Monday, August 14, 2017

RAIS MAGUFULI, DANGOTE, OBAMA KUHUDHURIA SHEREHE ZA KUAPISHWA KWA KENYATTA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Dkt John Magufuli na Rais mstaafu wa Marekani, Barack Obama ni miongoni mwa viongozi wanaotarajiwa kuhudhuria katika sherehe za uapisho wa Rais mteule wa Kenya, Uhuru Kenyatta.

Kamati ya maandalizi ya sherehe hizo inayoongozwa na Katibu Kiongozi, Joseph Kinyua imebainisha kuwa imeandaa orodha ya majina ya viongozi wa kimataifa kwa ajili ya kushuhudia tukio hilo la kihistoria la uapisho wa Kenyatta endapo ushindi wa Kenyatta hautopingwa mahakamani.

Kwa mujibu wa Katiba ya nchi hiyo, sherehe za uapisho hufanyika siku 14, baada ya mshindi wa uchaguzi kutangazwa ili kutoa fursa kwa chama chochote kinachotaka kupinga matokeo kufanya hivyo.

Viongozi wengine wanaotarajiwa kualikwa katika sherehe hizo wakiwemo wakuu wa nchi ni pamoja na Rais wa Rwanda Paul Kagame, Rais wa Uganda Yoweri Museveni, Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma na Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari. Wengine ni Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May.

Aidha, katika orodha hiyo pia yupo Rais wa Liberia, Ellen Johnson Sirleaf, mfanyabiashara tajiri namba moja Afrika Aliko Dangote, Kiongozi wa Jumuiya ya Ismailia, Aga Khan, Waziri Mkuu mstaafu wa Italia, Matteo Renzi na Rais Xi Jinping wa China.
“Tupo kwenye maandalizi ya sherehe za uapisho wa Rais wakati tukisubiria hatua za kikatiba kukamilika. Orodha hii ni ya marafiki wa Kenyatta, viongozi wa Afrika na viongozi wengine wa kimataifa, tunaotarajia kuwaalika”, amesema mmoja wa wanakamati hiyo ya maandalizi.


Mwenyekiti wa Tume Huru ya Mipaka na Uchaguzi Kenya, Wafula Chebukati mwishoni mwa wiki alimtangaza rasmi Rais Kenyatta na Naibu wake, William Ruto kuwa washindi katika uchaguzi uliofanyika wiki iliyopita nchini humo.

No comments: