Wednesday, April 19, 2017

HIVI NDIVYO INTANETI INAVYOATHIRI MAISHA YAKO YA KILA SIKU

Na Jumia Travel Tanzania

Hakuna kitu kinachoudhi kama kuwa sehemu na marafiki, familia au ndugu lakini unakuta kila mtu ameinamia skirini ya simu yake! Kwa kiasi kikubwa kuja kwa mtandao wa intaneti kumewafanya watu kujikita zaidi na simu zao badala ya watu au kufaidi mazingira yanayowazunguka.

Kuna tafiti nyingi zimekwishafanyika na kuthibitisha kuwa muda mwingi unaotumika kwenye intaneti una madhara kama vile ya kimwili na kiakili. Mbali na kuwepo kwa faida lukuki za mtandao huo, Jumia Travel ingependa kukujulisha kuwa yafuatayo yanaweza kukumba endapo utautumia vibaya: 
Intaneti husababisha hali ya kujisikia vibaya, kukosa furaha na wivu. Mtu anaweza kushangaa na kujiuliza hii inaweza kutokeaje. Jibu ni rahisi sana. Mambo tunayoyaona kwenye mitandao ya kijamii yanayowekwa na watu maarufu, ndugu, jamaa au marafiki wa karibu huweza kukukosesha furaha kwa namna moja ama nyingine. Hebu jaribu kufikiria unamuona rafiki yako wa karibu ameweka picha zake akiwa amesafiri sehemu ambayo wewe hujawahi kufika au chakula usichowahi kukila utajisikiaje? Ingawa sio wote wanaoweza kujisikia vibaya lakini kwa asilimia kubwa wengi wao hupatwa na wivu au kusononeka nafsi kuona kwamba inawezakana wao wasije kuwa na maisha kama yale. 
Intaneti husababisha watu wengi kujihisi kuwa wanapitwa na wakati. Tangu enzi za kale kila nyakati zimekuwa na mitindo tofauti ya maisha hapa duniani. Kwa bahati mbaya sio watu wote ambao wanao uwezo wa kuendana na mitindo au fasheni zilizopo. Hali hii imewafanya wengi kujihisi kupitwa na wakati endapo wasipoishi kama wanavyoona kwenye mitandao. Kupitia mitandao ya kijamii kama vile Instagram watu wanaweza kuwashirikisha wenzao picha na video za namna wanavyoishi kuendana na wakati. Ambapo mara nyingi yale yanakuwa sio uhalisia wa maisha yao.    

Intaneti imekuwa ni chanzo kikubwa kwa watu wengi kutokuwa na utulivu wa akili. Nadhani hii hali inawakuta watu wengi katika maisha yao ya kila siku katika ulimwengu wa sasa wa intaneti. Kuna wakati unajaribu kujikita kwenye suala fulani lakini shughuli zinazoendelea mtandaoni kupitia simu yako ni kikwazo kikubwa. Kwa mfano, unataka kukamilisha kazi uliyopewa na bosi wako, mara ujumbe wa Whatsapp umeingia, hujatulia Facebook, Twitter na Instagram nazo zote zinakujulisha kuwa unapitwa huku. Kwa hali hii sidhani kama kuna jambo ambalo mtu anaweza kulikamilisha kwa ufanisi na usahihi unaohitajika.
Intaneti inawanyima watu fursa ya kufurahia maisha halisi yanayowazunguka. Kwa sasa ni jambo la kawaida kabisa sasa kuona familia imekwenda hotelini kupata chakula pamoja na kubadilisha mazingira ya nyumbani lakini ukakuta kuanzia watoto mpaka wazazi wote wameinamisha nyuso zao kwenye skirini za simu zao. Hakuna tena ile hali ya zamani kwamba muda wa chakula ndipo familia hukutana kwa pamoja, kuzungumza, kucheka na kubadilishana mawazo juu ya yale waliyoyapitia siku nzima. Kwa hali ilivyo sasa hivi huwezi kusikia tena vicheko au gumzo kwenye familia nyingi kwani vyote hivyo vimeamia kwenye simu. Usishangae ukamuona mtu anacheka mwenyewe ukadhahania ni punguani, hapana, ni mambo ya intaneti hayo.

Intaneti imekuwa ni chanzo kikubwa cha watu kutokuwa wabunifu katika masuala mbalimbali. Hebu jaribu kufikiria ingekuwaje kama hizo video unazozitazama kupitia YouTube, habari unazoziona Facebook au Twitter, au picha unazoziona kupitia Instagram; vyote hivyo ungevipataje kama waliogundua nao wangekuwa wanatumia muda wao kwenye intaneti kupitia kazi za wenzao. Hii inamaanisha kwamba hatupaswi kutumia muda mwingi kuwa watumiaji wa vitu vya kwenye intaneti badala yake nasi tuwe wazalishaji ili kuwanufaisha na wengine zaidi. Unaweza kukuta mtu tangu siku inaanza mpaka inaisha yeye anaimaliza kwenye mitandao ya kijamii akipitia, kutazama na kusoma habari za watu wengine.
Yaliyozungumzwa katika makala haya ndio maisha ya wengi kwa sasa jinsi yalivyoathiriwa na kuja kwa intaneti. Lakini zipo mbinu kadhaa za kuweza kujiepusha na madhila hayo yote. Jumia Travel inashauri kwamba jukumu la mtu kuepukana na uraibu wa matumizi ya intaneti ni la kwake mwenyewe. Kwa mfano, kujiwekea au kutenga muda maalumu wa kuingia mtandaoni, kuzima ishara zitokanazo na mitandao ya kijamii au kuzima kabisa intaneti kwenye simu yako mpaka muda fulani inaweza kusaidia pia.   

No comments: