Monday, August 14, 2017

NAIBU SPIKA TULIA ACKSON AMEZINDUA MRADI WA UHAMASISHAJI DHIDI YA ATHARI ZA NDOA ZA UTOTONI NA UKEKETAJI

Shirika lisilo la kiserikali la jukwaa la utu wa mtoto (CDF) likishirikiana na halamashauri ya manispaa ya Ilala limezindua mradi wa uhamasishaji dhidi ya athari za ndoa za utotoni na ukeketaji katika kata ya kitunda wilaya ya Ilala jijini Dar es salaam.
Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Tulia Ackson akiongea na wageni waalikwa mapema leo kwenye uzinduzi wa mradi wa uhamasishaji dhidi ya athari za ndoa za utotoni na ukeketaji katika kata ya Kitunda
Mradi huo uliofadhiliwa na ubalozi wa uholanzi, kwenye utekelezaji wake utaanza kwa kuelimisha jamii na kuihamasisha juu ya madhara ya mimba za utotoni, ndoa za utotoni na ukeketaji pamoja na kutafuta ufumbuzi wa kuwalinda wasichana dhidi ya madhara hayo.

Tafrija hiyo fupi iliyofanyika hoteli ya Lamada iliyopo Ilala jijini Dar es salaam na mgeni rasmi akiwa ni Naibu Spika wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Tulia Ackson, na kuudhuliwa na wadau toka taasisi mbalimbali za kiserikali na binafsi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Jukwaa la Utu wa Mtoto (CDF) Mr.Koshuma Mtengeti akiongea na wageni waalikwa mapema leo Hoteli ya Lamada jijini Dar es salaam
Kwa nchi nzima ya Tanzania mkoa wa Dar es salaam unashika nafasi ya 20 kwa kuwa na watoto wengi walioolewa wakiwa na umri mdogo wa miaka chini ya 18 kwa kuwa na asilimia 19.

Lakini kwa ndani ya jiji la Dar es salaam lenye wilaya tano wilaya inayoongoza kwa kuwa na ndoa nyingi za utotoni ni wilaya ya Ilala na kata inayoongoza kwenye wilaya hiyo ni Kitunda na kutokana na kuwepo na vitendo vya ukeketaji vinavyosababisha kuwepo kwa ndoa za utotoni ndio sababu ya mradi huu kuanzia kwenye kata hiyo.
Naibu Balozi wa Uholanzi Bi.Lianne Houben akitoa ufafanuzi wa jambo kwenye uzinduzi wa mradi wa uhamasishaji dhidi ya athari za ndoa za utotoni na ukeketaji katika kata ya Kitunda mapema leo jijini Dar es salaam.
Katika kukabiliana na changamoto hizi za mimba za utotoni, ndoa za utotoni na ukeketaji kwenye kata ya Kitunda mradi utahusisha wadau mbalimbali ikiwemo Serikali, mashirika mbalimbali yanayojihusisha na haki na ustawi wa mtoto, viongozi wa kidini, kimila na vyombo vya habari kwa ujumla.

Lengo kuu la mradi huu ni kuhakikisha jamii ya kata ya Kitunda inakuwa mstari wa mbele katika kutokomeza mimba za utotoni, ndoa za utotoni, ukeketaji na ukatili wa kijinsia na vitendo vyote vinavyowaathiri watoto wa kike, na kuhakikisha watoto wa kike wanazitambua haki zao na kuzitetea.
Naibu spika Mh. Tulia Acksoni akijiandaa kukata utepe ishara ya kuzindua mradi huo.
Mradi huu uliofadhiliwa na ubalozi wa Uholanzi unatarajia kuafikia watoto 100 wenye umri kati ya miaka 12-16, wasichana 50 wenye umri wa miaka 15-19, wananwake 50 wenye umri wa 20-24, wanaume na watoto wa kiume 100 wenye umri wa miaka 15-24 waliopo kwenye sehemu husika na jamii yote kwa ujumla.
Naibu Spika Mh. Tulia Ackson akiwa amekata utepe ishara ya kuwa amezindua rasmi mradi huo mapema leo jijini Dar es salaam
Baadhi ya matokeo tarajiwa ya mradi huu ni pamoja na kuongezeka kwa ujuzi na maarifa kwa wasichana na wanawake walioko hatarini au waliokwisha athirika na ndoa za utotoni juu ya kufanya maamuzi sahihi kuhusiana na haki zao za afya ya uzazi.

Pia mradi huu unatarajia kuona watunga sera na wafanya maamuzi katika ngazi ya chini na ngazi ya juu ya serikali wanaonyesha ushirikiano kwa kuwawezesha wasichana kwa kuongeza miradi mbalimbali ya kutokomeza ndoa za utotoni katika wilaya pamoja na mkoa.

 
baadhi ya wageni waalikwa walioudhuria semina hiyo mapema leo jijini Dar es salaam




Wafanyakazi wa shirika la Jukwaa la Utu wa Mtoto(CDF) wakiwa kwenye picha ya pamoja na meza kuu mapema leo jijini Dar es salaam



No comments: