Sumaye kunyang’anywa shamba na serikali, apewa notisi ya siku 90

Waziri wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amesema hati ya shamba lililopo maeneo ya Bunju la aliyekuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Fredrick Sumaye liko katika hatua ya kufutwa na kwamba Afisa Ardhi Mteule wa Wilaya ya Kinondoni Rehema Mwinuka ameshatoa barua ya notisi.

Luluvi ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na wandishi wa habari.
“Shamba la Sumaye hati yake iko katika hatua za kufutiwa,
Afisa Ardhi Mteule wa Wilaya ambaye anajukumu la kutoa notisi, ameshatoa notisi kwamba hajaendeleza eneo hilo kwa muda mrefu hivyo kwa mujibu wa sheria hati yake inatakiwa kufutwa,” amesema.
Amesema serikali haitofumbia macho wamiliki wa ardhi na mashamba ambao hawajayaendeleza kwa muda mrefu.
Pia, kufuatia ongezeko la matapeli wanaotumia nyaraka za kughushi za barua za toleo (ofa) zinazodaiwa kutolewa na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Luluvi ametoa agizo hususani kwa wakazi wa jiji hilo wanaomiliki ardhi pasipo kuwa na hati miliki, kujisalimisha kwa kupeleka barua zao za ofa kwa Kamishna wa Ardhi ili wapatiwe hati halali.
“Wamiliki wote wanaomiliki ardhi kwa karatasi za ofa halali wazibadilishie ili wapewe hati halali, na atakaegundulika kumiliki ofa feki polisi watawakamata na kupelekwa mahakamani,” amesema.
Amesema asilimia 60 ya watu wanaopeleka kesi za migogoro ya ardhi wizarani, chanzo cha migogoro hiyo ni karatasi za ofa zinazotoka katika halamshauri za jiji na manispaa.
“Natoa miezi mitatu ili karatasi hizi zisitokee tena kila mtu alete barua ya ofa watapewa hati zao ndani ya mwezi mmoja ,wazilete kwa kamishna wa ardhi wa mkoa, baada ya hapo sitasikiliza malalamiko ya watu walioibiwa ardhi wakiwa na ofa ya namna hii.
“Tumieni miezi mitatu vizuri kubadilisha ofa,” amesema.
Hali kadhalika, Lukuvi amepiga marufuku vitendo vya uvamizi wa ardhi na mashamba vinavyofanywa na baadhi ya wananchi, na kuwataka wananchi kutoa taarifa pindi watakapobaini kuwa kuna shamba au ardhi isiyoendelezwa.
“Serikali ina laani uvamizi wa ardhi na mashamba unaofanywa na baadhi ya wananchi sababu baadhi yao yanamilikiwa kihalali na yana hati, serikali ipo na sheria zipo zitafanya kazi yake,” amesema.
CHANZO MO BLOG

About HABARI24 TV

Post a Comment
Powered by Blogger.