Wednesday, December 7, 2016

Mgogoro wa Tanzania na Malawi wazuka Upya,ila Tanzania imezungumza haya leo


Serikali ya Tanzania imesema mzozo kuhusu mpaka wake na Malawi katika Ziwa Malawi kwa sasa unashughulikiwa na jopo la maais wastaafu, na kwamba uhusiano kati ya nchi hizo mbili umeimarika.

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, kupitia taarifa, imesema kwamba licha ya kuwepo kwa mgogoro wa mpaka wa Tanzania na Malawi katika Ziwa Nyasa, uhusiano wa nchi hizo mbili ni mzuri.
"Ukweli ni kuwa, mgogoro wa mpaka kati ya Tanzania na Malawi kwa sasa upo chini ya Jopo la Viongozi Wastaafu wa Afrika wanaotokea kwenye nchi za Ukanda wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC)," taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imesema.

"Jopo hilo linaongozwa na Joachim Chissano, Rais Mstaafu wa Msumbiji akisaidiwa na Festus Mogae, Rais Mstaafu wa Botswana na Thabo Mbeki, Rais Mstaafu wa Afrika Kusini."
Taarifa hiyo ya serikali imetolewa baada ya wasiwasi kutanda kuhusu uwezekano wa kuzuka tena kwa mzozo kati ya nchi hizo kutokana na ramani iliyodaiwa kutolewa na Tanzania ikionyesha kuwa inaamiliki nusu ya Ziwa Malawi au Nyasa.
Ramani hiyo ya Tanzania ilionyesha kuwa eneo la Kaskazini Mashariki mwa ziwa hilo ni sehemu ya himaya yake, lakini Malawi nayo inadai kuwa eneo hilo lote ni lake.
Malawi ilikuwa imewasilisha ombi kwa Umoja wa Mataifa, Mungano wa Afrika na mashirika mengine ya kimataifa kuingilia kati.
Msemaji wa wizara ya mashauri ya nchi za kigeni nchini Malawi, Rejoice Shumba aliambia gazeti la The Nation la Malawi kuwa nchi yake ilikuwa imeandika barua kwa mashirika makuu duniani ikiyataka kupuuzilia mbali ramani ya Tanzania.
Serikali ya Tanzania hata hivyo imesema kwamba jopo hilo ambalo liliundwa na Umoja wa Afrika kupitia Jukwaa la Viongozi Wastaafu wa Afrika kwa ajili ya kusuluhisha mgogoro huu, linaendelea na kazi hiyo kwa kupitia taarifa mbalimbali na maandiko yaliyowasilishwa kwao na Tanzania na Malawi.
Vile vile, jopo lilikwisha zikutanisha pande zote mbili katika mashauriano ya awali yaliyofanyika nchini Msumbiji.
"Wizara inapenda kuujulisha umma kuwa licha ya kuwepo kwa mgogoro wa mpaka wa Tanzania na Malawi katika Ziwa Nyasa, mahusiano ya nchi hizi mbili yamezidi kuimarika siku hadi siku katika Nyanja zote za kiuchumi, kisiasa na kijamii," taarifa ya wizara ya mambo ya nje ya Tanzania ilisema.
"Hata wananchi wa pande zote mbili za Ziwa wameendelea kuishi kwa amani na ushirikiano wa karibu."
Kwa mujibu wa Tanzania, nchi hizo mbili zinatarajia kuwa na mkutano wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano mapema mwakani ambao utawaleta watalaam wa nchi hizo mbili kutoka sekta mbalimbali.
Lengo la mkutano huo litakuwa kujadili changamoto za ushirikiano katika sekta hizo, kubaini maeneo mapya ya ushirikiano pamoja na kuweka mikakati ya kutekeleza miradi ya pamoja itakayokubaliwa baina ya pande hizi mbili.
Aidha, watakaohudhuria watajadili masuala ya ushirikiano katika sekta za biashara na uwekezaji, usafirishaji, fedha, nishati, utalii, ulinzi na usalama uhamiaji, uvuvi na ardhi.
SOURCE -BBC

No comments: