Monday, August 7, 2017

Waethiopia 72 Wanaswa Chalinze Wakiingia nchini


HUKU serikali ikiwa inaweka mikakati ya kukabiliana na wimbi la wahamiaji haramu nchini, Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani limewakamata wahamiaji haramu 72 kutoka Ethiopia kwa tuhuma za kuingia nchini bila ya kibali.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye Kituo cha Wilaya ya Kipolisi Chalinze, Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Jonathan Shana alisema wahamiaji hao walikuwa safarini kwenda Afrika ya Kusini.

Kamanda Shana alisema wahamiaji hao walikamatwa Jumamosi saa 3:30 asubuhi kwenye Pori la Ranchi ya Taifa (NARCO) Kata ya Vigwaza, Chalinze wilayani Bagamoyo. “Mbali ya wahamiaji hao haramu, pia tunamshikilia Rajabu Hitaji (30) mkazi na mfanyabiashara wa Vigwaza baada ya msako mkali uliofanywa na makachero wa Jeshi la Polisi baada ya kupata taarifa kuwa kuna wahamiaji haramu wameingia bila ya kibali,” alisema Kamanda Shana.

Alisema wahamiaji hao haramu baada ya kugundua kuwa kuna gari la polisi linawafuatilia, waliingia kwenye hifadhi hiyo kwa lengo la kujificha, lakini msako mkali uliofanywa uliwabaini na kukamata kundi la kwanza la watu 63 ambao walikaa sehemu ambayo gari haliwezi kufika.

“Baada ya kuwakamata wahamiaji hao haramu kundi la kwanza askari waliendelea na msako ambapo waliwakamata wahamiaji wengine tisa waliokuwa wakijaribu kutaka kutoka kwenye pori hilo,” aliongeza Kamanda Shana. Alisema wahamiaji hao haramu wanatarajiwa kukabidhiwa Idara ya Uhamiaji kwa ajili ya hatua za kisheria pamoja na mfanyabiashara aliyekamatwa anayetuhumiwa kuwasafirisha.

No comments: