Tuesday, October 11, 2016

MFUMUKO WA BEI WA TAIFA KWA MWEZI SEPTEMBA 2016 UMEPUNGUA KWA ASILIMIA 4.5

 Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Ephraim Kwesigabo (kushoto), akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Dar eas Salaam leo, kuhusu mfumuko wa bei ya taifa kwa mwezi Septemba 2016. 
 Mkutano na wanahabari ukiendelea.
 waandishi wa habari wakichukua taarifa hiyo.
Waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali wakichukua taarifa hiyo

Na Dotto Mwaibale

MFUMUKO wa Bei wa Taifa kwa mwezi Septemba, 2016 umepungua hadi asilimia 4.5 kutoka asilimia 4.9 ilivyokuwa mwezi Agosti 2016.

Hayo yabebainishwa na Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Ephraim Kwesigabo wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Dar eas Salaam leo. 

" Hii inamanisha kuwa kasi ya upandaji wa bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia Septemba, 2016 imepungua ikilinganishwa na kasi ya upandaji ilivyokuwa kwa mwaka ulioishia mwezi Agosti 2016 " alisema Kwesigabo.

Alisema  Fahirisi za bei zimeongezeka hadi 103.05 mwezi Septemba 2016 kutoka 98.64 
mwezi Septemba 2015.Kwesigabo aliongeza kuwa mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi mwezi Septemba 2016 umepungua hadi asilimia 6.0 kutoka asilimia 7.0 ilivyokuwa 
mwezi Agosti 2016.

Alisema  kupungua kwa mfumuko wa bei wa mwezi Septemba 2016 kumechangiwa na kupungua kwa kasi ya bei za baadhi ya bidhaa za vyakula na zisizo za vyakula kwa kipindi kilichoishia mwezi Septemba 2016 zikilinganishwa na bei za mwezi Septemba 2015.

Alisema mwenendo wa bei za baadhi ya bidhaa za vyakula zilizoonesha kupungua ni pamoja na bei za dagaa kwa asilimia 11.6 na viazi vitamu kwa asilimia 3.2.

"Kwa upande mwingine mwenendo wa bei za baadhi ya bidhaa zisizo za vyakula zilionesha kupungua ni pamoja na bei za gesi kwa asilimia 10.4, dizeli kwa asilimia 2.9 na petrol kwa asilimia 2.8.

Akizungumzia mabadiliko ya bei kati ya mwezi Agosti na Septemba 2016 fahirisi za bei zimepungua hadi 103.o5 mwezi Septemba 2016 kutoka 103.28 mwezi Agosti 2016.

Alisema kupungua kwa fahirisi za bei kumechangiwa na kupungua kwa bei za baadhi ya bidhaa za vyakula na bidhaa zisizo za vyakula.

Alitaja baadhi ya bidhaa zilizochangia kupungua kwa fahirisi ni pamoja na mchele kwa asilimia 2.6, unga wa mahindi kwa asilimia 1.0, dagaa kwa asilimia 3.0 na mbogamboga kwa asilimia 4.3.

Alisema kwa upande mwingine baadhi ya bidhaa zisizo za vyakula zilizochangia kupungua kwa mfumuko wa bei ni pamoja na dizeli kwa asilimia 2.9, petroli kwa asilimia 2.8 na mafuta ya taa kwa asilimia 2.9

Akizungumzia thamani ya shilingi ya Tanzania kwa mwezi Septemba 2016 kutoka mwezi Desemba 2015 alisema uwezo wa shilingi 100 ya Tanzania katika kununua bidhaa na huduma umefikia sh.97 na senti 04 mwezi Septemba 2016 kutoka mwezi Desemba 2015 ikilinganishwa na shilingi 96 na senti 83 ilivyokuwa mwezi Agosti 2016.

Kwesigabo akizungumzia mfumuko wa bei kwa bidhaa ya nchi za Afrika Mashariki nchini Kenya mfumuko wa bei wa mwezi Septemba 2016 umeongezeka kidogo hadi asilimia 6.34 kutoka asilimia 6.26 mwezi Agosti 2016.

Alisema nchini Uganda mfumuko wa bei wa mwezi Septemba 2016 umepungua hadi asilimia 4.2 kutoka asilimia 4.8 mwezi Agosti 2016.




No comments: