Monday, October 3, 2016

WATANZANIA WATAKIWA KUPAMBANA NA DHULUMA,NA KUKEMEA MAOVU,IWE NJIA YA KUMUENZI IMAM HUSSEIN

Naibu kiongozi mkuu wa waislam Shia Ithnasharia Tanzania Sheikh Muhammad Abdi akizngumza na wanahabari Leo Jijini Dar es salaam PICHA NA EXAUD MTEI
 Watanzania wametakiwa kuhakikisha kuwa wanaishi katika njia za kumpendeza mwenyezi mungu ikiwa ni pamoja na kuhakikisha maswala ya kuboresha hali ya jamii yanayopewa kipaumbele,kukataa kudhulumu,kuamrisha mema pamoja na kukemea maovu kama mauaji ya walemavu wa ngozi,matendo ya kijambazi,ubakaji,ikiwa ni njia ya kumuenzi Imam Hussein aliyekuwa mstari wa mbele katika kukemea mambo hayo.

Wito huo umetolewa leo Jijini Dar es salaam na Naibu kiongozi mkuu wa waislam Shia Ithnasharia Tanzania Sheikh Muhammad Abdi alipokuwa anazungumza na wanahabari kuhusu kuukaribisha mwaka mpya wa kiislam mwaka ambao ni wa 1438H katika kalenda ya kiislam pamoja na kumbukumbu ya Imam Hussein mkutano ambao umefanyika katika msikiti wao uliopo Kigogo Post Jijini Dar es salaam.

Kiongozi huyo amesema kuwa Imam Hussein ambaye wanamkumbuka leo ni moja kati ya viongozi wa dini ambao aliwafunza watu namna ya kupinga ukandamizaji,dhuluma katika jamii pamoja na kutetea haki za wanyonge hivyo ni wakati wa wananchi wa Tanzania kuanza kufwata maneno yake na kuhakikisha kuwa wanaenzi yale mema aliyoyaacha katika jamii.
Amesema kuwa leo hii dunia inalazimika kuitika wito wa Imam Hussein ili kuinusuru dunia iliyotapakaa damu kila kona,ambapo akitolea mfano wa mashariki ya kati ambapo imekuwa ikishughudiwa watoto wanavyochinjwa na maelfu kukimbia makazi yao kwa sababu ya uharibifu,huku pia katika bara la Africa ikishughudiwa makundi ya kiigaidi yakiibuka katika nchi nyingi ambapo yamekuwa yakileta madhara makubwa kwa wananchi wasio na hatia huku  akisema kuwa mambo haya ni mambo ambayo yalikuwa yanamkera sana Imam Hussein na kama angekuwepo angejitokeza kupambana nayo.


Aidha Sheikh Muhammad Abdi ameonyesha kuhuzunishwa na baadhi ya matendo ambayo yamekuwa yakitokea nchini Tanzania yakiashiria matendo ya kigaidi na mauaji kwa wasio na hatia ambapo ametoa wito kwa watanzania kuacha mara moja maswala hayo na kurudisha umoja na upendo miongozi mwa jamii.

Aidha katika hatua nyingine kiongozi huyo ametoa pole kwa watanzania wote waliopatwa na janga la Tetemeko mapema mwezi jana huku akitoa wito kwa watanzania kuendelea kuwaombea na kuwasaidia wahanga hao.

No comments: