Monday, December 23, 2013

WABUNGE WAANZISHA MKAKATI MPYA WA KUMNG'OA WAZIRI MKUU MIZENGO KAYANDA PINDA KISA UTENDAJI MBOVU WA KIONGOZI HUYO KATIKA SERIKALI YA RAIS JK.

BAADHI ya wabunge wameanzisha mkakati wa kumwondoa madarakani, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda katika kile wanachodai kuwa hawaridhishwi na utendaji wake serikalini.
Hiyo ni dalili kwamba kung’oka kwa mawaziri wanne kutokana na matokeo ya ripoti ya utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili hakujamnusuru Pinda, kwani baadhi ya wabunge wanaendelea na msimamo kwamba naye ajiuzulu kwa kushindwa kuwasimamia wenzake.

Mawaziri waliong’oka baada ya Rais Jakaya Kikwete kutengua uteuzi wao kutokana na ripoti iliyowasilishwa na Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira ni Mawaziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha, wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi, Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Mathayo David Mathayo na Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki.

Hatua hiyo ya Rais Kikwete inatafsiriwa na wengi kama njia ya kuwapoza wabunge na kumwokoa Pinda ambaye ikiwa atang’oka itamaanisha kuundwa upya kwa Baraza la Mawaziri.
Habari ambazo zimelifikia gazeti hili jana zinasema wabunge 26 wametia saini fomu maalumu ya kutaka Bunge litumie mamlaka yake ya kikatiba kumng’oa Pinda kwa kumpigia kura ya kutokuwa na imani naye.
 
Kwa mujibu wa Ibara ya 53 A(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977, Bunge linaweza kupitisha azimio la kura ya kutokuwa na imani na waziri mkuu, endapo itatolewa hoja kupendekeza hivyo.

Kwa mujibu wa Ibara hiyo, hoja ya kumpigia kura ya kutokuwa na imani na waziri mkuu inapaswa kuungwa mkono na wabunge wasiopungua asilimia 20 ya wabunge wote.

Mbunge wa Kasulu Mjini (NCCR-Mageuzi), Moses Machali alisema hili jana kuwa ukusanyaji saini za wabunge aliouanzisha Ijumaa jioni unakwenda vizuri.

“Kung’oka kwa mawaziri wale wanne inatosha kuthibitisha kuwa Pinda amepoteza uhalali wa kuwa Waziri Mkuu kutokana na kushindwa kuwasimamia walio chini yake,” alisema Machali.

“Rais tunaweza kumuacha, lakini Pinda ndiye mtendaji mkuu wa shughuli za Serikali. Kama wapo mawaziri wameboronga ni wazi na yeye anaingia moja kwa moja katika hilo kapu,” alisema na kuongeza:

“Kama kweli tunataka taifa lisonge mbele kutoka hapa tulipo ni lazima tumuondoe Pinda…….. amekuwa mpole mno, mzito kufanya uamuzi na analea matatizo.”

Hata hivyo, alisema wabunge waliosaini fomu hiyo, wote wanatoka kambi ya upinzani na kusema wabunge wengi wa CCM aliowafuata kuwaomba watie saini wanaogopa au wanasita kufanya hivyo. MWANANCHI

No comments: