Wednesday, April 17, 2013

SOMA HISTORIA NDEFU YA MAREHEMU FATUMA BINT BARAKA BIBI KIDUDE

 

       Bi Kidude ni gwiji wa muziki katika Bara la Afrika. Jina lake halisi ni Fatuma binti Baraka. (Mwaka aliozaliwa haujulikani ila anakisiwa kuwa na umri wa miaka 102. amefariki 17 Aprili 2013, Bubu huko Zanzibar).
Bi Kidude ni msanii mkongwe na mahiri sana katika fani ya muziki wa mwambao ambao hujulikana kwa jina la Taarabu,  Muziki huu ambao ni mchanganyiko wa muziki toka nchi za Kiarabu na vionjo vya muziki wa Kiafrika umekita sana katika mwambao wa Afrika Mashariki yaani Zanzibar, Mombasa, Lamu na kwingineko.









Marehemu Bi Kidude - EnzI ZA Uhai wake

Fatuma binti Baraka au Bi Kidude, alizaliwa katika kijiji cha Mfagimarigo Zanzibar katika familia ya watoto saba (7).
Baba yake Mzee Baraka alikuwa ni mfanyabiashara wa nazi, zao ambalo ni la kutumainiwa sana Zanzibar.
Bi Kidude anasema hafahamu tarehe halisi aliyozaliwa, isipokuwa anachojua ni kwamba alizaliwa wakati rupia ikitumika kama fedha, na vilevile ana hakika ni kabla ya Vita Kuu ya Kwanza ya Ulaya.
Wataalamu wa mahesabu baada ya kupata taarifa hizo wakampigia mahesabu na kumkabidhi miaka yake kwamba ni zaidi ya miaka 90.
Bi Kidude enzi za uhai wake alisema uimbaji aliuanza tangu alipokuwa na umri wa miaka kumi na alijifunza kutoka kwa msanii mkongwe na aliyetamba sana enzi hizo Sitti binti Saad.
        

              Alisema wageni wengi kutoka sehemu mbalimbali walikuwa wakifika Zanzibar kuja kumwona Sitti, na kwa vile Bi Kidude na Sitti walikuwa wako karibu basi yeye alikuwa akiwapeleka wageni wale nyumbani kwa Bi Sitti, wakifika huko wageni walikuwa wakiingia ndani na yeye kubakia nje, kule ndani Bi Sitti alikuwa akiwaimbia wale wageni, na yeye huku nje alikuwa akimsikiliza kwa makini na kumfuatiliaa jinsi alivyokuwa akiimba. Aliendelea hivyo hadi akawa mahiri sana katika uimbaji.

       Alipokuwa na miaka 13, kwa mara ya kwanza alitoroka nyumbani kwao Zanzibar na kukimbilia Tanzania Bara, baada ya kulazimishwa kuolewa. Lakini alipokuwa kigoli wa kutosha kuolewa aliolewa ingawa ndoa hiyo nayo haikudumu kutokana na manyanyaso aliyokuwa akiyapata, hivyo aliamua kukimbilia kaskazini mwa Misri ikiwa ni katika miaka ya 1930, huko aling'ara sana katika fani yake ya uimbaji na uchezaji ngoma. Lakini ilipofika miaka ya 1940 aliamua kurudi nyumbani Zanzibar ambako aliendelea na shughuli zake uimbaji.
 

          Marehemu Bi Kidude alikuwa hategemeitegemei kazi moja tu ya kuimba, kwani pia alikuwa ni  mfanyabiashara wa 'wanja' na 'hina' ambavyo alikuwa anavitengeneza yeye mwenyewe.
Vile vile alikuwa ni  mtaalamu wa matibabu kwa dawa za mitishamba na zaidi ya hayo alikuwa ni mwalimu mzuri sana wa 'Unyago' na alianzisha chuo chake mwenyewe na alisema katika wanafunzi wake wote hakuna aliyewahi kupata talaka kutoka kwa mumewe.
Watu wanasema 'Utu uzima dawa' Bi Kidude alikuwa ana upeo mkubwa sana wa akili kwani pamoja na kukulia katika mazingira yaliyogubikwa na tamaduni za kiarabu ambapo mwanamke alikuwa anatakiwa wakati wote akiwa hadharani ajifunike, Bi Kidude aliliona hili katika upeo mwingine kwamba ni sheria tu ya kitamaduni toka Uarabuni, hivyo aliamua kuvunja sheria hiyo na kuondoa hijabu mwilini mwake, na sasa akawa  anavaa kama Mtanzania na si kama Mwarabu.
      

                 Lakini hakubakia hapo alivunja na miiko mingine zaidi ya kutokunywa na kuvuta, kwani Bi Kidude alikuwa anakunywa pombe na kuvuta sigara jambo ambalo si kawaida kwa wanawake Zanzibar.
Bi Kidude amekwisha tembelea nchi nyingi sana ikiwa ni pamoja na Oman, Ufaransa, Hispania, Ufini, Ujerumani na Uingereza.
Vile vile amekwisha pata tuzo mbalimbali ikiwa ni pamoja na ile ya Tamasha la Filamu la Nchi za Jahazi (ZIFF) mwaka 1999 tuzo ni ya maisha, Pia mwaka jana tuzo ya WOMAX ilienda kwake.
Nyimbo alizowahi kuimba ni pamoja na Muhogo wa jang'ombe, na anaimba kwa Kiswahili na Kiarabu. Hakuwahi kupata elimu nyingine zaidi ya Kurani.

KWA HISANI YA MR SEMVUA MSANGI BLOG

No comments: