Monday, October 22, 2012

                                                               TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

   


            Mpambano unaosubiriwa kwa hamu kubwa na wadau wa ngumi nchini Tanzania na Ujerumani kati ya Francis Cheka na Benjamin Simon wa Ujerumani sasa utafanyika tarehe 18 Novemba mwaka huu katika ukumbi wa Universal jijini Berlin nchini Ujerumani.
Awali mpambano huo ulikuwa ufanyike tarehe 17 Novemba mwaka huu jijini Berlin, Ujerumani na tayari bondia Francis Cheka ameshasaini mkataba wa kukutana na mbabe huyo wa Ujerumani anayejulikana kwa jina la “Iron Ben” kwa ajili ya ukali wa makonde yanayowasulubu wapinzania wake.
Bondia Benjamin Simon ana rekodi ya mapambano 24 ambapo amepoteza pambano moja wakati bondia Francis Cheka ana rekodi ya mapambano 33 amepoteza mapambano 6.
Akimwandikia “Eva Rolle” wa kampuni ya “Primetime Event Management” ya Ujerumani ambaye ndiye promota wa mpambano huo, mwenyekiti wa ubingwa wa IBF/USBA Lindsey Tucker alimfahamisha kuwa Rais wa IBF/USBA Daryl Peoples au yeye mwenyewe Lindsey Tucker watawasiliana na mama huyo kuhusu maofisa watakaosimamia mpambano huo.
Hii itakuwa mara ya kwanza kwa wababe hao kukutana kugombea mkanda wa IBF wa mabara (IBF I/C) na mpambano wao unategemnea kutoa ushindani mkubwa.
Mshindi katika mpambano huo ataingia moja kwa moja katika orodha ya mabondia 15 bora kwenye uzito wa Super Middle duniani.
Imetumwa na:
Onesmo Alfred McBride Ngowi
Rais IBF Africa, Mashariki ya Kati, Ghuba ya Uarabu na Uajemi
(IBF Africa, Middle East, Arabian Gulf and Persian Gulf)

No comments: