Friday, April 14, 2017

CHADEMA NA ACT-WAZALENDO WAGUSHWA NA MAUAJI YA POLISI

CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA)

SALAMU ZA RAMBIRAMBI NA POLE KWA VIFO VILIVYOTOKEA JANA NA LEO VYA POLISI NA NDUGU JOSEPHAT ISANGO- MWANDISHI.

CHADEMA tumepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za vifo vya Askari wa Jeshi la Polisi wanane vilivyotokea jana huko maeneo ya Rufiji Mkoani Pwani kwa kile kilichoelezwa awali kuwa ni kutokana na shambulizi la kuvizia linalosemekana limefanywa na Jambazi/ Majambazi. 

Taarifa hizi sio tu kuwa ni za kuogofya bali pia ni za kuhuzunisha na kusikitisha hasa ikitiliwa maanani kuwa ni miezi michache tu iliyopita tukio la kihalifu kama hili lilitokea maeneo hayohayo na taifa likapoteza Askari wake wengine. 

Tunachukua nafasi hii kulaani kitendo hiki ambacho kimefanywa na watu au mtu mwoga na ambacho kimepelekea kukatiza maisha ya Askari wetu ambao walikuwa kwenye majukumu yao ya kuimarisha ulinzi wa raia na Mali zao.

CHADEMA tunatoa salamu za pole na Rambirambi kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP,  Ernest Mangu kwa msiba huu mkubwa ambao sio tu kuwa ni pigo kwa taifa bali ni muendelezo wa matukio ambayo yanaashiria kuwa usalama wetu uko katika mtikisiko au mashaka makubwa .

Tunamtaka IGP afanye uchunguzi wa kina na achukue hatua stahiki juu ya matukio yote ambayo yamekuwa yakihatarisha usalama wa raia na Mali zao hapa Nchini kwa muda mrefu sasa na yaweze kukomeshwa mara moja kwani watanzania hatujazoea matukio ya kihalifu kama yanavyoendelea kutokea nchini mwetu.

Jeshi la Polisi linatakiwa kujipanga upya ili kuzuia matukio kama haya kutokea ama kwa Polisi wenyewe au kwa raia wengine kwani hili ni jukumu Lao la msingi na wasiogope kuchukua hatua kwa yeyote anayepanga na kiratibu matukio ya kihalifu kama utekaji,  utesaji na hata mauaji kama tunavyoendelea kushuhudia nchini kwa kipindi sasa kwani uhalifu hauna cheo,  hakuna aliye juu ya sheria nchini mwetu.

Josephat Isango.

CHADEMA inapenda kutoa pole kwa msiba mwingine mkubwa uliolikumba taifa kwa kuondokewa na Mwandishi mwandamizi wa Habari na ambaye alikuwa na ujasiri wa aina yake katika kuchunguza na kufichua maovu mbalimbali  Ndugu Josephat Isango Nghimba. 

CHADEMA daima tutamkumbuka katika harakati zake mbalimbali tangu alipokuwa mmoja wa waasisi wa CHASO katika Chuo Kikuu cha SAUT Mwanza alipokuwa mwanafunzi na hata alipohitimu alikuwa Mwenyekiti wa Vijana (BAVICHA ) Mkoani Singida.

Atakumbukwa kwa ujasiri wake ndani ya Chama aliposimamia kamati ya maadili ya Baraza la Vijana CHADEMA , wakati wa kushughulikia nidhamu ya waliokuwa wanachama wa Baraza hilo akina Juliana Shonza na wenzake .

Tunatoa salamu nyingi za pole kwa waandishi wote wa Habari nchini na wamiliki wa vyombo vya Habari vyote nchini kwa kuondokewa na mmoja wa mwanafamilia mwenzenu katika tasnia ya Habari. 

Zaidi sana tunatoa pole kwa waliowahi kuwa waajiri wake ambao ni kampuni za Freemedia, Mwanahalisi Publishers, Victoria Media (Mawio) na Jamii Media (Jamii forums) alikowahi kufanya kazi .

Hakika sote tumeondokewa na kijana mahiri na ambaye alikuwa hana woga katika kutimiza majukumu yake na katika kupigania uhuru na haki ya kupata Habari nchini. 

Mwisho tunatoa pole kwa watanzania wote kwa msiba huu ambao umetukumba sote , tunaungana na Ndugu na jamaa katika kipindi hiki kigumu kwa familia zote zilizoguswa kwa njia moja ama nyingine na msiba huu katika Dua zetu. 

John Mrema -Mkurugenzi wa Uenezi, Mawasiliano na Mambo ya Nje CHADEMA .

Imetolewa Leo Ijumaa, Aprili 14, 2017.
--------------------------------------
KUTOKA ACT WAZALENDO/
Watanzania Tushikamane Wakati Huu wa Majonzi ya Kupoteza Askari Wetu
Chama cha ACT Wazalendo kimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kushambuliwa na kuuawa kwa askari 8 wa jeshi la Polisi jana jioni katika eneo la Jaribu Mpakani, wilayani Kibiti, mkoa wa Pwani.

Chama cha ACT Wazalendo kinatoa pole kwa familia za mashujaa wetu hawa 8 waliouawa wakati wakilinda usalama wetu wananchi, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Ernest Mangu pamoja na Jeshi zima la Polisi.

ACT Wazalendo tunaungana na wito wa kuwataka Watanzania kushikamana na vyombo vya ulinzi na usalama katika kipindi hiki cha majonzi kwa Taifa pamoja na kutoa ushirikiano kwao kuhakikisha matendo ya namna hii yanakomeshwa.

Tunachukulia kitendo hiki Kama kitendo cha shambulio dhidi ya Jamhuri yetu na hatua kali na madhubuti zinapaswa kuchukuliwa. 

Mlolongo wa matukio ya namna hii unaonyesha kuwa nchi yetu inapambana na kundi lisilo la kawaida na hivyo weledi wa hali ya juu unatakiwa katika kukabiliana na tishio hili dhidi ya Jamhuri yetu. Jeshi la polisi linatakiwa kufanya kazi zake Kwa uangalifu mkubwa na kuepuka kabisa na kuwaingiza raia wasio na hatia kwenye mateso yeyote kwani adui asipopatikana madhara yake ni makubwa zaidi. Matukio ya aina hii katika miezi ya hivi karibuni yawe funzo katika kukabiliana na uhalifu Kama huu. Tunatahadharisha kutotumia mwanya huu kuingiza wasiohusika kwani kufanya hivyo ni kuwapa ushindi wahalifu. 

ACT Wazalendo tunaamini Jeshi letu la Polisi litahakikisha linawasaka, kuwakamata na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria wote waliohusika na mauaji haya ya askari wetu.

Mohammed Said Babu
Katibu, Kamati ya Amani na Usalama - ACT Wazalendo
Aprili 14, 2017
Dar es salaam

No comments: