Kigezo rahisi cha kujua kipato cha mtanzania ni kuangalia hali ya ajira katika sekta iliyo rasmi na isiyo rasmi kwa kuwa ajira ndiyo chanzo cha uhakika cha kipato duniani, na hasa kwa kuangalia ajira miongoni mwa vijana wenye umri kati ya miaka 15-35. Hili halina ubishi na wachumi wote wanakubaliana hivyo.

Kwa mujibu wa takwimu za nguvu kazi nchini ambazo hutolewa na Shirika la Takwimu la Taifa (NBS), hadi mwaka 2014, idadi ya vijana wenye umri kati ya miaka 15-35 nchini Tanzania walikuwa milioni 14.8 ambapo milioni 12.5 (84.5%) kati ya hawa walikuwa na nguvu za kufanya kazi. Kati ya idadi ya vijana wenye uwezo wa kufanya kazi, milioni 11 (88.3%) walikuwa wameajiriwa katika sekta mbalimbali, rasmi na zisizo rasmi.

Hata hivyo, kwa mujibu wa matokeo wa utafiti wa ajira na kipato katika sekta rasmi wa mwaka 2014 uliofanywa na NBS, idadi ya watu wote waliojiriwa katika sekta rasmi nchini Tanzania hadi mwaka 2014 walikuwa2,141,351. Hii ni sawa na asilimia 14.2 ya watu wote wenye nguvu za kufanya kazi nchini Tanzania au sawa na asilimia 19.1% ya watu wote walioajiriwa. Ndiyo kusema zaidi ya asilimia 80 ya watu wote wanaofanya kazi Tanzania wapo katika sekta isiyo rasmi.

Idadi ya wanawake walioajiriwa katika sekta rasmi ni ndogo sana ukilinganisha na idadi ya wanaume. Kwa mujibu wa utafiti wa NBS, watu wawili kati ya watatu (64.7%) waliojiriwa katika sekta rasmi ni wanaume. Ndiyo kusema mfumo wa ajira katika sekta rasmi nchini Tanzania bado unatawaliwa na mfumo dume. Wapigania haki za usawa wa kijinsia tunapaswa kuelekeza macho zaidi katika eneo hili pengine kuliko hata katika nafasi za kisiasa.

Mbali na jinsia, ajira nyingi katika sekta rasmi zipo Dar es Salaam na mikoa mingine mikubwa. Kwa mfano, pamoja na kwamba Dar es Salaam inachukua asilimia 10 ya idadi ya watu nchini, theluthi moja (33.6%) ya watu wote walioajiriwa katika sekta binafsi wapo Dar es Salaam. Hii ina maana kuwa katika watu watatu wanaojiriwa nchini, mtu moja anaajiriwe Dar es Salaam.

Ili kufikia uchumi wa kati ni lazima idadi ya watu wanaofanya kazi katika sekta rasmi wafikie angalau asilimia isiyopungua 50. Aidha, moja ya viashiria vya malengo endelevu ya maendeleo (Sustainable Development Goals-SDGs) ni kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2030, watu wote, wanawake na wanaume, wenye uwezo wa kufanya kazi wawe katika ajira rasmi na yenye staha. Kwa kuangalia uwezo wetu wa kuzalisha ajira kwa mwaka kufikia malengo haya ni changamoto kubwa. Kwa mfano, katika kipindi chote cha urais wa Ndugu Jakaya Kikwete tuliweza kutengeneza ajira 2,854,237 pekee pamoja na kwamba ilani ya CCM ya mwaka 2005 iliahidi kutengeneza ajira milioni moja kila mwaka! Hii inamaanisha kuwa serikali ya CCM ilitekeleza asilimia 20 tu ya lengo lake katika kuzalisha ajira! Tunahitaji kuongeza juhudu zaidi katika kuwekeza katika maeneo yanayoweza kuchochea ajira kwa vijana.

Ili kupanua wigo wa ajira nchini, katika ilani ya mwaka 2015, Chama cha Wazalendo kilipendekza uwekezaji katika maeneo makubwa matatu. Mosi, tulipendekeza kuwekeza katika kufufua na kuanzisha viwanda vya uzalishaji bidhaa zitokanazo na mazao ya kilimo na mifugo. Ili kuchochea uwekezaji katika viwanda vya uzalishaji, tulipendekeza kuwekautaratibu wa kisheria wa kutoa ruzuku ya gharama za umeme kwa viwanda vinavyozalisha bidhaa za matumizi muhimu ya wananchi kama sukari ili kuvifanya vishindane na tishio la bidhaa hizo kutoka nje ya nchi na kulinda ajira za Watanzania. 

Aidha tulipendekeza kuwa na utaratibu maalumu wa kisheria utakaohakikisha kwamba bidhaa na huduma zinazozalishwa nchini zinatumiwa na serikali na taasisi zake. Kwa mfano, tulipendekeza kwamba ofisi za serikali hazitaruhusiwa kutumia samani na bidhaa za nje kama bidhaa hizo zinaweza kuzalishwa hapa nchini.

Tunatambua kuwa serikali ya Rais Magufuli imeweka mkazo katika kujenga viwanda. Hili ni jambo jema kwa kuwa likitekelezwa vizuri litachochea ukuaji wa ajira kwa vijana nchini. Hata hivyo, pamoja na nia njema, haielekei kwamba serikali ya CCM inaelewa namna ya kutelekeleza lengo hili zuri. Kutokana na mkanganyiko wa kifalsafa, serikali haijui ni nani hasa anapaswa kujenga viwanda kati ya serikali yenyewe na sekta binafsi. Matokeo yake imekuwa ikivizia miradi ya sekta binafsi na kukimbilia kuizindua wakati huo huo serikali ikitoa kauli ambazo zinarudisha nyuma ari ya wafanyabiashara wazalendo kuwekeza katika viwanda.

Kwa mujibu wa siasa yetu ya ujamaa wa kidemokrasia, kwa hali yetu ya uchumi na kiwango cha sekta binafsi, ni lazima kuweka ushirika wa uhakika na kirafiki kati ya serikali na sekta binafsi katika uwekezaji wa viwanda. Kwa mfano, ni vigumu katika hatua za awali kwa sekta binafsi kuwekeza katika viwanda vya uzalishaji wa mazao ya kilimo kama vile viwanda vya nguo. Katika mazingira haya ni muhimu kwa serikali kuwekeza yenyewe moja kwa moja au kuweka mazingira maalumu kwa sekta binafsi kufanya hivyo.

Hatua ya pili katika kuchochea ukuaji wa ajira nchini ni kuwekeza katika elimu ya ufundi. Kwa mujibu wa utafiti wa mwaka 2014 kuhusu hali ya kuajirika kwa wahitimu wa vyuo vikuu uliofanywa na Taasisi ya Vyuo Vikuu Afrika Mashariki, ni asilimia 39 tu ya vijana wanaomaliza katika vyuo vya elimu ya nchini ndio wenye maarifa na stadi za kuajirika. Ndiyo kusema elimu yetu bado ni ya kitaaluma mno na haijajikita katika kuwapa wahitimu maarifa na stadi za msingi za kupambana katika ulimwengu wa ushindani wa kazi. Ili kuondokana na hali ni muhimu kuchukua hatua ya kuimarisha elimu ya ufundi ili vijana wengi zaidi waweze kupata maarifa muhumu.

Hatua ya tatu muhimu katika kuzalisha ajira ni uwekezaji katika sekta ya Utalii ambayo kwa kiasi kikubwa inazalisha ajira kwenye sekta za usafirishaji, malazi na huduma za vyakula. Sekta ya Utalii ndiyo sekta inayoongoza katika kuchangia Mapato ya kigeni nchini. Kwa takwimu zilizopo, utalii ulliingizia nchi jumla ya Dola za Kimarekani 2.1 bilioni kufikia Agosti 2016. Ikumbukwe kuwa kila mtalii anayeingia nchini anatarajiwa kula, kulala na kusafiri na yote hayo ni huduma zinazotolewa na watanzania wanaoajiriwa kwenye mahoteli na magari ya watalii.
Hata hivyo Serikali ya Awamu ya Tano katika Bajeti yake ya kwanza kabisa imeamua kurudisha nyuma juhudi zote za kukuza Sekta ya Utalii kwa kuanzisha kodi ya VAT kwenye huduma zote za Utalii. Pamoja na kwamba bado ni mapema kutathimini athari za kodi hii katika maendeleo ya utalii, wataalamu wa utalii wamekwisha onya kwamba kodi hii inaweza kuifanya Tanzania kuwa ghali kuliko majiranizake katika kuvutia watalii.
Kwa Ujumla Bajeti ya mwaka 2016/17 sio rafiki katika kuchochea ukuaji wa ajira. Katika miezi sita ya kwanza ya utekelezaji wa bajeti ya serikali, tayari tunashuhudia baadhi ya waajiri kuanza kupunguza wafanyakazi katika hatua za kubana matumizi. Hali itakuwa mbaya zaidi kwa wenye mahoteli na miji kama Arusha itaumia zaidi kwani inategemea sana Biashara ya Utalii. Kuanguka kwa sekta ya Utalii ni kuanguka kwa uchumi wa nchi kwa ujumla. Tutaendelea kumbana Waziri wa Fedha afuatilie kwa karibu maendeleo ya utalii katika kipindi hiki cha bajeti ili kufuatilia kwa umakini athari zinazoweza kujitokeza kutokana na hatua mpya za kodi tulizozieleza hapo juu.
Pamoja na udhaifu wa wazi katika eneo la utalii, jambo moja la kupongeza sana katika Bajeti ya mwaka 2016/17 ni uwekezaji mkubwa katika kuondoa changamoto ya miundombinu. Wenye Viwanda wengi wamekuwa wakilalamika kuhusu kutokuwepo kwa umeme wa uhakika, gharama kubwa za usafirishaji wa malighafi na bidhaa na mawasiliano ya intaneti yasiyo na kasi ya kutosha. Katika Bajeti ya mwaka 2016/17 Serikali imeelekeza rasilimali nyingi sana kujibu changamoto hizo. Kwa mfano, Bajeti za Miundombinu ya Usafirishaji na Umeme zimechukua 53% ya Bajeti yote ya Maendeleo. Jumla ya shilingi 6.2 trilioni ya Bajeti imetengwa kwa ajili ya miradi ya miundombinu na umeme. Huu ni mwelekeo mzuri katika kujibu changamoto hizo na tunatarajia kwamba hatua hii itachochea wawekezaji kuwekeza katika sekta ya viwanda.

Elimu Bora kwa Wote
ACT Wazalendo inaamini kwamba elimu ndiyo uti wa mgongo wa maendeleo ya nchi. Ujinga una gharama kubwa mno katika nchi. Vitendo vingi vya hovyo tunavyovishuhudia katika siku za karibuni kama vile kuchoma watu moto ni tunda la ujinga unaotokana na elimu duni. Aidha, tafiti zinaonyesha kuwa nchi nyingi zinazopiga hatua kubwa katika maendeledo ya uchumi ni zile ambazo zimewekeza katika kutoa elimu bora kwa wananchi walio wengi. Kwa hiyo hakuna mbadala wa elimu katika maendeleo ya nchi na mtu yeyote akisema anataleta maendeleo bila kuwekeza katika elimu mtu huyo atakuwa anadanganya.
Elimu ina sura mbili kubwa. Kwanza, ni watoto kwenda shule. Katika hili, lazima kukiri kwamba nchi yetu ni moja ya nchi katika Jangwa la Sahara ambazo zimewekeza sana katika kupanua fursa za elimu na kuhakikisha kwamba watoto wengi wanajiunga na mfumo wa elimu. Kwa mfano, katika kipindi cha miaka 10 kutoka mwaka 2005 hadi 2015, kiwango cha udahili katika za shule za sekondari imeongezeka kutoka wanafunzi 524,325 mwaka 2005 hadi wanafunzi 1,806,958 mwaka 2015, ikiwa ni ongezeko la asilimia 244.6% katika kipindi cha miaka kumi. Aidha, kiwango cha udahili katika elimu ya juu kimeongezeka kutoka wanafunzi 40,000 tu mwaka 2005 hadi kufikia zaidi la laki tatu mwaka jana. Elimu ya juu imepanuka nchini kwa kiwango ambacho baadhi ya vyuo vinakosa wanafunzi. Kwa mujibu wa takwimu za Tume ya Vyuo Vikuu, mwaka jana zaidi ya nafasi 30,000 zilibaki bila kujazwa katika vyuo vikuu kwa sababu ya kukosa wanafunzi wenye sifa. Pamoja na kwamba idadi ya watanzania wenye elimu ya juu bado ni ndogo sana (asilimia 6 pekee), juhudi kubwa zimefanyika katika miaka ya hivi karibuni.
Sura ya pili ya elimu ni kujifunza. Hapa ndipo palipo na changamotio kubwa. Kwenda shule sio sawa na kujifunza. Tafiti zinaonyesha kwamba idadi kubwa ya wanafunzi wanaopita katika mfumo wa elimu Tanzania wanamaliza shule wakiwa mbumbumbu. Kwa mfano, utafiti wa miaka kadhaa wa Shirika la Uwezo unaonyesha kwamba watoto watatu kati ya kumi wa Darasa la Tatu hawawezi kumudu kufanya mahesabu ya Darasa la pili. Aidha, takribani mwanafunzi mmoja kati ya wanne (25%) waliopo Darasa la Saba hawawezi kufanya mahesabu ya Darasa la Pili.
Aidha, uchambuzi wa matokeo ya mitihani ya kidato cha nne unaonyesha kwamba wahitimu wengi wanafeli mitihani ya mwisho. Kwa kipindi cha takribani miaka mitano iliyopita, chini ya asilimia 10 ya wanafunzi wanaomaliza Kidato cha Nne wanafaulu kwa kiwango cha Darasa la I hadi la III. Ndiyo kusema asilimia karibu 90 wanapata Daraja la Nne au wanafeli. Kwa mfumo wetu wa elimu hawa hawawezi kuendelea na ngazi yoyote rasmi ya elimu. Na kutokana na udhaifu katika elimu ya ufundi ina maana kuwa wanaingia mitaani wakiwa hawana maarifa na stadi muhimu za kujiajiri au kuajiriwa.
Hatua nyingi ambazo serikali inachukua katika sekta ya elimu zinalenga katika kuongeza idadi ya wanafunzi, lakini sio kuboresha ubora wa elimu. Tumesikia sana kauli kuhusu elimu bure. Tumesikia sana kuhusu kuongeza madawati. Pamoja na umuhimu wake, ukweli ni kwamba hatua hizi hazitasaidia kuongeza kiwango cha ubora wa elimu yetu.
Tafiti zinaonyesha kwamba ili kuboresha ubora wa elimu kitu kikubwa na cha msingi kabisa kuliko vyote ni kuwekeza kwa walimu na taaluma ya ualimu. Maeneo muhimu ni mafunzo ya walimu na kuhakikisha kwamba wanakuwa na motisha wa kutosha katika kufanya kazi zao. Bahati mbaya hapa Tanzania serikali na jamii kwa ujumla hatuthamini kazi ya ualimu. Taaluma ya ualimu imekuwa ni daraja la kujiokoa baada ya kukosa sehemu zingine. Walimu wetu wanaofundisha katika mazingira magumu sana hatuwathamini na wakati mwingine hata tunawabeza.
Kwa kuzingatia ushahidi wa kisayansi unaonyesha kuwa walimu ndio msingi mkuu wa kujifunza na kuboresha elimu, Chama chetu kinahimiza kuwekeza katika kuweka mfumo imara wa motisha na uwajibikaji kwa walimu. Tunasisitiza kuwekeza katika mafunzo ya walimu na kuhakikisha kwamba walimu wanalipwa kwa kiwango ambacho kitawawezesha kukabiliana na maisha huko walipo. Aidha, tafiti zinaonyesha kwamba walimu walio vijijini wanaishi katika maisha magumu sana hasa ya kukosa makazi yenye staha.
Ili kuwa na utatuzi endelevu wa matatizo ya walimu na kuchochea motisha wa kujiunga na taaluma ya ualimu, chama chetu kinapendekeza tuwe na mfumo mpya maalumu wa ajira ya walimu katika utumishi wa umma. Hii ni muhimu tukizingatia kwamba takribani nusu ya watumishi wote wa umma wapo katika sekta ya elimu. Hatua hii itawezesha kuwa na bajeti maalumu ya walimu. Aidha, hatua hii itawezesha kuwa na mfuko maalumu wa walimu ambao unaweza kutumika katika kutoa motisha maalumu kwa wale walimu wanaofanya kazi katika mazingira magumu na ambao wanaonyesha juhudi zaidi katika kufanikisha wanafunzi kujifunza.
Swala la mwisho ambalo ningependa kulizungumzia kwa leo kuhusu elimu ni lugha ya kufundishia, ambayo ni nyenzo muhimu katika kujifunza. Tafiti zinaonyesha kwamba mtoto hujifunza vizuri zaidi kama atatumia lugha anayotumia nyumbani katika kujifunza darasani.
Nchini kwetu tunatumia lugha mbili katika elimu, ambazo ni Kiswahili na Kiingereza. Kiswahili hutumika katika ngazi ya awali hadi msingi na Kiingereza hutumika kuanzia ngazi ya sekondari hadi elimu ya juu. Hata hivyo, sera mpya ya elimu inatoa nafasi kwa lugha zote mbili kutumika katika ngazi zote za elimu. Hii ni hatua muhumu pamoja na kwamba serikali haijatoa utaratibu wa kueleweka jinsi ya kutumia mfumo huu.
Sisi kama chama tunaamini kwamba Tanzania imebarikiwa katika bara la Afrika kwa kuwa na lugha mbili rasmi. Hata hivyo, ukweli ni kwamba kutokana na mazingira duni ya kujifunza lugha ya Kiingereza watanzania wengi hawamudu lugha hii na imekuwa kikwazo katika kujifunza. Katika kutatua changamoto ya lugha ya kujifunza nchini msimamo wetu ni kuwa na mfumo pacha wa lugha ya kufundishia yaani Bilingual Education System. Katika mfumo huu, Kiswahili na Kiingereza vitatumika sambamba kama lugha za kutoa na kutafuta maarifa. Ndiyo kusema kwamba vitabu na nyenzo zingine za kujifunzia zitakuwepo katika lugha zote. Aidha, wanafunzi watakuwa na uhuru wa kuchagua kujibu mitihani kwa kutumia lugha ya Kiswahili na Kiingereza. Lengo ni kuhakikisha kwamba lugha haiwi kikwazo katika kujifunza na kuhakikisha kwamba watanzania wengi wanaimudu lugha ya Kiingereza kama lugha ya mawasiliano na kujifunzia, sambamba na lugha ya Kiswahili.
Tunatambua uhaba mkubwa wa walimu wa Kiingereza na Sayansi katika shule zetu. Takwimu za serikali zinaonyesha kwamba kuna upungufu wa walimu zaidi ya elfu ishrini. Aidha walimu waliopo wa Kiingereza sio wa kiwango stahiki na hawapati mafunzo ya kutosha wawapo kazini. Katika kukabiliana na tatizo la walimu wa Kiingereza tunapendekeza, kama hatua za dharura na za muda mfupi, serikali iweke mazingira rafiki kwa ajili ya kuvutia walimu kutoka nchi zingine za Afrika kuja kufundisha somo la Kiingereza wakati huu sisi nasi tukiwahimiza na kuwakea mazingira wezeshi walimu wetu wa Kiswahili kwenda kufundisha nje za nchi. Kwa mfano, tunaweza kundoa ada ya ukaazi (resident permit fees) kwa walimu wa Kiingereza kutoka nchi jirani za Afrika Mashariki na Kusini kwa kipindi maalumu kama vile mika kumi, wakati huo tukiwekeza katika mafunzo ya walimu nchini.Hali ya siasa
Kikatiba, nchi yetu inafuata mfumo wa demokrasia ya vyama vingi. Katiba na Sheria mbalimbali zimeanisha utaratibu wa kazi na shughuli za vyama vya siasa. Ili kuhakikisha kwamba kazi na shughuli za vyama vya siasa zinakuwa endelevu, vyama vyenye kukidhi vigezo hupewa ruzuku kupitia Bajeti ya Serikali inayopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano Tanzania.
Aidha, kuimarisha demokrasia ya vyama vingi ni moja ya vigezo tulivyojiwekea kama nchi katika Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025, pamoja na matamko mbalimbali ya kisera za maendeleo. Nchi yetu inatambua kwamba uimara wa demokrasia ya vyama vingi na utawala wa sheria ni nguzo muhimu katika kuendeleza na kudumisha amani ya nchi na watu wake.
Hata hivyo, katika awamu hii ya tano, Serikali ya Chama cha Mapinduzi imeamua kuzuia shughuli za siasa kwa kutumia nguvu ya Jeshi la Polisi na hata Jeshi la Wananchi. Kwa mujibu wa serikali ya CCM, shughuli za kiuenezi za vyama vya siasa kama vile mikutano ya hadhara, maandamano, makongamano, na mijadala mingine ya aina hiyo inapaswa kukoma mapema baada ya uchaguzi. Tunaendeleza kusisitiza kuwa, kisheria, huu ni uvunjifu wa Katiba na Sheria za nchi. Aidha, utafiti wa hivi karibuni uliofanywa na Taasisi ya Twaweza unaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 80 ya wananchi wanataka demokrasia ya vyama vingi kudumishwa. Kiongozi yeyote au chama chochote kinachojaribu kuchezea mfumo wa vyama vingi anajaribu kuchezea matakwa ya watanzania walio wengi. Anacheza na moja ya tunu muhimu ya nchi.
Sisi kama chama tunasisitiza kwamba wananchi lazima wawe na uhuru wa kuikosoa Serikali. Vyama vya siasa vina haki ya kufanya mikutano, kupata taarifa na kushawishi wananchi kuviunga mkono. Haki hiyo bila ya haki ya kufanya mikutano ni haki butu. Ndio maana tumeendelea kuitaka Serikali kutoweka vizingiti vya vyama kufanya shughuli zao za kisiasa. Sisi ACT Wazalendo tumeendelea kusisitiza haki na wajibu wetu kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Aidha, sisi kama chama, tunaendelea kusisitiza kwamba uchaguzi wa Zanzibar wa mwaka jana ulichezewa na viongozi waliopatikana hawana uhalali wa kisiasa. Tunasisitiza kwamba ili kuleta uhalali wa kisiasa kwa utawala wa Zanzibar, na ili kurudisha na kudumisha maridhiano miongoni mwa jamii, ni muhimu pande mbili za upinzani na Chama cha Mapinduzi kuzungumza na kukubaliana namna ya kwenda mbele. Kufumbia tatizo hili ni kujaribu kufukia moto unaowaka chini kwa chini. Tunarudia tena kuwa Rais Magufuli hana namna ya kukwepa tatizo la Zanzibar. Tatizo lililopo ni tatizo la kisiasa na utatuzi wake lazima uwe wa kisiasa na sio mabavu ya kijeshi.
Hali ya kisiasa inayoendelea nchini tunapaswa kuiona katika picha pana ya bara zima la Afrika. Tunashuhudia wimbi la kuanza tena kuchezea sanduku la kura katika nchi nyingi za Afrika mithili ya tulichokishuhudia miaka ya 1960 mara baada ya uhuru.Tunashuhudia uvunjwaji mkubwa wa haki za binadamu katika mataifa ya Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Sudani ya Kusini na Ethiopia. Machafuko yote haya yanasababishwa na kupuuzwa kwa haki za kiraia na kidemokrasia.
Tunatoa wito maalumu kwa taasisi za kiraia, taasisi za dini na vyuo vikuu katika bara la Afrika kusimama imara katika kulinda utawala wa sheria na demokrasia ya vyama vingi. Tunazitaja taasisi hizi kwa sababu kazi zao na uwepo wao unategemea sana uwepo wa demokrasia katika nchi yoyote duniani. Demokrasia ya vingi ikichezewa na hatimaye kufififshwa taasisi za kiraia, taasisi za dini na vyuo vikuu haviwezi pia kuwa na uwezo wa kufanya kazi zao kwa uhuru.
Chama chetu kinamtaka Rais wa Jamhuri ya KIdemokrasia ya Kongo Joseph Kabila aheshimu Katiba ya nchi hiyo na kuruhusu uchaguzi kufanyika kama ilivyopangwa ili kuwezesha mpito wa kidemokrasia kwa amani kabisa. Tanzania haiwezi kuendelea kupokea wakimbizi wa kongo kwa makosa ya wanasiasa wanaong’ang’ania madaraka kinyume na katiba.
Huko Ethiopia tunaitaka Jumuiya ya Kimataifa kuingilia kati haki za wananchi na kuzuia Serikali ya nchi hiyo kuendelea kuua raia wasio na hatia. Mafanikio makubwa ambayo Serikali ya Ethiopia imeyatapata katika maendeleo ya nchi hiyo hasa miundombinu yametokana na kuhakikisha amani kwa muda mrefu. Hivyo tunaishauri serikali ya nchi hiyo ilinde mafanikio hayo kwa kutoa uhuru wa kisiasa kwa wananchi wake bila ubaguzi wowote. Afrika ya sasa lazima iwe ni Afrika ya maendeleo na sio Afrika ya vita na mauaji ya raia. Hatutaki kurudi tena enzi za kina Bokasa, Mobutu, Idi Amini na Mengistu. Tunataka Afrika inayolinda uhai na kuendeleza raia wake


Hitimisho
Kupitia falsafa yetu ya siasa ni maendeleo, tutaendelea kutoa mapendekezo juu ya namna ya kutatua changamoto mbalimbali na kushiriki kwa vitendo katika kutatua changamoto hizo kabla na baada ya kuunda serikali.
Sisi kama chama cha siasa, tunaendelea kusisitiza kuwa tutaunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano katika kupambana na ufisadi na kujenga uwajibikaji nchini. Aidha tunaendelea kusisitiza dhamira yetu ya kujitoa mhanga katika kulinda demokrasia ya mfumo wa vyama vingi nchini. Tunaamini kwa dhati kabisa kuwa kuheshimu na kulinda demokrasia na kuzingatia utawala wa sheria nidyo msingi wa mapambano dhidi ya ufisadi.
Sisi kama chama tunaamini, na tafiti zinaonyesha hivyo, kwamba demokrasia na kuzingatiwa kwa utawala wa sheria na haki za binadamu ndiyo msingi wa maendeleo ya kiuchumi, kijamii, kiutamaduni na kisiasa. Mtu yeyote anayedai kwamba anaweza kupambana na ufisadi na kuleta maedeleo kwa kukanyanga demokrasia na utawala wa sheria ni mwongo na anastahili kukataliwa na kukemewa mapema kabla hajaota pembe.  Tunasisitiza kuwa mtu yeyote wa kawaida au kiongozi anayesema kwamba anaweza akapambana na ufisadi kwa kukanyaga misingi ya demokrasia na utawala wa sheria mtu huyo ni fisadi na anataka kujenga himaya mpya ya ufisadi. Mtu huyo, pamoja na mambo yake yote, yafaa akataliwe na kudharauliwa haraka!

Ahsanteni sana kwa kunisikiliza.

About HABARI24 TV

Post a Comment
Powered by Blogger.