Saturday, January 7, 2017

Lowassa, Maalim Seif kushambulia jukwaa Dimani



Dar es Salaam. Vigogo wawili wa siasa za upinzani nchini, Edward Lowassa na Maalim Seif Sharif Hamad kesho watapanda jukwaani katika Skuli ya Fuoni, Zanzibar kumnadi mgombea ubunge Jimbo la Dimani kwa tiketi ya CUF, Abdulrazaq Khatib Ramadhan.

Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, Lowassa ambaye pia ni Waziri Mkuu wa zamani na Maalim Seif aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar katika Serikali iliyopita, waligombea urais wa Jamhuri ya Muungano na Zanzibar, mtawalia.

Uchaguzi huo wa Dimani, utafanyika Jumapili Januari 22, kujaza nafasi iliyoachwa na aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Hafidh Ally Tahir aliyefariki dunia Novemba 11, mwaka jana katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma.

Chini ya ushirikiano wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), jana Chadema kilitangaza utaratibu jinsi vigogo wake watakavyoshiriki kampeni za uchaguzi huo kwa staili tofauti ili kuhakikisha mshirika wake CUF anaibuka kidedea.

Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Salum Mwalimu alisema jana kwamba kesho, Lowassa ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu, atakuwa kiongozi wa kwanza wa Chadema kuhudhuria kampeni hizo akishirikiana na Maalim Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CUF.

No comments: