Monday, July 31, 2017

UNAITUMIAJE TEKNOLOJIA KURAHISISHA SHUGHULI ZAKO ZA KILA SIKU?



Na Jumia Travel Tanzania

Kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia binadamu waliyonayo kwa sasa si jambo la kushangaza kumuwezesha mtu akafanya shughuli zako zote akiwa yupo sehemu moja ndanin ya muda mfupi.

Kwa mfano, kwa kutumia simu yako ya mkononi unaweza kutatua changamoto kadhaa hapo nyumbani kwako kama vile kufanya miamala ya fedha kutoka benki na kisha kutoa kwa mawakala huduma za fedha, kulipia umeme, kulipia maji, kulipia king’amuzi, kuagiza chakula, kuagiza usafiri, kufanya manunuzi ya bidhaa na huduma mbalimbali.

Lakini swali ni kwamba, je ni watanzania wangapi wanaiona fursa hiyo iliyoletwa na teknolojia kama suluhu za changamoto tofauti zinazowazunguka?


Jibu ni kwamba ni watu wachache sana walioyapokea maendeleo yaliyoletwa na teknolojia na kuyatumia katika kurahisisha maisha yao ya kila siku. Ni jambo la ajabu kuona kwamba mtu ameishiwa na umeme nyumbani kwake lakini hana suluhu yoyote zaidi ya kwenda kwa mawakala wa huduma za malipo wakati yeye mwenyewe anao uwezo wa kufanya hivyo kwa kutumia simu yake ya mkononi.

Zipo sababu kadha wa kadha zinazopelekea watu wengi kushindwa kuzitumia huduma hizi ipasavyo mojawapo ikiwa ni elimu ya kuweza kuitumia mifumo na programu hizo. Ila kwenye suala la elimu sidhani kama ni hoja ya msingi kwa sababu mifumo takribani yote ni rahisi kwa mtumiaji na kikubwa zaidi ni kwamba ukiwa unaitumia mara kwa mara inazoeleka kwani hakuna kinachobadilika.
Kampuni ya Jumia ambayo imejikita kwenye masuala ya biashara kwa njia ya mtandao barani Afrika katika nyanja za hoteli na usafiri, manunuzi ya bidhaa, kazi, makazi, magari, chakula na matangazo mbalimbali imetimiza miaka mitano (5) tangu kuanzishwa kwake.

Katika maadhimisho ya sherehe hizo kampuni hiyo imekuwa ikifanya mikutano kwa njia ya ‘video za moja kwa moja’ na wataalamu na waasisi wa makampuni mbalimbali ya kiteknolojia duniani. Lengo kubwa likiwa ni kupata ushauri, uzoefu na mitazamo juu ya ukuaji wa sekta hiyo na mustakabali wake barani Afrika.

Mojawapo ya wageni walioalikwa kwenye mfululizo wa ‘video’ hizo alikuwa ni Afisa Mtendaji Mkuu na mwasisi mwenza wa 

Andela, Bw. Jeremy Johnson ambayo ni kampuni iliyoanzishwa kwa madhumuni makubwa ya kuwafunda watengeneza program barani Afrika (Softwarfe Developers) na kisha kuwaunganisha na makampuni yenye uhitaji wa wataalamu hao. Mpaka hivi sasa Andela imefungua matawi yake katika nchi tatu ambazo ni Nigeria (Lagos), Kenya (Nairobi) na mapema mwaka huu waliongeza tawi lingine jijini Kampala, Uganda.

Bw. Johnson katika mazungumzo yake na wafanyakazi wa Jumia alieleza kwamba mojawapo ya vigezo wanavyoviangalia mpaka wanafikia hatua ya kufungua tawi nchi husika ni baada ya kufanya utafiti wa kutosha wa maendeleo ya teknolojia pamoja na shauku ya wananchi wa eneo husika katika kuitumia ili kutatua changamoto mbalimbali za maisha yao ya kila siku.

Hoja ya msingi iliyoainishwa na mwasisi huyo ambayo Jumia Travel imeibaini katika mazungumzo yake ni utayari na shauku ya watu kutumia teknolojia. Kwa hoja hiyo kwa haraka haraka tunaweza kuona kwamba nchi za Nigeria na majirani zetu wa Kenya wametuacha hatua kadhaa katika kuyapokea mabadiliko ya kiteknolojia na kuyatumia ipasavyo. Na suala hilo ni mojawapo ya sababu zinazopelekea makampuni kadhaa kuanzia katika nchi hizo kabla ya kuvuka mpaka na kuja nchi nyingine ikiwemo Tanzania.
Imefikia mahali sasa watanzania kubadilika na kuyapokea mabadiliko yanayoletwa na teknolojia hususani mtandao wa intaneti katika kurahisha maisha yetu ya kila siku. Zipo huduma nyingi ambazo unaweza ukazipata kwa kubonyeza tu vitufe vya simu yako mahali popote ulipo na ukazipata. 

Tukumbuke kwamba mabadiliko haya yote huja kwa malengo ya kufanya shughuli zetu ziwe rahisi tofauti na awali na ndiyo maana watu wanaendelea kufanya uvumbuzi kila kukicha. 

No comments: