Wednesday, October 5, 2016

UHAKIKI NA UBORESHAJI WA TAARIFA ZA TIN KWA MKOA WA DAR ES SALAAM KUMALIZIKA OKTOBA 15/2016

2
Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa kodi TRA, Richard Kayombo akifafanua jambo kwa waandshi wa habari wakati wa mkutano huo uliofanyika Makao Mkuu ya TRA. Kulia ni Gabriel Mwangosi Meneja wa Huduma na Elimu kwa Mlipa kodi TRA.
Zikiwa zimebaki siku tisa kumaliza zoezi la uhakiki na uboreshaji wa taarifa za Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) kwa mikoa ya kodi ya Dar es salaam na Zanzibar, tayari Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imehakiki na kutoa vyeti vipya vya TIN 15,467.
Zoezi la ukakiki na uboreshaji wa taarifa za TIN linaendelea hadi tarehe 15 Oktoba 2016 katika ofisi zilizoanishwa hivyo wananchi wenye TIN wanashauriwa kuhakiki TIN zao kabla muda uliowekwa haujaisha kwani baada ya muda huo kuisha TIN ambayo itakuwa haijahakikiwa itaondolewa katika mfumo wa TIN wa TRA.
1
Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa kodi TRA, Richard Kayombo katikati akizungumza na waandishi wa habari  wakati alipokuwa akitangaza makusanyo ya kodi ya mwezi wa tisa pamoja na uhakiki wa TIN za wafanyabiashara ambapo amesema siku ya mwisho kwa Dar es salaam itakuwa Oktoba 15 2016, kulia ni Gabriel Mwangosi Meneja wa Huduma na Elimu kwa Mlipa kodi TRA na kushoto ni Julius Ciza Afisa Mkuu wa Huduma na Elimu ya Mlipa KodiTRA Makao Mkuu.
Vituo vya uhakiki:



  • Mkoa wa Kodi Ilala: Jengo la Mariam Tower (Shaurimoyo) na 14Rays (Kariakoo-Gerezani)
  • Mkoa wa Kodi Kinondoni: Jengo la LAPF (Kijitonyama) na Kibo Complex (Tegeta) na ofisi za TRA Kimara
  • Mkoa wa Kodi Temeke: Uwanja wa Taifa na Ofisi za TRA Mbagala- Zakhemu
  • Wilaya ya Kigamboni – Ofisi za TRA Kigamboni
Pamoja na kuwakumbusha wananchi kuendelea kuhakiki na kuboresha taarifa za TIN, tungependa pia kuwakumbusha na kuwahimiza wafanyabiashara na wananchi mambo yafuatayo:-
Wasafirishaji wa mizigo kwenda mikoani wanahimizwa kudai risiti za EFDs pindi wanaponunua bidhaa na kuwa nazo wakati wanasafirisha mizigo ili kuepuka usumbufu pale wanapohitajika kuonyesha risiti hizo.
Aidha wafanyabiashara nao wanahimizwa kutoa risiti kwa wateja wao ili kuhakikisha makusanyo ya kodi yanakusanywa kwa usahihi
Waagizaji wa mizigo nje ya nchi kwa upande wao wanatakiwa kutumia mfumo wa forodha wa TANCIS kila mara kufuatilia taarifa za upakuaji wa bidhaa zao ili kuepuka udanganyifu wa aina yoyote.
Kwa kutumia TANCIS mzigo unaweza kufualiwa kwa: kuandika namba ya TANSAD sehemu ya meseji/ujumbe bila kuacha nafasi. Mfano TZDL15XXXXXX kisha tuma kwenda namba 15111. Utapata ujumbe kuhusu hatua iliyofikiwa katika kuondosha mzigo.
Kwa wale wanaoagiza magari wanashauriwa kupata taarifa za kodi wanayostahili kulipa kabla magari hayajafika ili kuepuka malalamiko ya aina yoyote pale matarajio yao yanapotofautiana na makadirio ya kodi wanayostahili kulipa. Taarifa za kodi ya magari zinapatikana katika kikokotozi kilichopo katika tovuti ya TRA
Wale Walipakodi ambao wana madeni mbalimbali ya kodi tunawashauri waonane na mameneja wa Wilaya au Mikoa ya Kodi ili kuona jinsi ya kulipa madeni hayo kuliko kukaa kimya na hivyo deni kuendelea kuongezeka.
Katika hatua nyingine TRA imekusanya jumla shilingi trilioni 3.59 katika kipindi cha miezi mitatu ya mwanzo wa mwaka wa fedha 2016/17 kati ya lengo la mwaka la kukusanya shilingi trililioni 15.1 mwaka 2016/17. Makusanyo hayo yanajumuisha mwezi Julai shilingi Trilioni 1.05, mwezi Agosti Trilioni 1.13 na Septemba 2016 shilingi Trilioni 1.37.
Ukusanyaji wa mapato ya serikali unaenda sambamba na kuelimisha wananchi kuhusu wajibu wao wa kulipa kodi sahihi na kwa wakati hivyo tunawaomba waandishi wa habari kuendelea kutoa elimu hiyo kupitia vyombo vyao vya habari.
Mwisho napenda kuwasisitiza waandishi wa habari kuwania tuzo ya ‘Uandishi wa Kodi na Makusanyo ya Mapato ya Serikali’ katika tuzo za Umahiri katika Uandishi wa Habari 2016, ambazo hutolewa na Baraza la Habari Tanzania (MCT), pale MCT itakapozindua uwasilishwaji wa kazi za waandishi. ili kuendelea kuelimisha masuala mbalimbali yahusuyo kodi na kujishindia zawadi mbalimbali zitakazotolewa.
‘Pamoja Tunajenga Taifa Letu’
Richard M. Kayombo
Mkurugenzi Huduma na Elimu kwa Mlipakodi

No comments: