Saturday, December 7, 2013

STARS YAFANYA MAAJABU HUKU KENYA,YAIDUNGUA UGANDA,IVO MAPUNDA SHUJAA,CHEKI HAPA

Wachezaji wa Stars wakimbeba Ivo baada ya kuokoa penaltri ya Dani Sserunkuma na chini cha Kim Poulsen akimpongeza Ivo
Na Mahmoud Zubeiry, Mombasa
KIPA Ivo Mapunda leo ameibuka shujaa baada ya kuokoa penalti mbili za Dani Sserunkuma na Khalid Aucho wa Uganda na kuipa Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars ushindi wa penalti 3-2 baada ya sare ya 2-2 ndani ya dakika 90 Uwanja wa Manispaa, Mombasa, Kenya.
Mbali nan a kuokoa penalti hizo mbili, Uganda walipoteza penalti nyingine moja baada ya Godfrey Walusimbi kupiga, wakati Hamisi Kiiza Emannuel Okwi ndiyo pekee walioifungia Cranes penalti.
Shujaa; Ngassa amefunga mabao mawili ya Stars leo na chini ni shujaa Ivo Mapunda baada ya kupangua penalti ya mwisho ya Sserunkuma

Waliofunga penalti za Bara ni Kevin Yondan, Athumani Iddi ‘Chuji’na Erasto Nyoni, wakati Mbwana Samatta na Amri Kiemba walikosa.
Katika mchezo huo uliochezeshwa na Wish Yabarow wa Somalia, aliyesaidiwa na KInde Mussa wa Ethiopia na Mohamed Idam wa Sudan, hadi mapumziko Stars ilikuwa inaongoza kwa mabao 2-1.
      Mshambuliaji wa Gor Mahia ya Kenya, Dani Sserunkuma alitangulia kuifungia Cranes bao dakika ya 16, baada ya kupokea krosi ya Hamisi Kiiza aliyemtoka Erasto Nyoni na kufumua shuti la chini lililompita kipa Ivo Mapunda.  
Dakika mbili baadaye, Mrisho Ngassa aliisawazishia Stars baada ya kuwazidi ujanja na maarifa ya kisoka mabeki wa Uganda, akimalizia mpira uliopigwa na Mbwana Ally Samatta.
        Mshambuliaji huyo wa TP Mazembe ya DRC, aliangushwa chini nje kidogo ya eneo la hatari na mshambuliaji wa Yanga, Mrisho Ngassa akaenda kupiga mpira wa adhabu uliotinga moja kwa moja kuipatia Stars bao la pili.
Baada ya bao hilo, Stars waliendelea kuishambulia Uganda kwa kujiamini zaidi, lakini mabeki wa Cranes walisimama imara kutoruhusu mabao zaidi.
Kipindi cha pili, Stars ilipata pigo dakika ya 53 baada ya kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’ kutolewa nje kwa nyekundu kwa kumchezea rafu Sserunkuma.
Uganda ikapata bao la kusawazisha dakika ya 73 kupitia kwa Martin Mpuga, aliyeunganisha kona ya Godfrey Walusimbi.
       Kwa matokeo hayo, Stars inarudia kuingia Nusu Faniali kama mwaka jana, wakati Uganda wanaacha taji Mombasa na kurejea nyumbani, Kampala.     
Tanzania Bara; Ivo Mapunda, Michael Aidan, Erasto Nyoni, Said Morad, Kevin Yondan, Frank Domayo, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Mrisho Ngassa/Athumani Iddi 80, Amri Kiemba, Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu.
Uganda; Benjamin Ochan, Nico Wadada, Muga Martin, Geoffrey Kizito/Said Kyeyune dk64, Godfrey Walusimbi, Kasaga Richard, Khalis Aucho, Mpande Joesph/Brian Majwega dk46, Daniel Sserunkuma, Hamisi Kiiza na Emmanuel Okwi.

No comments: