ACT WAZALENDO WALIA NA RAFU UCHAGUZI MDOGO

 Ado Shaibu,Katibu wa Itikadi, Mawasiliano na Uenezi akizungumza na wanahabri mapema leo makao makuu ya chama hicho Jijini Dar es salaam


Chama cha ACT Wazalendo kinalaani vitendo vyenye uelekeo wa kukipendelea Chama cha Mapinduzi vinavyofanywa na watendaji wa serikali kwenye maeneo mbalimbali ambako uchaguzi wa marudio wa ubunge na madiwani unaendelea.

Kwa muda mrefu Chama cha mapinduzi kimekuwa kikitumia vyombo vya dola na watumishi wa umma kuwashawishi wananchi kukipigia kura chama hicho kwa ahadi mbalimbali za kimaendeleo na kuvihujumu vyama vya upinzani licha ya vitendo hivyo kuwa kinyume na sheria, kanuni, maadili na taratibu za uchaguzi.

Kwa mujibu wa Kanuni za Maadili ya Uchaguzi ambazo vyama vyote vimetia saini, kuanzia kipindi cha kampeni za uchaguzi mpaka kutangazwa kwa matokeo, mawaziri , watendaji na mamlaka nyingine za serikali haziruhusiwi kutoa ahadi za shughuli za maendeleo ya jamii kwa wananchi. Kinyume na matakwa haya ya kisheria, Chama cha mapinduzi kimeendelea kuwatumia watendaji wa serikali kuwashawishi wananchi kukipigia kura chama hicho kwa kutumia ahadi mbalimbali za kimaendeleo.

Mathalani, kwenye kata ya Nkome iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Geita, watendaji wa Halmashauri wameanza kuwahadaa wazee kwa namna ambayo inalenga kukipendelea Chama cha Mapinduzi. Jana tarehe 11 Januari, 2017, Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Geita ilimuagiza Afisa Mtendaji wa Kata ya Nkome kuwakusanya wazee wa Kata hiyo na kuwaahidi kuwapatia huduma ya afya bure. 

Kwenye zoezi hilo, wazee waliagizwa kubeba vitambulisho vyao vya kupigia kura na kuviwasilisha mezani kwa maafisa waliofika katika ofisi ya afisa mtendaji kabla ya kuorodheshwa majina yao kwa ajili ya kupata huduma za afya bure. Wazee ambao hawakubeba vitambulisho vya kupigia kura waliwekwa kando na kutakiwa wakatafute hata vya ndugu zao!

Tumewasiliana na mkurugenzi wa Halmashauri ya Geita juu ya mpango huo unaolenga kukibeba chama tawala kwa rushwa ya matibabu,hata hivyo hakuwa na majibu ya kueleweka zaidi ya kusema atafuatilia jambo hilo.

Maswali ya msingi ya kujiuliza ni kuwa kwa nini zoezi hili lianze katika kipindi hiki cha kampeni? Kwa nini wazee walazimishwe kwenda na vitambulisho vyao vya kupigia kura?
Ni dhahiri kuwa kwa vitendo hivi watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita wanalenga kutumia zoezi la huduma ya afya bure kukipendelea chama cha mapinduzi kinyume na sheria na taratibu za uchaguzi.

Chama cha ACT Wazalendo kimeiandikia Tume ya Uchaguzi kulalamikia vitendo hivi na kuitaka ivikomeshe mara moja kwa ustawi wa demokrasia na amani ya nchi yetu. Tunakitaka pia chama cha mapinduzi kuacha mara moja vitendo vya kutumia watumishi wa umma kujipendelea katika uchaguzi. Vitendo hivi havisadifu tambo zinazotolewa na viongozi wa CCM hivi karibuni za “CCM Mpya” inayochukia vitendo vya rushwa na kuwajali wanyonge. Kuendelea na vitendo hivi ni ushahidi kuwa CCM ni “mvinyo wa zamani kwenye chupa mpya”.
Ado Shaibu,
Katibu wa Itikadi, Mawasiliano na Uenezi
Imetolewa leo 12 Januari, 2017.

About HABARI24 TV

Post a Comment
Powered by Blogger.