Wednesday, October 26, 2016

MATUMAINI YA KAFULILA KURUDI BUNGENI YAFUFULIWA TENA NA MAHAKAMA


HATUA ya Mahakama ya Rufaa, Kanda ya Tabora kutupilia mbali maombi ya kufutwa rufaa ya Davidi Kafulila iliyowasilishwa na mawakili wa Hasna Mwilima, Mbunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jimbo la Kigoma Kusini, inainua matumaini mapya kwa mdai, anaandika Pendo Omary.  


Mdai katika kesi hiyo ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana ya kupinga matokeo kwenye jimbo hilo yaliyotangazwa kumpa ushindi Mwilima ni Kafulila. Kafulila alikuwa mbunge wa jimbo hilo kwa miaka mitano (2010-15).

Swali linaliobuka hapo ni je, uamuzi huo unaweza kuwa hatua nzuri kwa Kafulila (NCCR-Mageuzi) kufikia malengo yake ya kutangazwa mshindi kama anavyoiomba mahakama kutokana na ushahidi wake ambao tayari ameuwasilisha?

Mahakama hiyo kupitia Majaji Luanda, Mbarouk na Mziray tarehe 12 mwezi huu walitengua hati iliyowasilishwa na mawakili wa serikali ya kuitaka mahakama hiyo kufuta rufaa iliyofunguliwa na Kafulila dhidi ya Mwilima kwamba, hati hiyo ilikuwa na kasoro za kiufundi.


Majaji hao kwa pamoja waliamua kwamba, Kafulila anaweza kurejesha rufaa hiyo baada ya kurekebisha kasoro tajwa kwa hoja kuwa, mahakama haiwezi kuifuta moja kwa moja wakati haijafikia kusikiliza hoja za msingi  wa rufaa yenyewe.

“Kufuatia uamuzi huo niliiomba mahakama kurekebisha kasoro hizo ili kesi ya msingi isikilizwe kuamua nani aliyeshinda uchaguzi wa Jimbo la Kigoma Kusini mwaka 2015 kwa mujibu wa fomu za matokeo 21B ambazo ingawa ziliwasilishwa na tume ya mahakama huku kila upande ukidai umeshinda.

“Lakini Jaji anayesikiliza shauri hili ngazi ya Mahakama Kuu, Jaji Wambali ambaye siku chache baada ya hukumu hiyo aliteuliwa kuwa jaji kiongozi, alikataa fomu hizo kuhesabiwa ili kuamua mvutano huo,” amesema Kafulila kwenye mahojiano na MwanaHALISI Online leo.
Kutokana na hatua ya Kafulila kufikisha maombi ya kutaka kesi ngazi ya rufaa iendelee, mahakama leo imeagiza pande husika za kesi kufika mbele ya Jaji Mrangu tarehe 3 Novemba, 2016 Tabora kwa ajili ya ombi hilo lilowasilishwa na Kafulila ili rufaa iweze kuendelea.

Kafulila aliamua kwenda mahakamani kwa lengo la kutafuta haki yake baada ya kutoridhishwa na matokeo ya kushindwa na kwamba, matokeo yaliyotangazwa katika nafasi hiyo jimboni kwake ni tofauti na yale aliyonayo ya vituo 382 kwenye jimbo hilo ambayo yanampa ushindi.

Alisema kusudio kubwa la kwenda mahakamani ni kuiomba mahakama kuhesabu upya matokeo ya kura zilizopigwa ambazo nakala zake kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) anazo mkononi kama ushahidi na kisha mahakama kutangaza upya mshindi wa jimbo hilo bila kurudia tena uchaguzi.

Kafulila amedai kuwa, yeye ndiye alipaswa kuibuka mshindi katika uchaguzi huo kwa kura 34,149 huku mpinzani wake (Mwlima) akipata kura 32, 982 lakini badala yake kura zilizotangazwa kuwa amezipata ni elfu 33 pekee ambazo hakubaliani nazo.

Hata hivyo baada ya matokeo hayo kutangazwa Kafulila alishindwa kusaini fomu ya kukubali matokeo ya kushindwa katika uchaguzi huo. Katika kesi hiyo namba 2 ya mwaka 2015.
Walalamikiwa katika kesi hiyo ni pamoja na Mwilima na mwanasheria wa serikali anayewakilisha Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).


Katika kesi hiyo wakili Kenedy Fungamtama anamtetea Mwilima huku Kafulila akitetewa na mawakili watatu Prof. Abdallah Safari, Tundu Lissu na Daniel Rumenyela.


No comments: