Thursday, January 26, 2017

Huyu ndiye Mkuu wa Wilaya mteuliwa wa Mh Magufuli aliyeamua kuachia Ngazi leo

Aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Uyui Bw. Gabriel Mnyele akizungumza na Mwandishi wa habari wa Azam tv Juma Kapipi wakati akiwa ofisi za CCM Wilaya ya Uyui ikielezwa kuwa alikuwa ameitwa na Uongozi wa chama hicho kufuatia kuwepo kwa taarifa kwamba ameamua kuachia ngazi nafasi ya Ukuu wa wilaya hiyo ya Uyui jambo ambalo alilithibitisha kwa Katibu wa CCM wilaya ya Uyui kwamba ni kweli amemwandikia barua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania-Picha kwa hisani ya Kapipij blog
Bw.Gabriel Mnyele hakuwa tayari kuelezea maamuzi aliyochukua na kuwataka waandishi wa habari waliokuwa wakihoji hatua ya maamuzi yake wasubiri tamko kutoka juu."Mimi sina la kusema kuhusu hilo nimeamua mwenyewe,kwani mmesikia kuwa nimetumbuliwa?Aliwahoji waandishi wa habari

******* 
Mkuu wa wilaya ya Uyui Mkoani Tabora,Gabriel Simon Mnyele ametangaza kujiuzulu nafasi hiyo.

Inaelezwa kuwa Mkuu wa Wilaya huyo amejiuzulu nafasi hiyo leo Alhamisi Januari 26, 2017 na kuwaaga madiwani wa Chama cha Mapinduzi (CCM) katika mkutano alioufanya wilayani humo.

Akieleza sababu ya kufanya uamuzi huo, Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa alimwandikia Rais Dkt Magufuli barua ya kujiuzulu nafasi hiyo akielezea kusongwa na majukumu binafsi.

Amesema ameacha ukuu wa wilaya kwa hiyari yake na wala hajatumbuliwa na kwamba anahitaji muda wa ziada wa kufanya majukumu yake binafsi.

Taarifa za kujiuzulu kwa Mnyele zimethibitishwa na katibu wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Uyui Hamis Kananda na mwenyekiti wa halmashauri hiyo Said Ntahundi ambao wamesema Mnyele amewaaga kwenye kikao cha kamati ya siasa ya wilaya na kwamba amekamilisha taratibu zote za kujiuzulu. 

Taarifa za kujiuzulu kwa Mnyele zimethibitishwa pia na katibu tawala wa mkoa wa Tabora Dr. Ntala na kueleza kuwa tayari Mnyele amerejesha kitambulisho chake cha kazi.

Mkuu wa Wilaya, Gabriel Simon Mnyele alikuwa miongoni mwa Wakuu wa Wilaya 139 walioteuliwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 26 Juni, 2016.
Taarifa kwa hisani ya MALUNDE1 BLOG

No comments: