Sunday, December 11, 2016

Azam FC yatoka sare na Mtibwa Sugar


KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imelazimishwa sare ya mabao 2-2 dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye mchezo wa kirafiki uliofanyika Uwanja wa Azam Complex usiku huu.
Azam FC imeutumia mchezo huo kama maandalizi tosha ya kujiandaa na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), ambapo itaanza kufungua dimba Desemba 18 mwaka huu kwa kuvaana na African Lyon katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Kocha Mkuu wa Azam FC, Zeben Hernandez, alitumia vikosi viwili tofauti kwenye mchezo huo cha kwanza kikianza kipindi cha kwanza na kingine kikimalizia kipindi cha pili.
Alikuwa ni Enock Atta Agyei, aliyeweza kuipatia bao la uongozi Azam FC kwa mkwaju wa penalti dakika ya 14, kufuatia kipa wa Mtibwa Sugar, Said Mohamed, kumwangusha ndani ya eneo la hatari mshambuliaji wa mabingwa hao, Francisco Zekumbawira.

Azam FC iliyoonekana kucheza vema kwa soka la kasi kipindi cha kwanza, ilijikuta ikiwaruhusu Mtibwa Sugar kusawazisha dakika ya 28 kupitia kwa nahodha wao, Shaban Nditi na hivyo kufanya mchezo huo kwenda mapumziko kwa sare ya bao 1-1.
Mshambuliaji mpya wa Azam FC, Yahaya Mohammed, aliyeingia dakika ya 61 kuchukua nafasi ya Agyei, naye alifungua akaunti ya mabao kama mtangulizi wake huyo kwa kuipatia bao la pili timu hiyo kwa shuti la kiufundi.

Kinda wa zamani wa timu ya vijana ya Azam FC, Ibrahim Rajab ‘Jeba’, aliisawazishia Mtibwa Sugar dakika ya 90 kwa njia ya mkwaju wa penalti na kufanya mpira kumalizika kwa sare hiyo.
Tukio la kuvutia kwenye mchezo huo ni mashabiki waliokuwa uwanjani kumpigia makofi ya shukrani winga wa Azam FC, Enock Atta Agyei, wakati akitolewa na kuingia Mohammed dakika ya 61, na hii ni kufuatia konyesha kiwango kizuri kwenye mchezo huo.

Benchi la ufundi la Azam FC, pia liliutumia mchezo huo kuwafanyia majaribio wachezaji wawili kiungo mkabaji Stephane Kingue na beki wa kati, Yakubu Mohamed aliyetokea Aduana Stars ya Ghana.

Kikosi cha Azam FC leo:
Mwadini Ally/Aishi Manula dk 46, Abdallah Kheri/Shomari Kapombe dk 46, Erasto Nyoni/Bruce Kangwa dk 46, Aggrey Morris/Daniel Amoah dk 46, David Mwantika/Yakubu Mohammed dk 46, Jean Mugiraneza/Himid Mao dk 46, Frank Domayo/ Stephane Kingue dk 46, Ramadhan Singano/Salum Abubakar dk 46, Francisco Zekumbawira/John Bocco dk 46, Enock Atta/Yahaya Mohammed dk 61, Joseph Mahundi/Samuel Afful dk 46

No comments: