Friday, February 17, 2017

VIONGOZI NA WANACHAMA 215 WA CHADEMA WAFUNGULIWA KESI MAHAKAMANI


CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema wanachama na viongozi wake 215 wamefunguliwa kesi katika mahakama mbalimbali nchini tangu kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015. 


Chadema imesema wanachama hao wamepandishwa kizimbani katika jumla ya kesi 78 huku wengi wao wakinyimwa dhamana na wale waliopatikana na hatia, walipewa adhabu za vifungo bila ya kupewa fursa ya faini.

Kutokana na hali hiyo Chadema inatarajia kuandaa orodha itakayoainisha kesi zote za jinai ambazo bado zipo mahakamani pamoja na kuonyesha aina ya mashtaka na vifungo vilivyotolewa, kwa vyombo vya habari na taasisi za ndani na nje ya nchi. 

Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Profesa Abdallah Safari aliyasema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mrejesho wa kikao cha kamati ndogo ya Kamati Kuu ya Chadema kilichokaa Jumanne. 

Katika uchaguzi huo uliofanyika Oktoba 25, 2015 Rais John Magufuli wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) aliibuka mshindi kwa kupata kura 8,882,935 sawa na asilimia 58.46 ya kura zote halali. 

Nafasi ya pili ilishikwa na mgombea wa Chadema aliyeungwa mkono na mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa aliyepata kura 6,728,480 sawa na asilimia 39.97. 

Prof. Safari alisema mara baada ya Uchaguzi Mkuu huo kumalizika, viongozi wa Chadema wamekuwa wakikamatwa na kushtakiwa kwa makosa ya kubambikizwa; kwa kisingizio cha uchochezi. 

“Hivi sasa umekuwa ni mtindo kwa mahakama kuwakatalia dhamana wanachama wa Chadema bila ya sababu za msingi," alisema Prof. Safari. 

"Pia imekuwa ni mtindo kuwahukumu vifungo bila kuwapa fursa ya kulipa faini.” 

Prof. Safari alisema katika kikao hicho cha kamati kimetoa wito kwa mhimili wa Mahakama kutekeleza wajibu wake kwa weledi uliotukuka; kuhakikisha kuwa haki inatendeka bila kuwapo kwa vitisho kutoka kwa mtu yeyote. 

“Majaji wanapaswa kuiga mfano wa uhuru wa Mahakama na weledi wa majaji wa Afrika Kusini, Zimbabwe na Marekani ambao waliweza kutengua amri batili zilizotolewa na marais wa nchi zao,” alisema Prof. Safari. 


Aidha, Profesa Safari alisema Kamati Kuu imetoa wito kwa mawakili kuchukua wajibu mkubwa kuisaidia mahakama kutekeleza majukumu yake kwa weledi kwa kuhakikisha haki inatendeka bila woga, vitisho au vishawishi, pamoja na kutokukubali kutishwa na mtu au asasi yoyote katika kuitetea, kuilinda Katiba na sheria za nchi.nipashe

No comments: