Friday, March 21, 2014

TAARIFA JUU YA UTEKELEZAJI WA MPANGO KABAMBE WA MIAKA KUMI (2014 - 2023) WA SHIRIKA LA POSTA TANZANIA


Waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali kutoka vyombo mbalimbali wakiwasikiliza viongozi wa shirika la posta tanzania wakati wakiwasilisha report ya mpango kabambe wa miaka kumi leo jijini dar es salaam.PICHA NA KAJUNASON BLOG

(1)               Wakati Tanzania inaelekea kuadhimisha miaka 50 ya Muungano, Shirika la Posta Tanzania limeanza utekelezaji wa Mpango Kabambe wa miaka kumi  (2014 hadi 2023) ikiwa ni dira na mwelekeo wa kuliongoza Shirika hili liweze kujiendesha kibiashara, kubuni na kutoa huduma  mbadala, kutumia teknolojia maridhawa na kukidhi mahitaji ya soko la huduma za mawasiliano jumuishi. 


(2)               Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika hili ambayo ni  chombo cha juu cha utoaji maamuzi ndani ya Shirika imeidhinisha utekelezaji wa mpango huu ambao umebuniwa kwa kuzingatia matukio muhimu ya kihistoria pamoja na maendeleo ya sasa na mwelekeo wa hapo baadae wa kibiashara, kiuchumi,   kijamii  na kiteknolojia hapa nchini na duniani kote.

(3)               Tangu miaka ya kabla na baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Shirika la Posta ambalo ni Taasisi mojawapo  iliyoko chini ya muungano huu, limejikita katika kutekeleza wajibu wake wa kuhakikisha kuwa huduma za mawasiliano  jumuishi hasa yale ya msingi zinawafikia watu wote wa mijini na vijijini (universal service obligation)  katika  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

(4)               Mantiki hii ya kuweka umuhimu wa kusambaza mtandao wa ofisi na vituo vya Posta ili kuwafikia watu wengi zaidi unazingatia hali halisi ya kihistoria kuwa huduma hizi ndizo zenye gharama nafuu zinazowezesha wananchi wengi kupata haki ya msingi ya kuwasiliana na kufanya miamala ya kijamii, kibiashara na kiuchumi kupitia ofisi za Posta.
(5)               
                  Ili kuhakikisha kuwa Shirika la Posta linaendelea kutekeleza wajibu huu wa kihistoria na pia linashiriki kikamilifu  katika utekelezaji wa sera na mipango ya sasa na ya baadae katika mazingira mapya na kushiriki ipasavyo kwenye kuharakisha  maendeleo ya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025, Shirika pamoja na kujiwekea mipango ya muda mrefu (Mpango Kabambe – Master Plan 2014/2023) pia limejiwekea mipango ya muda wa kati ambao ni Mpango Mkakati wa miaka mitano (Strategic Plan 2014 – 2018) ambao utekelezaji wake umeanza na Mpango wa mwaka huu wa 2014. 

(6)               Mipango hii ya muda mrefu, muda wa kati na muda mfupi ni  mwendelezo wa mkakati mpya utakaoleta mabadiliko katika uendeshaji na utoaji wa huduma za Posta nchini ili kukabiliana na changamoto zinazoletwa na utandawazi, mapinduzi ya teknolojia na mabadiliko ya mionjo ya wateja. 

(7)               Katika kuhakikisha kuwa Shirika linashiriki na kuchangia kikamilifu matumizi ya TEHAMA, msukumo umewekwa kwa lengo la kupiga hatua katika utekelezaji na uwekaji wa mfumo wa kisasa wa  mawasiliano (Automation Programmes) kwa awamu kwa kuanzia na ofisi za Posta zipatazo 86 hapa nchini ili kutoa huduma kwa ufanisi zaidi, kuongeza idadi ya wateja wanaohudumiwa, kuondoa uchelewesho na kupunguza malalamiko kwa wateja.

(8)               Aidha, Shirika limeunganishwa katika mfumo wa elektroni wa kimataifa (International Postal Systems) ambao unawezesha ufuatiliaji (Track and Trace) wa nyaraka na vipeto vinavyopitia EMS, Rejista, Vifurushi vya kimataifa vinavyopitia katika mtandao wa ofisi za Posta.  Lengo la Shirika ni kuwawezesha wananchi na wajasiriamali wa kawaida kunufaika na maendeleo ya teknolojia na ubunifu uliopo hapa nchini na duniani, hivyo kufanya amali za kijamii, kibiashara na kiuchumi kwa uhakika zaidi.

(9)               Katika mwelekeo huu wa matumizi ya TEHAMA, Shirika litaendelea kupanua mifumo na  kujiimarisha  zaidi katika matumizi ya Teknolojia hiyo hadi kufikia ofisi za wilaya na miji midogo, kwa lengo la kurahisisha ufikishaji wa huduma, sampuli  na bidhaa za wateja mpaka majumbani/maofisini kwao. 


(10)           Vile vile mtandao wa ofisi za Posta utaweza kufikisha bidhaa zitakazonunuliwa na wateja kupitia mtandao wa Internet (e-commerce) na kuwajengea uwezo wananchi wa kawaida katika matumizi ya  mtandao  wa mawasiliano ya kisasa kupitia Vituo vya Mawasiliano kwa Jamii (CIC) ambavyo viko kwenye baadhi ya ofisi za Posta.      

(11)           Lengo ni kuongeza vituo vya mawasiliano kwa Jamii (CIC) ili kuwawezesha wananchi wengi zaidi wanufaike na huduma za kisasa ikiwa ni pamoja na elimu mtandao (E-Education au distance learning), biashara mtandao (E-commerce), Serikali mtando (E-Government), matibabu mtandao (E-medicine) na huduma nyingine za kiuchumi na kijamii kupitia ofisi na vituo vya Posta.

(12)           Aidha chini ya mipango hiyo, utekelezaji wa mfumo mpya wa Anuani za Makazi na Postikodi    (Physical Address and Postcode System)   umeanza na umelenga kila mwananchi kuwa na anuani kamili inayotambulisha makazi yake.  Mfumo mpya wa anuani unaweka msukumo na shinikizo katika kutoa huduma mtambuka (cross-cutting services) zinazofikia viwango vya kimataifa.

(13)           Shirika la Posta Tanzania kwa upande wake linaendelea kujizatiti ili  kuhakikisha kuwa mfumo huu wa Anuani za Makazi na Postikodi unaanza kazi mwaka huu hususan kwenye maeneo machache ambayo majina ya mitaa yamewekwa na namba za nyumba zimebandikwa. 

(14)           Postikodi ni mfumo wa anuani unaotumia utambulisho maalum katika kumfikishia mteja  huduma za kijamii, kiuchumi na kibiashara pamoja na barua, nyaraka, vifurushi na vipeto kwenye makazi/ofisini.  Anuani kamili lazima iwe na majina kamili ya mtumiwa, majina ya mtaa, nambari ya nyumba na postikodi.

(15)           Wote tunafahamu kuwa mfumo wa anuani unaotumika hivi sasa  hapa nchini kwetu ni wa masanduku ya kupokelea barua yaliyoko kwenye ofisi za Posta.  Mfumo huu humlazimisha mteja kufuata barua, vifurushi na vipeto katika ofisi za Posta kupitia sanduku

alilokodisha.  Kwa hivi sasa huduma za EMS na pCUM pekee  ndizo zenye fursa kwa mteja kupelekewa barua, nyaraka, vipeto na vifurushi kwenye makazi au ofisini. 

(16)           Chini ya mfumo huu  wa Postikodi, uchambuzi wa barua utafanyika kwa ufanisi na haraka zaidi, utarahisisha utambuaji wa anwani kwa digitali, utaongeza ufanisi katika usafirishaji na usambazaji wa barua, nyaraka, vifurushi, vipeto, na mizigo.  Aidha mfumo mpya utaongeza ufanisi katika kuhudumia wateja na kupunguza na kuondoa uwezekano wa kuwepo makosa katika uchambuzi, usambazaji na ufikishaji  wa mali za wateja pamoja na huduma nyinginezo za kijamii, kibiashara na kiuchumi.

(17)           Katika ngazi ya kimataifa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni mwanachama wa Umoja wa Posta Duninai (Universal Postal Union) ambapo Tanzania ilijiunga mwaka 1963 na kwa hivi sasa ni moja ya taasisi za Umoja wa Mataifa.  Malengo ya umoja huo ni pamoja na kuisimamia (regulate) sekta ya Posta pamoja na kutoa ushauri, usuluhishi, kuunganisha ushirikiano baina ya nchi wanachama na kutoa/kujengea uwezo wa kiufundi nchi wanachama.

(18)           Kupitia umoja huo suala la ubora na  usalama  katika usambazaji wa barua, nyaraka, vipeto, vifurushi na miamala ya kimataifa kupitia Posta unazingatiwa, ambapo viwango vya ubora na usalama vimewekwa kwa kila nchi mwanachama kuzizingatia.  Pia Shirika linapata nafasi kubadilishana uzoefu katika shughuli mbalimbali za posta baina ya nchi wanachama na kujifunza kutoka nchi zilizoendelea juu ya uendeshaji na maboresho ya huduma za mawasiliano jumuishi kupitia mtandao wa ofisi za Posta.

(19)           Ubora, ukubwa na ufanisi  (qualitative and quantitative) wa mtandao wa mawasiliano ya posta ni kigezo muhimu cha kiwango cha maendeleo ya jamii kitaifa na kimataifa.  Kwa mfano kwa kuzingatia takwimu za sasa za Umoja wa Posta Duniani (UPU), idadi ya ofisi za posta duniani inafikia 660,000 ambapo idadi ya ofisi hizi katika Bara la Afrika ni takriban 16,000 ambazo ni karibu ya asilimia 2.3 ya ofisi zote za  Posta duniani huku idadi ya watu duniani asilimia 13 wanaishi kwenye Bara la Afrika.

(20)           Aidha takwimu za Shirika la Umoja wa Posta duniani zinaonyesha kuwa wastani wa idadi ya barua kwa kila mtu mmoja (letter per capital) ni   wastani wa barua 66 kwa dunia nzima kwa mtu mmoja, kwa nchi zilizoendelea (nchi za viwanda) mtu mmoja ni wastani wa barua 403, nchi za Bara la Asia ni barua 12, bara la Afrika hususan kusini mwa Jangwa la Sahara ni wastani wa barua 3 kwa mtu, na hapa kwetu Tanzania wastani wa barua zinazopitia Posta ni chini ya barua moja kwa mtu.

(21)           Takwimu hizi zinaonyesha uwepo wa changamoto katika nchi yetu na Bara la Afrika kwa ujumla.

(22)                     Licha ya kwamba shughuli za posta ni mtambuka na zinajumuisha majukumu mengine ya kijamii, kiuchumi na kibiashara ndani ya mwavuli wa uwakala (Agency Services) ambazo ni pamoja na miamala ya kutuma, kupokea na kulipa fedha, msingi na historia ya Posta imejikita katika shughuli za kupokea, kuhudumia, kusafirisha na kufikisha barua, nyaraka, vifurushi na vipeto.    

(23)           Sisi Shirika la Posta tunayo dhamira chini ya mipango yetu ya muda mrefu, muda wa kati na muda mfupi ya  kubadilisha hali hii, ili ifikapo mwaka 2025, Tanzania iwe katika kiwango cha ubora kinacholingana na nchi za uchumi wa kati kwenye tasnia  ya shughuli za Posta.

(24)           Ni dhahiri kuwa, ili Shirika hili liweze kutekeleza kwa ufanisi mipango yake na kufikia malengo yanayotarajiwa, ushirikiano na michango ya wadau wote inahitajika.



(25)           Shirika la Posta Tanzania linayo nia na sababu za maboresho na mageuzi yatakayoleta ufanisi na tija katika majukumu yake, na limejipanga vizuri kwa lengo la kufikia dhamira yake.   Penye nia kuna njia.
 

Imetolewa na:
OFISI YA POSTAMASTA MKUU 
SHIRIKA LA POSTA TANZANIA
MTAA WA OHIO/GHANA
S.L.P. 9551,
POSTIKODI: 11300
DAR ES SALAAM
21 MACHI, 2014

No comments: