MSIBA MWINGINE KWENYE SOKA LA TANZANIA MCHANA HUU

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikito taarifa ya kifo cha Nahodha wa timu ya 94 Green Warriors, Ikongo Julius Mbaga aliyefariki dunia leo alfajiri (Februari 17, 2017) kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ambapo alikuwa amelazwa.


Mchezaji huyo alijeruhiwa kwenye ajali ya gari ya timu yake iliyotokea Februari 13, 2017 Ihumwa mkoani Dodoma wakati ikiwa njiani kwenda Shinyanga kucheza mechi ya Ligi Daraja la Pili (SDL) dhidi ya Bulyanhulu FC.

Taratibu za mazishi ya Marehemu ambaye mwili wake umehamishiwa Hospitali Kuu ya Jeshi (GMH) ya Lugalo jijini Dar es Salaam zinafanywa na familia yake kwa kushirikiana na klabu ya 94 Green Warriors. Taarifa rasmi za mazishi zitatolewa baadaye.

TFF imetuma salamu za rambirambi kwa familia ya Marehemu, klabu ya 94 Green Warriors na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) na kuwataka kuwa na uvumilivu kwa kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.

Kwa Msiba huu, Rais wa TFF Jamal Malinzi ametuma salamu za rambirambi kwa Mwenyekiti wa 94 Green Warriors, familia ya marehemu, ndugu, jamaa na marafiki kwa msiba huo mkubwa wa mpendwa wao.

Bwana ametoa, Bwana ametwaa jina lake lihimidiwe.


About HABARI24 TV

Post a Comment
Powered by Blogger.