Thursday, December 5, 2013

IGP SAID MWEMA AWAAPISHA MAOFISA WALIOPANDISHWA VYEO NA NYADHIFA MPYA

mwemaTAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Said Mwema, amewavisha vyeo Maofisa wa Jeshi la Polisi watano na kuwaapisha makamishina wanane (8) kulingana na nyadhifa zao walizoteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa  Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete.
Miongoni mwa Maafisa waliovishwa vyeo kutoka cheo cha Naibu Kamishina Polisi kuwa Kamishina wa Polisi ni pamoja  na Hamdani Makame, Thobías Andengenye, Abdulrahmani Kaniki  na Ernest Mangu.

 Pia IGP Mwema,  amemvisha cheo cha Naibu Kamishina wa Polisi Diwani Athumani ambaye alikuwa ni  Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Polisi.
Kufuatia tukio hilo, IGP Mwema,  amewaapisha Makamishina wanane kulingana na nyadhifa zao mpya,  ambapo Kamishina wa Polisi (CP) Clodwig Mtweve ameapishwa kuwa Kamishina wa Fedha na Logistics, Kamishina wa Polisi (CP) Paulo Changonja ameapishwa kuwa Kamishina wa Operesheni na Mafunzo, Kamishina wa Polisi (CP) Mussa Ally Mussa ameapishwa kuwa Kamishina wa Polisi Jamii na Kamishina wa Polisi (CP) Hamdani Makame ameapishwa kuwa Kamishina wa Polisi Zanzíbar.
Wengine ni Kamishina wa Polisi (CP) Issaya Mngulu ameapishwa kuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Kamishina wa Polisi (CP) Thobías Andengenye ameapishwa kuwa Kamishina wa Utawala na Utumishi, Kamishina wa Polisi (CP) Abdulrahmani Kaniki ameapishwa kuwa Kamishina wa Uchunguzi wa Sayansi ya Makosa ya Jinai na Kamishina wa Polisi (CP) Ernest Mangu ameapishwa kuwa Kamishina wa Intelijensia ya Makosa ya Jinai.
Kufuatia kupandishwa vyeo  na kupata nyadhifa mpya kwa Maafisa hao, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Said Mwema, amemshukuru Rais wa Jamuhuru ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Mhe. Dkt Jakaya Mrisho Kikwete  kwa kutambua na kuthamini mchango wa Jeshi la Polisi katika kuimarisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao.
Aidha, IGP Mwema amewapongeza wale wote waliopandishwa vyeo na walioteuliwa katika nyadhifa mpya  na kusema kuwa, kupitia vyeo na nyadhifa hizo ni lazima Jamii ya watanzania iendelee kuwa salama, vitendo vya uhalifu visiwe kikwazo cha jamii kujiletea maendeleo na kuhakikisha kwamba usalama unashuka hadi ngazi ya familia.
Imetolewa na:
Advera Senso-SSP
Msemaji wa Jeshi la Polisi.

No comments: