Thursday, November 28, 2013

MZEE WA MIAKA 55 ABAKA MTOTO WA MIAKA 12 NA KUJITOSA BAHARINI KUKWEPA MKONO WA DOLA

Na Mohamded Mhina wa Jeshi la Polisi, Zanzibar 

          Mzee mmoja mwenye umri wa miaka 55, mkazi wa Kijiji cha Kidutani Gando mkoa wa Kaskazini Pemba ametiwa mbaroni kwa tuhuma za kumbaka mtoto mwenye umri wa miaka 12 na baadaye kujitosa bahari kukwepa mkono wa dola.
ENDELEA HAPO CHINI-----------

          Mzee huyo Muslih Mserembe, alikamatwa na wananchi waliokuwa wamekizingira kibanda chake kilichojengwa kwa miti, kuezekwa kwa makuti na kukandikwa kwa udongo wakati akimbaka binti huyo bila ya huruma. (Jina la binti huyo linahifadhiwa kwa usalama).

          Kamishna wa Polisi Zanzibar CP Mussa Ali Mussa(Pichani), amesema kuwa tukio hilo limetokea jana majira ya saa 12.00 alfajiri wakati binti huyo akiwafuatilia wenzake kwenda shambani kuokota maembe na ndipo mzee huyo alipomuona na kumuita

           Amesema baada ya binti huyo kumsogelea mzee huyo, alimwambia waingie ndani ya nyumba yake akidai kuwa angempatia maembe badala ya kuwafuata wenzake na ndipo alipombaka na binti kupiga kelele za kuomba msaada.

           Kamishna Mussa alisema baada ya kelele hizo wananchi walikwenda nyumbani kwa mzee huyo na wakati wakiizingira nyumba yake, mzee huyo alitoka na kutimua mbio na kwenda kujitosa baharini lakini wananchi nao walijitosa humo na kumvua kama samaki.

           Amesema baada ya kumkamata mtuhumiwa huyo, wananchi hao walimpeleka katika kambi moja ya KMKM na ndipo Polisi walipofika na kumchukua kwa hatua zaidi.

          Kamishna huyo wa Polisi Zanzibar amesema kuwa binti aliyebakwa alikimbizwa katika Hospitali ya Wete mkoa wa Kaskazini Pemba kwa matibabu zaidi na hali yake imeelezwa kuendelea vizuri.

         Kamishna Mussa ambaye amelaani vikali kitendo hicho, lakini amepongeza hatua za wananchi za kumkamata mtuhumiwa bila ya kumzuru na kumfikisha kwenye vyombo vya dola akiwa salama.

         Mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani kujibu shitaka lake.
 

No comments: