Wednesday, November 27, 2013

BANDARINI MAJANGA ,MPANGO WA KUSUKA UFISADI WANASWA,MSUGUANO MKUBWA WAIBUKA,SOMA ZAIDI

Na Karoli Vinsent

    MSUGUANO umeibuka ndani ya Bandari Tanzania (TPA) kutokana na kuwepo tuhuma za maandalizi ya manunuzi ya kifisadi kupitia kitengo cha manunuzi cha mamlaka hiyo, imefahamika.
 soma zaidi hapo chini---------


     Tuhuma hizo zimeibuka baada ya kuwapo kwa hatua za kufanya mabadiliko katika kitengo hicho na kuingizwa kwa watu ambao waliingia TPA katika mazingira tata, wakitokea maeneo alikotokea mmoja wa viongozi wa mamlaka hiyo.

         Kabla ya kuingia kwa uongozi mpya chini ya Kaimu Mkurugenzi Mkuu, Madeni Kipande, ziliibuka tuhuma za kuunda kitengo cha manunuzi (Management Procurement Unit-PMU) kwa ajili ya maslahi binafsi.

      “Kilichofuata ni Kipande akiungwa mkono na wizara kuvunja PMU na Bodi za Ununuzi Bandari ya Dar es Salaam na Makao Makuu na kuunda Bodi Kuu ya Zabuni (CTB) wakidai uamuzi huo utakuwa  muarobaini wa rushwa na ufisadi na hakutakuwepo athari zozote kiutendaji.  “Wahenga husema mtoto akililia wembe mpe ajikate na sasa mambo yamebadilika,” anasema ofisa mwandamizi wa TPA.

       Imeelezwa kwamba ndani ya mwaka mmoja sasa Kipande ameanza kulaumu kuwa Bodi ya Zabuni ya TPA inakwamisha ununuzi na hivyo kukwamisha ufanisi ndani ya TPA.

       “Lawama hizo hata hivyo hazikuwa za ukweli kwa vile sheria ya ununuzi iko wazi, na CTB ilikuwa inaeleza wazi kuwa inaongozwa na sheria hiyo.

     “Kipande na watu wake wakashindwa kufanya wanachotaka wao na sasa wanazirudisha zile bodi zilizovunjwa na kuweka watu wao,” anasema ofisa huyo ambaye  yuko karibu na Kipande kiutendaji.

,      Habari ndani ya TPA na nyaraka ambazo Habari24 imeziona zinaeleza kwamba Kipande ameunda bodi hizo zikisheheni watu kutoka TANROADS alikotokea.

         Bodi mpya ya Ununuzi ya Bandari ya Dar es Salaam inaongozwa na Alois Matei, ambaye ni Kaimu Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TPA (Miundombinu) kutoka Makao Makuu alitokea TANROAD S alikokuwa akifanya kazi na Kipande kabla ya TPA huku Bodi Kuu (CTB) ikiongozwa na Kaimu Mkurugenzi wa Rasilimali Watu ambaye kwa muundo uliopo anafanya kazi chini ya Matei.

     Kwa muundo huu Matei atawajibika kwa CTB ambayo iko chini ya “mfanyakazi” wake!
Mbali na hayo, Kipande pia kamteua  ofisa mwingine kwenye Bodi ya Ununuzi ya Bandari ya Dar es Salaam ambaye ni William Shila, Kaimu Mkurugenzi wa Uhandisi ambaye naye aliletwa TPA akitokea TANROADS .

    “Hivi hawa viongozi walioko makao makuu  wanaingia vipi Bodi ya Ununuzi ya Bandari ya Dar es Salaam kama sio kwa lengo la kufanya ufisadi?

        “Maajabu mengine ni kuwa mtumishi mmoja  kateuliwa kuajiriwa bila usaili wowote pamoja na ukweli ambao umedhihirika kuwa hana uzoefu katika fani ya ununuzi jambo ambalo sheria ya manunuzi inakataza.

        “Isitoshe mtumishi huyo pamoja na kutokuwa na sifa za kazi hiyo, ndiye kateuliwa na kuwa Katibu wa Bodi ya Ununuzi ya Bandari ya Dar es Salaam na kuwaacha wafanyakazi wazoefu na wenye uwezo wa kufanya kazi kwa weledi na kuzingatia sheria ya ununuzi,” anasema ofisa huyo akisema ni vyema serikali kuu ikafuatilia.

     TPA imeingia kwenye misuguano ya muda mrefu toka kuingia kwa uongozi mpya kiasi cha bodi ya mamlaka hiyo kutaka kumsimamisha Kipande kabla ya Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, kuivunja na kuunda mpya.

       Mmoja ya tuhuma ambazo bodi iliyovunjwa iliuhusisha uongozi wa Kipande ni pamoja na kuingiza kinyemela mradi wa tozo ya ufuatiliaji wa mizigo kwa mtandao (Eletronic Cargo Tracking Note, e-CTN)  bila kufuata sheria na kanuni.

          Tayari Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Majini na Nchi Kavu (Sumatra) ilishazuia mradi huo wa e-CTN usitishwe hadi taratibu zitakapofuatwa lakini habari sasa zinaeleza kwamba TPA iko kwenye mkakati wa kubadilisha baadhi ya vipengele kwenye sheria ya TPA ili iweze kutekeleza miradi yake bila udhibiti wowote.


       Huu si mwanzo wa urasimu pamoja na ufisadi ndani TPA,ufisadi huu umekuwa ukijotokeza kwenye Mamlaka hiyo kila mala ikumbukwe ufisadi huu ulimfanya Waziri wa uchukuzi Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe kuivunja bodi ya bandari na kuunda bodi mpya lakini bado ufisadi pamoja na urasimu umekuwa ukitokea katika mamlaka husika,

      Miezi michache iliyopita CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kiliibua tuhuma nzito za ufisadi wa mabilioni ya fedha, kikidai kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), hasa kupitia makundi ya wasaka urais, kimeanza kutumia mbinu haramu kutafuna fedha za Watanzania kwa ajili ya kampeni za 2015, kwa namna ile ile iliyotumika kufanikisha wizi wa EPA, wakati wa uchaguzi mkuu mwaka 2005.

       Katika mkutano na waandishi wa habari, CHADEMA kimedai kuwa ufisadi huounasimamiwa na Waziri wa Uchukuzi, Harrison Mwakyembe, kikimtuhumu kuwa anatumia madaraka yake ya uwaziri ‘kuipatia’ Kampuni ya CCM iitwayo Jitegemee Trading Company zabuni ya kujenga mradi yenye thamani ya bilioni 10, kinyume cha taratibu kujenga eneo la maegesho kwenye eneo la CCM.

       Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Oganaizesheni na Mafunzo wa CHADEMA, Singo Benson Kigaila, amesema kuwa kwa msukumo wa Mwakyembe, Mamlaka ya Bandari (TPA), imetoa zabuni kwa kampuni hiyo inayodaiwa ni ya CCM, kujenga maegesho ya magari makubwa, makontena na malori eneo la SUKITA (Tabata) jijini Dar es Salaam.

        Amesema kuwa kwa mujibu wa nyaraka ambazo chama hicho kimezinasa, Kampuni ya Jitegemee imepewa zabuni hiyo kinyume na shera za nchi, hususan ile ya Manunuzi ya Umma (PPRA), akisisitiza kuwa hakuna zabuni yoyote iliyotangazwa ili kuruhusu ushindani wa makampuni mbalimbali yenye sifa kufanya kazi hiyo.

        Vilevile Mkurugenzi huyo wa Oganazisheni na Mafunzo wa CHADEMA alisema kuwa tangu Mwakyembe aondoe uongozi wa zamani wa Mamlaka ya Bandari, yeye na viongozi wapya, wamepuuza miradi yote ya mwanzo na badala yake wameingiza miradi mipya takriban 35, ambayo imeombewa fedha kwa nia hiyo hiyo ya kusaka fedha za urais.

       Amewataka Watanzania kuzijua sura mbili za Waziri Mwakyembe, akidai kuwa si kiongozi wa kuaminika, akikumbushia namna alivyolinda maslahi ya CCM kwa kuwaficha Watanzania baadhi ya masuala katika kashfa ya Richmond na kukaa kimya pale maazimio ya bunge yaliyotokana na kamati yake, yalipopuuzwa.

        Mwakyembe ndiye alifanikisha kujiuzulu kwa aliyekua Waziri Mkuu, Edward Lowassa,baada ya kuuvalia njuga mradi wa kifisadi ulopewa kampuni ya Richmond Development LLC, kwa njia ambayo sasa anautoa kwa kampuni ya Jitegemee.

      Hatua hiyo ilimpa heshima kubwa Mwakyembe, jambo ambalo wadadisi wa mambo wamesema sasa ametumia heshima hiyo “kufanya atakavyo” hata kufikia hatua ya kuingia kwenye ufisadi

No comments: