Tuesday, December 6, 2016

Bocco: Tutakaa nafasi nzuri raundi ya pili


 IKIWA ni siku ya pili tu tokea Azam FC ianze mazoezi, nahodha wa mabingwa hao wa Afrika Mashariki na Kati, John Bocco ‘Adebayor’, anaamini ya kuwa kikosi hicho kitakuwa vizuri na kukaa nafasi nzuri kwenye mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).

Azam FC inayodhaminiwa na kinywaji safi cha Azam Cola kinachosisimua koo na kuchangamsha mwili, pamoja na Benki bora kabisa nchini kwa usalama wa fedha zako ya NMB, tayari kimeanza mazoezi tokea jana asubuhi ili kujiweka fiti zaidi kwa ajili ya kuanza mzunguko wa pili wa ligi.
Bocco ameunambia mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz mara baada ya mazoezi ya leo ya asubuhi kuwa morali waliyokuwa nayo wachezaji pamoja na nguvu za nyota wapya walioongezwa kikosini kwenye usajili huu wa dirisha dogo, utaweza kuwasaidia kufanya vizuri.
“Tunamshukuru Mungu tumeweza kufika na kufanya mazoezi salama kwa ajili ya kujiandaa na mzunguko wa pili, mazoezi tumeanza vizuri, wachezaji wote wanamorali, wamerudi wameonekana hawakwenda nyumbani tu kupumzika bali walikuwa wakifanya baadhi ya mazoezi, kwa hiyo naamini raundi ya pili itakuwa ni nzuri sana kwetu,” alisema.
Nahodha huyo aliongeza kuwa: “Ukizingatia hata katika usajili kuna nguvu tumeweza kuiongeza, kwa hiyo ninaimani wachezaji tutaweza kujituma na Mungu atatusaidia tutaweza kufanya vizuri raundi ya pili.”
Benchi la Ufundi la Azam FC kwa kushirikiana na uongozi wa timu hiyo, katika usajili huu wa dirisha dogo unaoendelea uwemeza kuongeza nguvu mpya kwa kuwasajili washambuliaji nyota wawili kutoka Ghana, Yahaya Mohamed anayetokea Aduana Stars na staa wa Sekondi Hasaacas, Samuel Afful.
Pia imeweza kuwarudisha kundini wachezaji wake wawili waliokuwa kwa mkopo, beki wa kati kinda Abdallah Kheri aliyekuwa Ndanda na winga wa kushoto Enock Atta Agyei (Medeama).
Mabingwa hao wa Ngao ya Jamii, wanaojiandaa pia na michuano ya Mapinduzi Cup, Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) na Kombe la Shirikisho Afrika (CC), hadi inamaliza mzunguko wa kwanza wa ligi imefanikiwa kujikusanyia jumla ya pointi 25 katika nafasi ya tatu kwenye msimamo ikizidiwa pointi 10 na kinara Simba aliyejikusanyia 35 na Yanga ikiwa nazo 33 


No comments: