Sunday, August 20, 2017

Tundu Lissu na Zitto Kabwe wamezuia "Bombadier yetu" kufika?Zitto ameamua kuyajibu haya leo

Suala la ndege yetu kuzuiwa nchini Canada lisifanywe ni suala la ushabiki kama ushabiki wa mpira. Ni suala la Nchi hili, na mjadala wake ni lazima uwe na hadhi hiyo. Kitendo cha Kaimu Msemaji wa Serikali kulaumu wanasiasa kwa jambo la kisheria kama hili ni utoto. Historia yetu inaonyesha hakuna mwanasiasa (hasa wa upinzani) anayeweza kushirikiana na kampuni za kigeni kuhujumu nchi.
Falsafa ya chama ninachokiongoza, ACT Wazalendo, ni 'Taifa Kwanza, Leo ni Kesho'. Mimi binafsi filosofia yangu ni rahisi sana 'My Country First, Right or Wrong' (Nchi Yangu Kwanza, Kwa Usahihi au Kwa Makosa). Maneno yanayosambazwa kuwa nimeshiriki kuwezesha ndege ya Bombardier iliyonunuliwa na Serikali Kwa niaba ya ATCL kukamatwa huko Canada ni takataka tu zinazosambazwa na wapika propaganda. Ni upuuzi!
Serikali lazima ifahamu kuwa ni lazima ihojiwe, na iwe tayari kutoa majibu. Sisi kama vyama vilivyo Nje ya Serikali ni wajibu wetu kuhoji jambo lolote. Pia ni haki yetu kupata Taarifa zozote kutoka mahala popote zitakazosaidia kuisimamia Serikali. Wajibu wa Serikali ni kujibu hoja zinazoibuliwa nasi. Majibu ya Msemaji wa Serikali yanataka kuligeuza suala hili kuwa la kisiasa na watu wameangukia kwenye ushabiki huo.
Tusikubali kuingia kwenye huu ushabiki. Hili ni suala la kisheria, na ni suala la nchi ambayo sisi wote tuna maslahi ya kuona inakwenda mbele.
Nchi yetu kudaiwa sio dhambi. Hata mataifa makubwa duniani yanadaiwa. Watu binafsi tunadaiwa sembuse Serikali? Mimi binafsi ninadaiwa madeni ya uchaguzi mpaka sasa, na wengine (kati ya wanaonidai) wamenipeleka mahakamani. Sio dhambi kudaiwa.
Muhimu ni (1) Je Deni limetokana na Nini? Ni maamuzi mabovu ya kisiasa? (2) Unalipa deni hilo au kuweka mikakati ya kulipa?
Serikali yetu inafahamu kuwa nchi yetu ina madeni mengi, na miongoni mwa madeni hayo yapo ambayo yameshaamuliwa na Mahakama. Kinachopaswa ni kuwa na MAARIFA ya kupita ili kuzuia Mali zetu nje ya nchi kuzuiwa kama ilivyo Kwa Ndege hii.
Serikali iwe wazi kuhusu suala hili la Ndege. Je ile ya Boeing (Terrible Teen) ipo salama? Madeni mengine yenye amri ya mahakama ni yepi? Kwanini Serikali inasubiri kuhojiwa ndipo itoe Taarifa?
Hii ni nchi yetu sote. Hakuna mwenye hatimiliki ya ukweli. Ukweli pia haupendi kupindwapindwa. Serikali itoke kueleza nini kimetokea mpaka Ndege kuzuiwa, iachane na tabia ya hovyo ya kutafuta mchawi 'kwamba eti wanasiasa ndio wamesababisha'. Kutafuta mchawi ni kutowajibika kwa maamuzi ya Serikali yenyewe.
Kabwe Z. Ruyagwa Zitto
Kiongozi wa Chama - ACT Wazalendo
Jimboni Kigoma Mjini
Agosti 20, 2017

No comments: