JESHI LA POLISI KUIMARISHA ULINZI WAKATI WA MAADHIMISHO YA SIKU YA UHURU NA SIKUKUU YA MAULID


 


Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar Es salaam kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama limejipanga ipasavyo kuhakikisha amani na utulivu vinatawala wakati  wa kuazimisha sikukuu ya uhuru itakayofanyika tarehe 09/12/2016 katika uwanja wa uhuru jijini  Dsm.

Sherehe hiyo itahudhuriwa na viongozi na wakuu wa nchi za jirani, viongozi wa kitaifa, mabalozi, wanasiasa mbalimbali pamoja na viongozi wengine waliolitumikia taifa na kustaafu.

Aidha tunaomba wananchi wasiwe na shaka yoyote ya kiusalama na pia wajitokeze kwa wingi katika uwanja huo ili kusherehekea sikukuu hiyo kwa utulivu na amani.
Kutakuwa na doria kuzunguka uwanja huo pamoja na maeneo mbalimbali ya jiji ya  jiji la Dar Es salaam.

Sambamba na hilo pia tarehe 12/12/2016 ni sikukuu ya MAULID, Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam limejipanga vizuri katika kuhakikisha katika kipindi chote cha kuazimisha sikukuu hii ulinzi na usalama unakwepo hususan katika maeneo ya misikiti ambapo ibada zitafanyika.

Kutakuwa na doria ya miguu, askari kanzu, askari wa Mbwa na farasi, FFU na askari wa doria za magari ili kuhakikisha sikukuu inasherekewa kwa furaha na amani.
Pia askari watafanya doria katika maeneo yote yenye mikusanyiko mkubwa kama fukwe za bahari ya Hindi na maeneo mengine ya starehe ili kuzuia vitendo vya uvunjifu wa amani.

Disko toto haziruhusiwi na wazazi/walezi wasiwasiwaache watoto wao watange tange ovyo.
Nyumba zisiachwe bila mwangalizi kwa kipindi cha sherehe kwani wahalifu wanaweza kutumia mwanya huo kufanya uhalifu.


POLISI KANDA MAALUM DSM WAKUSANYA TSH 451,590, OOO /= KUPITIA TOZO ZA MAKOSA YA USALAMA BARABARANI
Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dsm kupitia kikosi chake cha usalama barabarani kimekamata makosa mbalimbali ya usalama barabarani kwa kipindi cha kuanzia tarehe 02/12/2016 hadi tarehe 07/12/2016 na kuingizia serikali mapato ya ndani kama ifuatavyo;
1.     Idadi ya magari yaliyokamatwa                            - 13,496
2.    Idadi ya Pikipiki zilizokamatwa                             - 1,296       
3.    Daladala zilizokamatwa                                      - 5,713
4.    Magari mengine (binafsi na malori)                        - 7,783
5.    Bodaboda waliofikishwa Mahakamani
kwa makosa ya kutovaa helmet na
kupakia mishkaki                                                - 4
6.    Jumla ya Makosa yaliyokamatwa                             -  15,053
Jumla ya Fedha za Tozo zilizopatikana TSH 451,590,OOO/=

Aidha madereva wanatakiwa kuwa makini katika kipindi hiki cha kuelekea mwisho wa mwaka ili kuepuka ajali zisizo za lazima.

POLISI DSM YAWAKAMATA WATUHUMIWA SUGU 103

Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar Es salaam limefanya msako mkali kuanzia tarehe 02.12.2016  hadi 08.12.2016 na kufanikiwa kuwakamata jumla ya watuhumiwa sugu 103 wa makosa mbalimbali. Watuhumiwa hao wamekamatwa maeneo mbalimbali kwa nyakati tofauti tofauti. Wamekamatwa kwa makosa ya unyang’anyi wa kutumia nguvu, kuvunja nyumba usiku na kuiba, wizi kutoka maungoni, kucheza kamari, kubughudhi abiria, wizi wa magari, wizi kutoka maungoni, kutengeneza, kuuza na kunywa pombe haramu ya Gongo, uvutaji bhangi nk

Oparesheni hii ni endelevu tunawaoba raia wema waendelee kutoa taarifa za uhakika za kuhusu uhalifu unaotendeka, uliotendeka na unaotarajiwa kutendeka.


NIWATAKIE SIKUKUU NJEMA YA UHURU NA MAULIDI


S.N.SIRRO - CP
KAMISHNA WA POLISI KANDA MAALUM

DAR ES SALAAM

About HABARI24 TV

Post a Comment
Powered by Blogger.