Friday, January 20, 2017

KUWENI TAYARI KUKABILIANA NA CHANGAMOTO ZA KUHAMIA DODOMA- PROF MCHOME

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Katiba na Sheria Prof Sifuni Mchome amewataka Watumishi wa wizara kuwa tayari kutekeleza majukumu yao katika mazingira ya Makao Makuu ya Serikali mkoani Dodoma na wale wanaobaki Dar es salaam katika kipindi hiki cha mpito kuzingatia, hali itakavyokuwa kulingana na sheria, kanuni taratibu na miongozo na maelekezo ya kiutumishi.

Prof Mchome ametoa rai hiyo katika kikao cha pamoja na watumishi wa wizara kilichofanyika mjini Dar es salaam ili kuwekana sawa kufuatia kuanza kuondoka kwa kundi la kwanza la watumishi wa Wizara kuelekea makao makuu ya Serikali mjini Dodoma.
Prof Mchome amewataka watumishi kujiweka tayari katika kila hali kwa kuwa Wizara imeanza kutekeleza agizo la kuhamia makao makuu ya Serikali na kuchukua hatua stahiki katika kukabiliana na changamoto zitakazo jitokeza katika utekelezaji wa zoezi la kuhamia makao makuu.
“Nimewaita tuagane, mimi na viongozi wenzangu na watumishi wengine tunaanza safari ya kuhamia Dodoma, tumepeana wiki ijayo kuwa tumefika Dodoma kuanzia Januari 23 ili tuanze kujipanga, muwe tayari, kipindi hiki ni cha mpito, kina changamoto zake kama ilivyo katika maisha ya binadamu, hakuna kitu rahisi katika kuhama, kuanzia kwa mtumishi binafsi hadi kwa ofisi, lakini mkijiweka sawa mkawa macho na makini nina hakika sote kwa pamoja tutaweza kukabiliana na changamoto hizo,” alisema Prof Mchome

Awamu ya Kwanza yenye watumishi  25 wa wizara wakiongozwa na Waziri Dkt Harrison Mwakyembe , Katibu Mkuu Prof Mchome na Naibu Katibu Mkuu Bw. Amon Mpanju imeanza kuondoka mjini Dar es salaam kuanzia Januari 15, watakuwa wanaendelea kuwasili mkoani Dodoma hadi wiki ijayo na Wizara inatarajia kuzindua rasmi ofisi yake mkoani Dodoma Jumanne ya Januari 31, 2017.


Awamu ya pili na ya tatu zitafuata utaratibu ambao umewekwa na kwamba zoezi hilo linatarajiwa kukamilika ifikapo mapema mwaka 2018.


No comments: