Thursday, May 15, 2014

MAONI YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI, WIZARA YA KATIBA NA SHERIA, MHESHIMIWA TUNDU A.M. LISSU (MB.) KUHUSU MPANGO NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA YA WIZARA YA KATIBA NA SHERIA KWA MWAKA 2014/2015


UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika,
Ofisi ya Waziri wa Katiba na Sheria imeanzishwa kwa mujibu wa kipengele cha 12 cha Nyongeza ya Waraka wa Rais uliochapishwa kama  
        Tangazo la Serikali Na. 494 la tarehe 17 Desemba 2010.
Majukumu ya Ofisi hii yameainishwa katika Tangazo la Ukasimishaji wa Majukumu ya Kiuwaziri la mwaka 2010 (The Ministers [Assignment of Ministerial Functions] Notice, 2010) lililochapishwa katika Gazeti la Serikali kama Tangazo la Serikali Na. 494A la tarehe 17 Desemba 2010. Kwa mujibu wa Nyongeza ya Pili ya Tangazo hilo, pamoja na mengine, Ofisi ya Waziri wa Katiba na Sheria imekasimiwa majukumu ya masuala ya kikatiba, uendeshaji na utoaji wa haki, uendeshaji mashtaka na  haki za binadamu.
Mheshimiwa Spika,
Majukumu haya ni mazito katika hali ya kawaida, kwani mfumo wa kikatiba, haki za binadamu na utoaji haki katika nchi yenye kufuata mfumo wa kidemokrasia ndiyo roho ya mfumo mzima wa utawala. Mfumo wa kikatiba na wa utoaji haki ndio unaotofautisha dola iliyoparaganyika (a failed state) na dola inayoongozwa kikatiba (a constitutional state) na utawala wa sheria (rule of law). Majukumu haya ni mazito zaidi katika nchi ambayo, kama ilivyo nchi yetu, inatengeneza Katiba Mpya. Hapa, vile vile, mfumo unaotumika kutengeneza Katiba Mpya ndiyo utakaotofautisha nchi hiyo kuwa a failed state, au kuwa nchi yenye mfumo imara wa kikatiba na wa kisiasa. Kwa sababu hiyo, kwa vyovyote vile, majukumu ya Wizara ya Katiba na Sheria ni mazito na yenye umuhimu mkubwa.
BUNGE MAALUM NA HARUFU YA UFISADI
Mheshimiwa Spika,
Vyombo vya habari mbali mbali hapa nchini vimemnukuu Waziri wa Fedha Mh. Saada Salum Mkuya akisema kwamba, hadi kuahirishwa kwake, Bunge Maalum limetumia zaidi ya Shilingi bilioni 27. Kama kauli ya Waziri wa Fedha ni sahihi, kiasi hiki cha fedha kitakuwa kikubwa kuliko fedha za matumizi ya kawaida ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, Divisheni ya Uendeshaji Mashtaka na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kwa ujumla wao kwa mwaka unaoisha wa fedha. Hiki sio kiasi kidogo cha fedha katika nchi kama yetu ambayo shughuli mbali mbali za huduma za jamii zimekwama kwa kukosa fedha.
Mheshimiwa Spika,
Mwaka jana wakati Bunge lako tukufu linajadili makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka wa fedha 2013/2014, Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala iliagiza kwamba bajeti ya Bunge Maalum “… iletwe Bungeni kwa ajili ya kujadiliwa na kupitishwa.” Kamati ilitoa agizo hilo kwa sababu wakati Wizara ilikuwa imewasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, yaani Fungu 08, hakukuwa na Fungu lolote linalohusu Bunge Maalum. Hii ni licha ya ukweli kwamba hadi kufikia mwaka jana, tayari ilikuwa inajulikana kwamba kutakuwa na Bunge Maalum, kwa sababu vifungu husika vya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba vilikwishapitishwa na Bunge lako tukufu.
Mheshimiwa Spika,
Agizo la Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala lilipuuzwa mwaka jana kwani Serikali hii sikivu ya CCM haikuleta makadirio ya mapato na matumizi ya Bunge Maalum kwa ajili ya kujadiliwa na kuidhinishwa na Bunge lako tukufu. Na hata mwaka huu agizo hilo limepuuzwa kwani hakuna makadirio ya mapato na matumizi ya Bunge Maalum ambayo yameletwa kwa ajili ya kujadiliwa na kuidhinishwa na Bunge lako tukufu.
Ili kuhalalisha vitendo vyake vya kupuuza agizo la Bunge lako tukufu, Waziri wa Katiba na Sheria, Mheshimiwa Dkt. Asha-Rose Mtengeti Migiro, alidai mbele ya Kamati kwamba “… masuala yote ya Bunge la Katiba yapo chini ya Bunge Maalum la Katiba ambapo fedha kwa ajili ya Bunge hili zinatolewa na Mfuko Mkuu wa Hazina.” Kwa jibu hili, Waziri alitaka kuiaminisha Kamati kwamba hakukuwa na haja ya fedha za Bunge Maalum kujadiliwa na kuidhinishwa na Bunge lako tukufu kwa sababu tu fedha hizo zilikuwa zinatoka kwenye Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali.
Hata hivyo, Mheshimiwa Spika, baada ya kuonyeshwa kwamba fedha zinazolipwa kutoka kwenye Mfuko Mkuu wa Hazina hazina budi kuidhinishwa na sheria iliyotungwa Bunge na matumizi yake kuidhinishwa na Sheria ya Matumizi ya Serikali, sasa Waziri amebadili kauli na kudai kwamba fedha za matumizi ya Bunge Maalum ziliidhinishwa na Bunge lako tukufu!
Katika Majibu yake ya Hoja za Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala Wakati wa Kupitia Makadirio ya Wizara kwa mwaka wa Fedha 2014/2015, Mheshimiwa Waziri amesema yafuatayo: “Bajeti ya Bunge Maalum ya shilingi bilioni 24.4 ilipitishwa na Bunge katika mwaka wa fedha 2013/2014 kupitia Fungu 21 – Hazina kwenye kifungu cha ‘Special Expenditure.’ Serikali ilifanya hivyo kwa kutambua kwamba Bunge Maalum lingeanza kazi zake katika mwaka huo wa fedha. Wakati huo mahitaji halisi ya uendeshaji wa Bunge hilo yalikuwa hayafahamiki.”
Waziri ameongeza kusema kwamba “kwa kutumia uzoefu uliopatikana katika uendeshaji wa Bunge hilo, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 20.0 kwenye Fungu 21 – Hazina kwenye kifungu cha ‘Special Expenditure’ katika mwaka wa fedha 2014/2015 ili kukamilisha kazi zilizosalia.”
Mheshimiwa Spika,
Kauli za Waziri wa Katiba na Sheria juu ya masuala yote yanayohusu bajeti ya Bunge Maalum hazina ukweli wowote. Kwanza, kuhusu kiasi cha fedha kilichokwishatumika kwa ajili ya Bunge Maalum. Kauli ya Waziri kwamba kiasi hicho ni shilingi bilioni 24.4 inapingana moja kwa moja na kauli iliyotolewa na Waziri wa Fedha ndani ya Bunge Maalum.
Kwa mujibu wa Taarifa Rasmi (Hansard) ya Majadiliano ya Bunge Maalum ya Kikao cha Ishirini na Tisa cha tarehe 24 Aprili, 2014, Mheshimiwa Saada Mkuya Salum, alisema yafuatayo kuhusu matumizi ya Bunge Maalum: “Mheshimiwa Mwenyekiti, inasikitisha kwamba hatutumii fursa hii, nasikitika tumechukua fedha, yaani kodi ya wananchi ambayo kila siku wanalia na wameweza ku-sacrifice tunakwenda kwenye twenty seven billions kwa ajili ya session hii, tumeweza ku-sacrifice kupeleka umeme kwa wananchi, hususan vijijini.”

         Mheshimiwa Spika,
Kiasi kilichotajwa na Waziri wa Fedha kinalingana na kiasi kilichotajwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Utaribu na Bunge, Mheshimiwa William Lukuvi, aliyeiambia Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala kwamba hadi linaahirishwa tarehe 25 Aprili mwaka huu, Bunge Maalum lilikwishatumia takriban shilingi bilioni 27.
Mheshimiwa Spika,

          Bunge lako tukufu linahitaji majibu ya kuridhisha kuhusu mkanganyiko huu katika kauli za Waziri wa Katiba na Sheria na Mawaziri wenzake wa Fedha na Sera, Uratibu na Bunge. Kwa sababu hiyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali hii ya CCM ilieleze Bunge lako tukufu ni kauli ya Waziri yupi kati ya hawa watatu ndiyo iaminiwe na kuchukuliwa kuwa ndiyo kauli sahihi na Bunge lako tukufu.

       Aidha, kama itajulikana kwamba mmojawapo kati ya mawaziri hawa watatu ametoa taarifa za uongo kwa Kamati ya Bunge lako tukufu, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka mamlaka ya uteuzi wao, yaani Rais wa Jamhuri ya Muungano, awawajibishe kwa kuwafukuza kazi. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaamini kwamba Waziri anayedanganya Bunge lako tukufu au Kamati zake sio tu analidharau Bunge, bali pia anaidharau mamlaka ya uteuzi wake, yaani Rais. Vinginevyo Bunge lako tukufu liambiwe kwamba Waziri huyo ametumwa na Rais kuja kudanganya Bunge.
Mheshimiwa Spika,

        Uongo wa pili wa kauli ya Waziri wa Katiba na Sheria unahusu madai yake kwamba bajeti ya Bunge Maalum iko kwenye Fungu 21 – Hazina. Uthibitisho wa uongo huu uko kwenye Kitabu cha II cha Makadirio ya Matumizi ya Umma ya Huduma za Mfuko Mkuu kwa mwaka wa fedha 2013/2014 kilichowasilishwa Bungeni mwaka jana; na Kitabu hicho hicho kilichowasilishwa Bungeni mwezi huu kwa ajili ya mwaka wa fedha 2014/2015. Katika Vitabu vyote viwili hakuna kifungu chochote kinachoitwa ‘Special Expenditure’ au kasma yoyote inayohusu Bunge Maalum.

      Aidha, hakuna kifungu chochote chenye makadirio ya matumizi ya shilingi bilioni 24.4 kwa ajili ya Bunge Maalum au kwa ajili nyingine yoyote katika Kitabu cha mwaka 2013/2014; na wala hakuna makadirio ya matumizi ya shilingi bilioni 20.0 kwa ajili ya matumizi ya Bunge Maalum katika Kitabu cha mwaka 2014/2015. Na hata kwenye Vitabu vya Makadirio ya Matumizi ya Maendeleo kwa mwaka wa fedha 2013/2014 na mwaka wa fedha 2014/2015, hakuna kifungu chochote kinachoitwa ‘Special Expenditure’ au chenye kiasi cha fedha kilichotajwa na Waziri wa Katiba na Sheria.

       Mheshimiwa Spika,
Kama hakuna vifungu vyovyote vya ‘Special Expenditure’ kwa ajili ya Bunge Maalum, na kama hakuna kiasi chochote kilichoonyeshwa kwenye Vitabu vya bajeti, maana yake ni kwamba Bunge lako tukufu halijaidhinisha bajeti yoyote kwa ajili ya Bunge Maalum. Kwa kifupi, Waziri wa Katiba na Sheria amelidanganya Bunge lako tukufu, na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni itaona ajabu sana endapo Bunge lako tukufu litaamua, licha ya ushahidi wote huu, kufunika kombe ili wanaharamu wapite!
Mheshimiwa Spika,

         Katika Maoni yake juu ya hotuba ya Waziri Mkuu Kuhusu Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa Mwaka 2014/2015, Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Mheshimiwa Freeman A. Mbowe aliliambia Bunge lako tukufu kwamba: Fedha zote zilizotumika kwa ajili ya gharama mbali mbali za Bunge Maalum hazikuidhinishwa na Bunge lako tukufu. Ukweli ni kwamba hadi sasa Bunge lako tukufu halijui bajeti yote ya Bunge Maalum, halijui fedha kiasi gani zimetumika kwa ajili ya matengenezo mbali mbali ya miundombinu ya Bunge hili, au kwa ajili ya posho, mishahara na stahili mbali mbali za wajumbe na watumishi wa Bunge Maalum hadi lilipoahirishwa tarehe 25 Aprili, 2014. Aidha, Bunge lako tukufu halina ufahamu wowote juu ya gharama za Bunge Maalum pale litakaporudi tarehe 5 Agosti, 2014, kuendelea kujadili Rasimu ya Katiba Mpya.”
Katika hali hiyo, Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni alitaka maswali yafuatayo yapatiwe majibu:
(i)                          Je, bajeti ya matumizi ya Bunge Maalum ni kiasi gani na kwa ajili ya matumizi gani?
(ii)                       Je, ni kiasi gani cha fedha hizo kimeshatumika hadi sasa na kwa ajili ya matumizi gani?
(iii)                    Je, ni nani aliyejadili na kupitisha bajeti hiyo?
(iv)                     Je, ni Sheria gani iliyotungwa na Bunge lipi iliyoidhinisha matumizi haya ya fedha za umma?
(v)                        Je, ni lini na kwa waraka gani Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali aliidhinisha matumizi haya?
Mheshimiwa Spika,
Maswali haya hayajapatiwa majibu yoyote. Badala yake, Waziri wa Katiba na Sheria amelipa Bunge lako tukufu sababu za kuuliza maswali mengine yafuatayo:
(a)             Je, ni ukurasa upi kati ya kurasa za 55-60 zenye makadirio ya Fungu 21 – Hazina kwenye Kitabu cha II ambapo kuna kifungu cha ‘Special Expenditure’ chenye makadirio ya matumizi ya shilingi bilioni 24.4 kwa ajili ya Bunge Maalum kwa mwaka wa fedha 2013/2014?
(b)            Je, ni ukurasa upi kati ya kurasa za 68-73 zenye makadirio ya Fungu 21 – Hazina kwenye Kitabu cha II ambapo kuna kifungu cha ‘Special Expenditure chenye makadirio ya matumizi ya shilingi bilioni 20.0 kwa ajili ya Bunge Maalum kwa mwaka wa fedha 2014/2015?
(c)             Je, kati ya kauli yake kwamba hadi linaahirishwa Bunge Maalum limekwishatumia shilingi bilioni 24.4, na kauli ya Waziri wa Fedha kwamba Bunge hilo limekwishatumia shilingi bilioni 27, ipi ndiyo kauli ya kweli?
(d)            Na mwisho, kama itajulikana kwamba kauli yake kuhusu masuala yanayohusu bajeti ya Bunge Maalum ni ya uongo yuko tayari kulinda heshima yake iliyobaki kwa kujiuzulu au atasubiri mamlaka yake ya uteuzi imwajibishe kwa kumfukuza kazi kwa kulidanganya Bunge?
MAHAKAMA YA TANZANIA
Mheshimiwa Spika,
Ibara ya 4(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa tanzania, 1977, inaelekeza kwamba vyombo vyenye mamlaka ya kutekeleza utoaji haki ni Mahakama ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Mahakama ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Ibara ya 107A(1) inaweka wazi kwamba “mamlaka ya mwisho ya utoaji haki katika Jamhuri ya Muungano itakuwa ni Mahakama.” Maoni haya yanahusu Mahakama ya Tanganyika kwa sababu, mbali na Mahakama ya Rufani ya Tanzania, masuala ya mahakama sio mambo ya Muungano.
Katika mwaka wa fedha 2013/2014, Mahakama iliidhinishiwa shilingi bilioni 117.580 kwa ajili ya matumizi ya kawaida. Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 86.600 zilikuwa kwa ajili ya matumizi mengineyo na shilingi bilioni 30.980 kwa ajili ya mishahara. Aidha, Mahakama iliidhinishiwa shilingi bilioni 42.716 kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Kwa mujibu wa Maelezo ya Makadirio ya Mapato, Matumizi ya Kawaida na Mpango wa Maendeleo kwa Mwaka 2014/2015, hadi Machi 2014, Mahakama ilikuwa imepokea shilingi bilioni 72.106, sawa na asilimia 61 (sio 56 zilizotajwa katika Maelezo!) ya fedha zilizoidhinishwa na Bunge lako tukufu. Kati ya hizo, shilingi bilioni 36.253 au asilimia 42 zilikuwa kwa ajili ya matumizi mengineyo, na shilingi bilioni 26.652 au asilimia 86 zilikuwa kwa ajili ya mishahara.
Mheshimiwa Spika,
Kwa upande wa fedha za maendeleo, hadi kufikia Machi 2014, Mahakama ilikuwa imepokea shilingi bilioni 5.508 au asilimia 13 ya fedha zilizoidhinishwa na Bunge lako tukufu. Mahakama imeeleza katika Maelezo yaliyoletwa mbele ya Kamati kwamba kutopokea fedha zilizoidhinishwa “kumeisababishia Mahakama kuendesha shughuli zake kwa ugumu mkubwa.” Aidha, “mwenendo … wa upatikanaji wa fedha za maendeleo umekuwa si wa kuridhisha na hivyo kuashiria kukwama kwa utekelezaji wa miradi ya Mahakama ambayo mchakato wake umefikia ukingoni.”
NDIMI MBILI ZA MAHAKAMA
Mheshimiwa Spika,
Lugha iliyotumika katika Maelezo ya Mahakama kuelezea matatizo ya kutopatiwa fedha zinazoidhinishwa na Bunge lako tukufu ni ya kidiplomasia ambayo pengine ndiyo lugha sahihi kwa mamlaka ya utoaji haki katika nchi. Hata hivyo, lugha hiyo haitoi picha kamili na halisi ya ukubwa wa matatizo hayo, na inaweza kuwa inapotosha ukweli wa hali halisi. Kwa mfano, Maelezo ya Mahakama yanadai kwamba “… Mahakama ya Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuondoa mlundikano wa mashauri (backlog clearance) na kuonyesha ongezeko kubwa la wastani wa uondoaji wa mashauri katika ngazi zote za Mahakama.…”
Hata hivyo, Taarifa ya Waziri inatoa picha kinyume kabisa. Hivyo basi, kwa mujibu wa Taarifa ya Waziri, upungufu huu wa bajeti umesababisha “… kukwama kwa shughuli za uendeshaji na usikilizaji wa mashauri na kusababisha kuongezeka kwa msongamano wa mahabusu na wafungwa magerezani.” Vivyo hivyo tunaambiwa, kama tulivyoambiwa miaka miwili iliyopita, kwamba “suala la usafiri kwa ajili ya shughuli za Mahakama limepewa uzito unaostahili.” Ili kuthibitisha uzito huo ‘unaostahili’, Mahakama inatuambia kwamba “... mwaka 2013/2014 Mahakama ilipanga kununua ... magari 218 na pikipiki 200 kwa ajili ya kuimarisha ukaguzi na usimamizi wa shughuli za Mahakama.”
Hata hivyo, kwa mujibu wa Maelezo hayo hayo ya Mahakama, “hadi sasa tiyari Mahakama imenunua magari ... 7 na imeingia mkataba wa ununuzi wa magari mengine 211 na pikipiki 200 ambayo yanatarajiwa kupatikana mwishoni mwa mwezi Juni, 2014.” Kwa maneno mengine magari saba au asilimia 3 ya matarajio ndiyo yaliyokwishanunuliwa na bado Mahakama inaona huu ni ‘uzito unaostahili’!
Kwa upande mmoja, Mahakama inatuambia kwamba umalizaji wa mashauri katika Mahakama ya Ardhi ulikuwa asilimia 99, lakini kwa upande mwingine Wizara inatuambia “imeshindwa kufuatilia migogoro ya ardhi.” Ulimi mmoja wa Wizara unaliambia Bunge lako tukufu juu ya “kuimarika kwa usimamizi na ukaguzi wa kazi za Mahakama kwa kuongeza vitendea kazi na rasilimali watu.” Ulimi mwingine wa Wizara hiyo hiyo unakiri mbele ya Bunge lako tukufu juu ya “kupungua kwa imani ya wananchi kwa Serikali kutokana na kukosekana kwa huduma au huduma hafifu”!
Mdomo mmoja wa Wizara unasema kwamba ukaguzi wa Mahakama uliofanywa na viongozi wa Mahakama ya Tanzania “… umesaidia kusikiliza maoni na malalamiko mbalimbali ambayo yamesaidia kuboresha utendaji kazi katika Mahakama husika.” Mdomo mwingine wa Wizara hiyo hiyo unakanusha kwa kusema kwamba vikao vya Kamati za Maadili vimekwama hivyo “… kupelekea kuongezeka kwa malalamiko dhidi ya vyombo vya kutoa haki.”
Aidha, wakati Mahakama inadai Mahakama imeendelea kuwapatia motisha na kuboresha maslahi ya wafanyakazi kwa kuwapatia posho za masaa ya ziada, mikopo, zawadi wakati wa sikukuu za kitaifa na za kidini, mafunzo na usafiri kazini; Wizara inakanusha mambo hayo mazuri kwa kudai kuna “kupungua kwa ari ya watumishi kufanya kazi”! Contradictions hizi kati ya kauli za Wizara na taasisi yake kuu zinahitaji maelezo ya kuridhisha kwa Bunge lako tukufu.
TAKWIMU ZILIZOREMBESHWA
Mheshimiwa Spika,
Mahakama ya Tanzania imekuwa na matatizo mengi na sugu yanayotokana na ukosefu wa mgawo wa kibajeti. Matatizo haya yanafahamika na tumeyazungumza sana katika Bunge hili tukufu. Hata hivyo, takwimu zinazotolewa na Wizara na, hasa, Mahakama yenyewe zinaleta tatizo lingine ambalo halihitajiki katika mazingira tuliyo nayo. Hili ni tatizo la sexed up statistics, yaani takwimu zilizorembeshwa. Kuna msemo wa Kiingereza kuhusu takwimu unaosema: statistics are like a woman’s bikini. What they reveal is interesting, but what they conceal is vital! Yaani, takwimu zinafanana na vazi la kuogelea la mwanamke. Zinachokionyesha kinapendeza, lakini zinachokificha ndiyo muhimu zaidi!
Msemo huu unajidhihirisha katika takwimu zilizoletwa mbele ya Bunge lako tukufu na Mahakama ya Tanzania juu ya utendaji kazi wake. Tunaambiwa, kwa mfano, kwamba mwaka 2013 mashauri 168,068 ya aina zote yalisajiliwa. Hata hivyo, kwa mujibu wa takwimu hizo, “… mashauri 182,237 (ya aina zote) yalisikilizwa … na kutolewa hukumu kwa kipindi hicho na kubaki na mashauri 100,109 (ya aina zote) … ilipofika Disemba, 2013.”
Hata kwa mtu asiyekuwa na shahada ya uzamivu ya takwimu, kama ilivyo kwa Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni anayewasilisha Maoni haya, hesabu hizi za Mahakama ya Tanzania zina walakini mkubwa. Haiwezekani kwa mashauri 168,000 kufunguliwa katika mwaka mmoja, halafu mashauri 182,000 yasikilizwe na kutolewa maamuzi na bado yabaki mashauri 100,000 katika mwaka huo huo!
Mheshimiwa Spika,
Tatizo la sexed up statistics linaelekea kuwa sugu katika Mahakama ya Tanzania. Miaka miwili iliyopita, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ililalamika kwamba “... takwimu za mafanikio ya Mahakama ya Tanzania katika kusikiliza na kutoa maamuzi ya mashauri zinapotosha ukweli....”
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilisema wakati ule kwamba “kama hali halisi ingekuwa ndio hii inayoelezewa na Wizara basi ni wazi kwamba nchi yetu ya Tanzania isingekuwa na tatizo la mlundikano wa kesi katika Mahakama zetu zote. Na, kwa hiyo, Wizara ... isingekuwa na changamoto za ‘bajeti finyu isiyokidhi majukumu ya Mahakama’; au ya ‘fedha kutokutolewa kadiri ya mpango wa kazi ... wa mwaka na kwa wakati’ kama inavyodaiwa katika Maelezo ya Wizara hayo hayo yanayotangaza mafanikio makubwa katika usikilizaji wa mashauri na utoaji wa maamuzi ya mashauri hayo.”
Tofauti na Taarifa ya Waziri ya sasa, Maelezo ya Wizara ya mwaka 2012/2013 yalitoa takwimu zilizoonyesha mlundikano wa mashauri ya aina zote katika ngazi mbalimbali za Mahakama. Hivyo ilikuwa sio vigumu kugundua kwamba takwimu za mafanikio makubwa zilikuwa hazilingani na takwimu za mlundikano wa mashauri.
Ndio maana tuliweza kusema kwamba, kwa sababu ya kutopatiwa fedha za kukidhi mahitaji yake halisi, “Mahakama ya Tanzania imeshindwa kabisa kutatua tatizo la mlundikano mkubwa wa kesi katika ngazi zote.” Kwa sababu ambazo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kuzijua, mwaka huu Maelezo ya Mahakama hayana takwimu zozote za mlundikano wa mashauri katika ngazi zote za Mahakama ya Tanzania.
Mheshimiwa Spika,
Pamoja na kutokuwa na taarifa za mlundikano mashauri katika Taarifa ya Waziri na Maelezo ya Mahakama, bado zipo ishara kwamba hali sio nzuri. Hivyo, kwa mfano, Taarifa ya Waziri inaonyesha kwamba idadi ya mahabusu magerezani imepungua kutoka 18,203 mwezi Juni, 2012 na kufikia mahabusu 17,284 mwezi Machi, 2014. Hili ni punguzo la mahabusu 919 au asilimia 5 tu katika kipindi cha karibu miaka miwili!
Takwimu hizi zinaonyesha kwamba badala ya kupungua, tatizo la mlundikano wa mahabusu linaweza kuwa limeongezeka kwa kiasi kikubwa. Katika hali hii, hitimisho letu kuhusu masuala haya katika bajeti ya mwaka 2012/2013 bado ni sahihi: “Kwa ushahidi huu ... ni wazi kwamba Mahakama ya Tanzania imeshindwa kutekeleza wajibu wake huu wa kikatiba kwa sababu ya kunyimwa fedha na vitendea kazi vingine na Serikali hii hii inayodai kwamba dira yake ni ‘haki kwa wote na kwa wakati’!”
Mheshimiwa Spika,
Miaka miwili iliyopita Jaji Mkuu wa Tanzania, Mheshimiwa Mohamed Chande Othman, aliiambia semina juu ya ‘Kudhibiti Ucheleweshaji wa Utatuzi wa Migogoro ya Kibiashara: Usuluhishi Kama Njia ya Kuharakisha Utoaji Haki’, iliyofanyika Dar es Salaam tarehe 20 Julai, 2012, kwamba “… case delay is a sign of an inefficient judicial system.... Excessive case delays may amount to a denial of justice.”
Yaani, “ucheleweshaji wa kesi ni ishara ya mfumo wa kimahakama usiokuwa na ufanisi.... Ucheleweshaji mkubwa wa kesi unaweza kuwa udhumaji wa haki.” Kauli hiyo ya Jaji Mkuu imerudiwa na Waziri ambaye amesema katika Taarifa yake kwamba msingi wa dhima ya Wizara yake ni kuwa “haki iliyocheleweshwa ni sawa na haki iliyodhulumiwa.”
Kama kauli hizi ni za kweli, na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaamini ni za kweli, basi ni kweli vile vile kwamba maelfu ya mahabusu na wafungwa ambao wamejaa katika magereza yetu wakisubiri maamuzi ya kesi zao, na maelfu ya wadaawa ambao kesi zao zimelundikana katika mahakama zetu zote watakuwa wamedhulumiwa haki zao na Serikali hii ya CCM ambayo sera za utoaji haki za hazitekelezeki.
Mheshimiwa Spika,
Katika hotuba yake ya mwaka 2011/2012, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilielezea upungufu mkubwa wa watumishi wa ngazi mbali mbali wa Mahakama ya Tanzania ambao ni matokeo ya moja kwa moja ya kunyimwa fedha na Serikali. Tulirudia maelezo yetu katika Maoni yetu ya mwaka 2012/2013. Miaka mitatu baadaye, tatizo hili halijapatiwa ufumbuzi wowote na kuna uwezekano kwamba linazidi kuwa kubwa zaidi.
Kwa mujibu wa takwimu za Wizara, kwa ujumla wake Wizara ina upungufu wa watumishi 2,521 au asilimia 27 ya mahitaji yake, ambayo ni watumishi 9,351. Kwa upande wa Mahakama, upungufu huo ni asilimia 25 au watumishi 1,891 kati ya 9,627 wanaohitajika. Ili kushughulikia tatizo hilo la uhaba wa watumishi, Serikali hii ya CCM imetoa kwa Mahakama kibali cha ajira mpya kwa ajili ya watumishi 148 ambayo ni sawa na asilimia 8 tu ya wanaohitajika ili kuondoa upungufu huo!
Aidha, Mheshimiwa Spika, katika Maoni yetu ya miaka miwili iliyopita tulieleza jinsi ambavyo Mahakama ya Tanzania “imeendelea kufedheheka kwa kuwa mdeni mkubwa na sugu.” Wakati tunaandika Maoni hayo, Mahakama ya Tanzania inadaiwa na majaji na watumishi wengine wa Mahakama, watoa huduma, wenye nyumba za kupangisha majaji, wajenzi na wazabuni mbali mbali jumla ya shilingi bilioni 5.2.
Fedha zote hizo zilikuwa ni madeni ya miaka ya nyuma hadi kufikia mwaka wa fedha 2010/2011. Hadi Machi 2014, kwa mujibu wa Taarifa ya Waziri, madeni ya Wizara kwa watoa huduma na wakandarasi yamefikia zaidi ya shilingi bilioni 5. Kwa maana nyingine, madeni ya Wizara hayajapungua kwa kiasi chochote cha maana tangu mwaka wa fedha 2011/2012.
Mheshimiwa Spika,
Tulipendekeza, wakati wa mjadala wa Sheria ya Uendeshaji Mahakama miaka mitatu iliyopita, kwamba badala ya Mahakama kutegemea ukomo wa bajeti unaowekwa na Hazina, sheria ielekeze – kama ilivyo kwa Bunge na vyama vya siasa vyenye uwakilishi Bungeni na nchi jirani ya Kenya - kwamba bajeti ya Mahakama ya kila mwaka isiwe pungufu ya asilimia 3 ya bajeti ya kila mwaka ya Serikali ili kuiwezesha Mahakama kuwa na uhakika wa fedha zake na kuiwezesha kupanga mipango yake kwa uhakika zaidi.
Pendekezo letu lilikataliwa na limeendelea kukataliwa na Serikali hii sikivu ya CCM. Matatizo ya bajeti ya Mahakama ambayo tumeyaeleza hapa, na ambayo tumeyaeleza kwenye Maoni yetu ya kila mwaka, yanathibitisha wazi kwamba utaratibu wa sasa wa kutegemea mgawo wa Hazina hauwezi kutatua matatizo ya fedha ya Mahakama ya Tanzania.
Kwa mara nyingine tena, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali itoe kauli Bungeni ni kwa nini inakataa kuihakikishia Mahakama fedha zake kwa kurekebisha Sheria ya Uendeshaji Mahakama ili kuweka a minimum percentage ya bajeti ya Serikali kwa ajili ya Mahakama - kama ilivyofanya kwa Bunge na kwa vyama vya siasa.
HALI YA HAKI ZA BINADAMU
Mheshimiwa Spika,
Hali ya haki za binadamu katika nchi yetu inatisha. Mauaji na mashambulio dhidi ya viongozi wa kidini na waumini wao na sehemu zao za ibada yaliyotokea kati ya mwaka 2012 na 2013 hayajatatuliwa hadi leo. Hakuna mtu yeyote ambaye ameadhibiwa kwa mauaji ya padre mmoja wa Kanisa Katoliki Zanzibar. Hakuna aliyeadhibiwa kwa shambulio la risasi na la tindikali dhidi ya mapadre wengine wawili wa Kanisa hilo huko huko Zanzibar wala kwa shambulio la tindikali dhidi ya Msaidizi wa Mufti wa Zanzibar.
Hakuna aliyetiwa hatiani wala kuadhibiwa kwa kuhusika na shambulio la bomu katika Kanisa Katoliki Olasiti Arusha lililoua watu watatu na kujeruhi wengine wengi. Serikali ya CCM haijatoa taarifa yoyote rasmi hadharani au Bungeni juu ya wahusika wa mauaji na mashambulio hayo na sababu zake. Hakuna mtu aliyepatikana na hatia ama kuadhibiwa kwa kuhusika na mauaji na mashambulio hayo hadi sasa.
Mauaji na mashambulio ya waandishi wa habari na wanaharakati wengine kama madaktari yaliyotokea kati ya 2012 na 2013 hayajatatuliwa pia. Maafisa wa Jeshi la Polisi walioamuru mauaji ya mwandishi wa habari Daudi Mwangosi hawajachukuliwa hatua yoyote. Badala yake, aliyekuwa kamanda wa polisi hao amepandishwa vyeo na kuhamishiwa Makao Makuu ya Jeshi la Polisi. Huu ni ushahidi wa wazi kabisa kwamba mauaji hayo yalipangwa na/au yalifanywa kwa maelekezo ya Serikali ya CCM.
Maafisa wa Idara ya Usalama wa Taifa na wa Jeshi la Polisi waliohusika kumteka nyara na kumtesa Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari Tanzania, Dk. Steven Ulimboka hawajakamatwa hadi leo licha ya majina yao kujulikana. Raia wa Kenya aliyebambikiziwa kesi ya kumteka Dk. Ulimboka amekwishaachiliwa huru na mahakama. Serikali ya CCM haijatoa taarifa yoyote rasmi hadharani au Bungeni kuhusu jambo hili. Huu ni ushahidi wa kuhusika kwa Serikali ya CCM katika shambulio hilo.
Hakuna aliyekamatwa wala kuadhibiwa kwa kumteka nyara na kumtesa aliyekuwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Absalom Kibanda. Serikali ya CCM haijatoa taarifa yoyote rasmi hadharani au Bungeni kuhusu shambulio hilo linalofanana na shambulio dhidi ya Dk. Ulimboka. Serikali hii ya CCM ina wajibu kisheria na kisiasa wa kulinda maisha ya Watanzania na mali zao. Imeshindwa kutekeleza wajibu huo kwa Watanzania.
DEMOKRASIA KITANZINI!
Serikali ya CCM imeitia demokrasia kitanzini na inatishia kuinyonga na kuiua. Mikutano halali ya vyama vya siasa vya upinzani imeshambuliwa kwa mabomu na risasi za moto na Jeshi la Polisi. Watu wengi wameuawa katika mashambulizi hayo. Wengine wengi wamejeruhiwa. Viongozi, wanachama na hata wapita njia tu wamepigwa, kukamatwa na kufunguliwa mashtaka ya jinai kwa kushiriki mikutano halali ya vyama vya siasa vya upinzani.
Jeshi la Polisi likishirikiana na watumishi wa Idara ya Usalama wa Taifa na viongozi na makada wa CCM wameshirikiana kuwabambikizia viongozi na wanachama wa CHADEMA kesi za uongo za ugaidi. Wengi wameteswa kwa ukatili mkubwa baada ya kukamatwa na kuhojiwa katika vituo vya polisi katika kesi hizi. Hadi sasa Serikali hii ya CCM haijasema chochote juu ya kufutwa kwa kesi za uongo za ugaidi walizofunguliwa viongozi na wanchama wa CHADEMA kama vile Wilfred Lwakatare na Henry Kilewo. Walioshiriki kutunga mashtaka hayo ya kidhalimu hawajachukuliwa hatua yoyote.
MATUMIZI HARAMU YA NGUVU ZA KIJESHI!
Serikali ya CCM imewageuka Watanzania walioipigia kura na kuwaua, kuwatesa na kuwatia vilema vya maisha, kuwabaka, kuwafukuza kwenye maeneo yao na kuwafanya wakimbizi wa ndani au internally displaced persons (IDPs). Badala ya kulinda mali zao, Serikali ya CCM imekuwa mwizi wa mali za wananchi. Serikali ya CCM imeendesha Operesheni Kimbunga kwa kisingizio cha kuondoa wahamiaji haramu nchini. Matokeo ya Operesheni hiyo ni kwamba maelfu ya watu wasiokuwa na hatia wa mikoa ya Kagera na Kigoma – inayopakana na Burundi na Rwanda – walikamatwa, kuteswa na kuporwa mifugo, fedha na mali zao nyingine na makazi yao kuharibiwa.
Utaratibu wa kisheria wa kuwakamata watuhumiwa, kuwapeleka mahakamani, kuwapata na hatia na kuwaadhibu kwa mujibu wa sheria umepuuzwa. Cha kushangaza Operesheni Kimbunga haikuihusu mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Mara, Mbeya, Mtwara, Rukwa na Ruvuma ambayo inapakana na nchi jirani za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Kenya, Malawi, Msumbiji na Zambia ambayo nayo pengine ina wahamiaji haramu. Katika mazingira haya, ni sahihi kuamini kwamba Operesheni Kimbunga ilikuwa ni lengo la kuwaadhibu watu wenye asili ya Rwanda kwa sababu ya mgogoro wa kidiplomasia kati ya Rais Jakaya Kikwete na Rais Paul Kagame wa Rwanda.
Hata kabla vumbi lililotimuliwa na Operesheni Kimbunga halijatulia, Serikali ya CCM ilianzisha vita nyingine kubwa dhidi ya Watanzania. Hii ni Operesheni Tokomeza Ujangili. Licha ya jina lake, Operesheni hiyo imetokomeza maisha ya Watanzania wasiokuwa na hatia yoyote. Makumi ya watu wameuawa, mamia wamejeruhiwa, maelfu wamekamatwa na kuteswa, vijiji vizima vimechomwa moto na makazi ya wananchi kuharibiwa, mifugo imeuawa ama kuporwa kwa mtutu wa bunduki, mashamba na mazao yameharibiwa na maelfu ya wananchi wametiwa umaskini mkubwa na Serikali hii ya CCM.
Hatimaye, baada ya kelele kubwa ndani na nje ya Bunge, Operesheni Tokomeza ilisitishwa na Mawaziri wa Ulinzi, Mambo ya Ndani, Maliasili na Utalii na Mifugo wakaondoshwa madarakani kwa sababu ya Operesheni hiyo. Walioua, kutesa na kulemaza Watanzania na kuwaibia au kuharibu mali zao hawajakamatwa wala kuchukuliwa hatua zozote za kisheria.
Operesheni Kimbunga na Tokomeza zilikuwa Operesheni za Kijeshi. Zilianzishwa, kuongozwa na kutekelezwa na maafisa na askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania na vikosi vingine vya ulinzi na usalama. Operesheni hizi za kijeshi zimefanyika wakati Tanzania haiko vitani na wala haiko katika hali ya vita. Rais Kikwete hakutangaza vita wala kuwepo kwa hali ya vita kwa mujibu wa Katiba ili kuweza kuamuru kutekelezwa kwa Operesheni hizi za kijeshi.
Hakukuwa na maasi au vurugu zozote zozote za kijamii. Kwa sababu hiyo, hakuna Mkuu wa Mkoa yeyote aliyeomba msaada wa kijeshi ili kuwezesha matumizi ya Majeshi ya Ulinzi katika kusaidia mamlaka za kiraia kama inavyotakiwa na Sheria ya Ulinzi wa Taifa, 1970 na Kanuni zake. Kwa kila namna inavyoonekana, Operesheni Kimbunga na Operesheni Tokomeza zilikuwa ni matumizi haramu ya nguvu za kijeshi dhidi ya raia. Kama hii haitoshi, sasa Serikali hii ya CCM inazungumza kuianzisha tena Operesheni hii dhidi ya wananchi wa Tanzania!


TUME YA UCHUNGUZI YA JAJI MSUMI
Mheshimiwa Spika,
Tume ya Uchunguzi iliyoahidiwa Bungeni na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuchunguza masuala yanayohusu ukiukwaji huu wa haki za binadamu imeundwa Rais kupitia Tangazo la Serikali Na. 131 la tarehe 2 Mei, 2014. Tume hiyo inaongozwa na Jaji Kiongozi mstaafu Hamisi Amir Msumi na Makamishna wenzake Majaji wastaafu Stephen Ihema na Vincent Kitubio Damian Lyimo.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inafahamu na kutambua utumishi uliotukuka wa Jaji Kiongozi Msumi. Hata hivyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haina imani kabisa na uteuzi wa Makamishna Ihema na Lyimo. Itakumbukwa kwamba tarehe 13 Julai, 2012, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ililalamikia uteuzi wa Majaji wa Mahakama Kuu “... wakiwa wamekaribia muda wao wa kustaafu kwingineko katika utumishi wa umma (na) wanapewa ‘zawadi’ ya ujaji ili kuwawezesha kupata mafao ya Majaji wastaafu ambayo yameboreshwa sana katika miaka ya karibuni.”
Ushahidi tuliowasilisha mbele ya Kamati ya Haki, Madaraka na Maadili ya Bunge baada ya Msemaji wa Kambi kushtakiwa kwenye Kamati hiyo kwa kile kilichoitwa ‘kuwadhalilisha’ majaji uliwahusisha Majaji wastaafu Ihema na Lyimo katika kundi la Majaji ambao uteuzi wao tuliupigia kelele. Sehemu ya ushahidi huo inaonyesha kwamba tarehe 16 Juni 2003, aliyekuwa Mwenyekiti CCM wa Mkoa wa Singida, Mzee Joram Allute alimwandikia Rais Benjamin Mkapa maombi ya kumwondoa Jaji Ihema kama Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania ‘kwa uzembe na kukosa maadili.’ Mzee Allute alikuwa na kesi kwa Jaji Ihema ambapo Jaji huyo ‘alikalia’ uamuzi kwa zaidi ya miaka minne hadi aliponyang’anywa faili la kesi hiyo na kukabidhiwa Jaji mwingine aliyeandika uamuzi huo ndani ya wiki tatu! Mwezi mmoja kabla ya barua ya Mzee Allute kwa Rais Mkapa, mawakili wake walikuwa wamemwandikia Jaji Mkuu Barnabas Samatta kulalamikia ucheleweshaji wa uamuzi wa kesi hiyo. Mawakili hao walidai: “Hadhi na heshima ya Mahakama inaporomoka vibaya kama inachukua zaidi ya miaka mitatu kwa Jaji kutafakari na kutoa uamuzi kwa jambo jepesi kama maombi ya pingamizi.”
Mheshimiwa Spika,
Sio tu kwamba Jaji mstaafu Ihema ana rekodi mbaya ya kijaji, bali pia ana rekodi ya kutumiwa na Serikali hii ya CCM kuisafisha Serikali kwa matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu unaofanywa na watendaji wa Serikali. Mwaka 2012, mara baada ya Jeshi la Polisi mkoani Iringa kumuua Daudi Mwangosi aliyekuwa mwandishi habari wa Kituo cha Televisheni cha Channel Ten, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mheshimiwa Dkt. Emmanuel Nchimbi alimteua Jaji Ihema kuongoza Kamati iliyoundwa na Waziri Nchimbi kuchunguza mauaji ya Marehemu Mwangosi. Taarifa ya Uchunguzi wa Kifo cha Mwandishi wa Habari wa Channel Ten Bw. Daudi Mwangosi, iliyoandaliwa na Kamati ya Jaji Ihema ni mfano wa namna ya kuisafisha Serikali kutoka kwenye lawama ya mauaji ya raia wake. Taarifa hiyo ilitofautiana kimsingi na Taarifa ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ya Uchunguzi wa Tukio Lililopelekea Kifo cha Daudi Mwangosi Kilichotokea Septemba 2, 2012 Kijijini Nyololo, iliyoandaliwa na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora; na Ripoti ya Timu Maalum ya Uchunguzi Iliyoteuliwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT) na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) Kuchunguza Mazingira Yaliyopelekea Kuuawa kwa Mwandishi wa Habari Daudi Mwangosi Septemba 2, 2012 Katika Kijiji cha Nyololo, Wilaya ya Mufindi, Mkoani Iringa, iliyotolewa na Baraza la Habari Tanzania (MCT) na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF).
Kwa upande wake, Jaji Lyimo aliteuliwa tarehe 28 Machi 2007, mwaka mmoja kabla ya muda wake wa kustaafu kwa mujibu wa sheria. Hata hivyo, ilipofika tarehe 26 Oktoba, 2007 Katibu Mkuu Kiongozi wa wakati huo Phillemon Luhanjo alimtaarifu Jaji Mkuu kwamba Rais Kikwete “... ameamua kusogeza mbele muda wa kustaafu wa Mhe. Jaji Vincent Kitubio Damian Lyimo ... kwa miaka mitatu ... kuanzia tarehe 28 Machi 2008, siku ambayo angestaafu kwa lazima.”
Uteuzi wa Majaji hawa na wengineo wenye sifa kama hizo ulilalamikiwa mno na majaji wengine kiasi kwamba ‘Kikundi Kazi kwa Ajili ya Kuchambua na Kushauri Kuhusu Ajira ya Majaji Baada ya Kustaafu’ chini ya Ofisi ya Rais, kilihitimisha, katika Taarifa yake tarehe 7 Machi 2008, “inaonekana wazi kuwa suala la ajira za mikataba kwa Majaji ambao wamekuwa wakifanya kazi za Jaji baada ya kufikia umri wa kustaafu ni kinyume cha Katiba.”
Sasa Majaji hawa ndiyo wamepewa jukumu la kuchunguza matukio ya ukiukwaji haki za binadamu ambayo hayana mfano katika historia ya Tanzania tangu uhuru. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haina imani yoyote na uteuzi wa Majaji Ihema na Lyimo na inapendekeza uteuzi wao ufutwe na majaji wenye sifa bora zaidi wateuliwe kwa ajili ya kazi hii muhimu. Vinginevyo matokeo ya Tume ya Msumi hayatakubaliwa na umma wa Watanzania.
UENDESHAJI MASHTAKA YA JINAI
Mheshimiwa Spika,
Mamlaka ya uendeshaji wa mashtaka ya jinai yamekasimiwa kwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka kwa mujibu wa ibara ya 59B(2) ya Katiba. Mamlaka haya yamefafanuliwa na kutiliwa nguvu na kifungu cha 16(1) cha Sheria ya Utumishi wa Mashtaka ya Taifa, Na. 27 ya 2008 (National Prosecutions Service Act, 2008).
Kwa mujibu wa kifungu hicho, Mkurugenzi wa Mashtaka ana mamlaka sio tu ya kudhibiti mashtaka yote ya jinai bali pia kuratibu shughuli za upelelezi wa makosa ya jinai. Aidha, kwa mujibu wa kifungu cha 17(1) na (3), Mkurugenzi ana uwezo wa kutoa maelekezo ya maandishi kwa ofisa yeyote wa umma ili apatiwe taarifa yoyote inayohusu upelelezi au uendeshaji wa mashtaka ya jinai na ofisa huyo anatakiwa kutii maelekezo hayo.
Ili kumwezesha Mkurugenzi wa Mashtaka kutekeleza wajibu wake wa kikatiba kwa uhuru kamili na bila woga au upendeleo, Mkurugenzi wa Mashtaka amewekewa kinga ya ajira yake. Hivyo, kwa mfano, ibara ya 59B(4) ya Katiba inaelekeza kwamba katika kutekeleza mamlaka yake, “Mkurugenzi wa Mashtaka atakuwa huru, hataingiliwa na mtu yeyote au na mamlaka yeyote na atazingatia ... nia ya kutenda haki, kuzuia matumizi mabaya ya taratibu za utoaji haki na maslahi ya umma.”
Aidha, kwa mujibu wa kifungu cha 19(1) na (2) cha Sheria ya Utumishi wa Mashtaka ya Taifa, sifa, masharti na mafao ya ajira ya Mkurugenzi wa Mashtaka yatakuwa sawa na yale ya ajira ya Jaji wa Mahakama Kuu. Vile vile, kufuatana na kifungu cha 19(3), Mkurugenzi wa Mashtaka hawezi kuondolewa kwenye madaraka yake isipokuwa kwa kushindwa kutimiza wajibu wake kwa sababu ya ugonjwa au kwa kukiuka Kanuni za Maadili ya Kitaaluma chini ya Sheria ya Utekelezaji wa Mamlaka ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Sura ya 268 ya Sheria za Tanzania. Hii ndio kusema kwamba, kwa mujibu wa Sheria Na. 27 ya 2008, utaratibu wa kumwondoa Mkurugenzi wa Mashtaka kwenye ajira yake hauna tofauti na utaratibu wa kumwondoa Jaji wa Mahakama Kuu kwenye ajira yake.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaamini kwamba utaratibu huu wa kikatiba na kisheria umempa Mkurugenzi wa Mashtaka nyenzo za kutosha kisheria za kupambana na uhalifu mkubwa hapa nchini na vile vile kuzuia matumizi mabaya ya mfumo wa uendeshaji na utoaji haki na hasa hasa ya mfumo wa mashtaka ya jinai. Hata hivyo, Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inashangazwa na kusikitishwa na kushindwa kwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka kufungua na/au kuendesha mashtaka yanayohusu matukio makubwa ya uhalifu ambayo yametikisa taifa letu katika mwaka huu wa fedha na kabla ya hapo.
Tarehe 16 Juni, 2013, mkutano wa hadhara wa kampeni za uchaguzi wa madiwani uliokuwa unafanywa na viongozi wakuu wa CHADEMA katika eneo la Soweto mjini Arusha ulishambuliwa kwa mabomu na risasi za moto. Watu watatu waliuawa pale pale na mwingine alifia hospitalini baadaye. Wengine wengi walijeruhiwa vibaya.
Hadi sasa Serikali hii ya CCM haijatoa taarifa yoyote rasmi, ndani ya Bunge hili au nje, juu ya waliohusika na mashambulizi haya ya kigaidi. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kufahamu hatua zozote, kama zipo, zilizochukuliwa na Mkurugenzi wa Mashtaka kuchunguza tukio hilo la kigaidi. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kujua matokeo yoyote, kama yapo, ya uchunguzi wa tukio hilo.



UTEKELEZAJI WA MAELEKEZO YA MAHAKAMA
Mheshimiwa Spika,
Eneo lingine ambalo linahitaji majibu linahusu utekelezaji wa maelekezo ya Mahakama Kuu ya Tanzania juu ya marekebisho ya sheria ambazo Mahakama Kuu imetamka kwamba zinakiuka Katiba. Kama tulivyosema katika Maoni yetu miaka miwili iliyopita, mfumo wa dhamana chini ya kifungu cha 148(5)(a) cha Sheria ya Mwenendo wa Jinai ambao unaokataza dhamana kwa idadi kubwa ya watuhumiwa wa makosa yaliyotajwa katika aya (e) ndiyo sababu kubwa ya magereza kufurika mahabusu na mlundikano wa kesi za jinai kwa ujumla.
Kwa sababu hiyo, Mahakama Kuu ilitamka, katika kesi ya Jackson s/o ole Nemeteni @ ole Saibul @ Mdosi @ Mjomba na wenzake 19 dhidi ya Mwanasheria Mkuu, Shauri la Madai Na. 117 la 2004, kwamba bila kuwepo utaratibu uliowekwa na sheria kama inavyoelekezwa na ibara ya 15(2)(a) ya Katiba, “utekelezaji wa masharti ya kifungu cha 148(5)(a) umetumiwa vibaya.” Kwa sababu hiyo, Mahakama Kuu ilitamka kwamba kifungu hicho kinachokataza dhamana kwa watuhumiwa wa makosa ya wizi wa kutumia silaha ni kinyume cha ibara ya 15(2)(a) ya Katiba.
Kuhusiana na kifungu cha 148(5)(e) cha Sheria ya Mwenendo wa Jinai kinachoweka masharti ya dhamana ‘yasiyotekelezeka’ kwa watuhumiwa wa makosa ya uhujumu uchumi, Mahakama Kuu – katika kesi ya Prof. Dr. Costa Ricky Mahalu & Mwenzake dhidi ya Mwanasheria Mkuu, Shauri la Maombi Na. 35 la 2007 – ilitamka kwamba kifungu hicho ni cha kibaguzi kwa watuhumiwa maskini na kinakiuka matakwa ya ibara ya 13(2) ya Katiba inayokataza ubaguzi ‘ama wa dhahiri au kwa taathira....’
Kwa kutumia mamlaka yake chini ya ibara ya 30(5) ya Katiba, badala ya kukifuta kifungu hicho, Mahakama Kuu katika kesi zote mbili iliielekeza Serikali ifanye marekebisho katika kifungu cha 148(5)(a) na (e) ya Sheria ya Mwenendo wa Jinai ili kuweka utaratibu bora zaidi wa kushughulikia dhamana za watuhumiwa wa makosa ya wizi wa kutumia silaha na wa uhujumu uchumi. Katika Kesi ya Jackson s/o ole Nemeteni, Mahakama Kuu ilitoa muda wa miezi kumi na nane – kuanzia tarehe 13 Julai, 2007. Na katika Kesi ya Prof. Dr. Costa Ricky Mahalu, Mahakama Kuu ilitoa muda wa mwaka mmoja kuanzia tarehe 4 Oktoba, 2010. Hii ina maana kwamba Serikali ilitakiwa iwe imetekeleza maelekezo ya Mahakama Kuu juu ya kifungu cha 148(5)(a) kufikia tarehe 12 Desemba, 2008. Aidha, Serikali ilitakiwa kutekeleza maelekezo ya Mahakama Kuu kuhusu kifungu cha 148(5)(e) kufikia tarehe 3 Oktoba, 2011.
Huu ni mwaka wa tano na nusu tangu kwisha kwa muda uliowekwa katika Kesi ya Jackson s/o ole Nemeteni lakini Serikali haijafanya marekebisho tajwa ya Sheria ya Mwenendo wa Jinai. Aidha, huu ni karibu mwaka wa tatu tangu muda uliowekwa katika Kesi ya Prof. Dr. Costa Ricky Mahalu lakini Serikali haijatekeleza maelekezo hayo.
Kuhusiana na utekelezaji wa maelekezo ya Mahakama Kuu katika Kesi ya Prof. Dr. Costa Ricky Mahalu, Mwanasheria Mkuu ametoa maelezo kwamba “Serikali haikuridhika na uamuzi huo na hivyo iliamua kukata rufaa katika Mahakama ya Rufani kwa kutoa notisi ili kupinga uamuzi huo.” Mwanasheria Mkuu ameeleza kwamba “marekebisho ya kifungu hicho hayajafanywa kwa kuwa rufaa dhidi ya uamuzi huo haijasikilizwa.”
Mheshimiwa Spika,
Mwanasheria Mkuu hajasema ni lini Serikali ilitoa notisi ya rufaa dhidi ya uamuzi wa Mahakama Kuu. Aidha, Mwanasheria Mkuu hajasema kama tayari Serikali imeshakata rufaa hiyo, ijapokuwa maelezo yake yanaashiria kwamba rufaa hiyo bado haijawasilishwa kwenye Mahakama ya Rufani.
Kwa sababu hiyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaamini kwamba Serikali hii ya CCM inaweza kuwa inatumia vibaya masharti ya kifungu cha 14(3) cha Sheria ya Utekelezaji wa Haki za Binadamu, Sura ya 3 ya Sheria za Tanzania, yaani The Basic Rights and Duties Enforcement Act, Chapter 3 of the Laws of Tanzania. Kifungu hicho kinazuia utekelezaji wa uamuzi wowote wa Mahakama Kuu pale ambapo Serikali imewasilisha notisi ya rufaa yenye kuonyesha nia ya kupinga uamuzi husika.
Kwa kutumia kifungu hicho, Serikali inaweza kuzuia uamuzi huo kwa kutoa notisi ya rufaa tu bila kulazimika kukata rufaa yenyewe na utaratibu mzima wa kurekebisha sheria mbovu na za kikandamizaji kwa kutumia Mahakama ukasitishwa. Kwa sababu hiyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali hii ya CCM itoe nakala ya notisi ya rufaa iliyoiwasilisha katika Mahakama ya Rufani katika Kesi ya Prof. Dr. Costa Ricky Mahalu. Hii ni muhimu ili kuhakikisha kwamba taarifa ya Mwanasheria Mkuu ni ya kweli.
Aidha, kama itathibitika kuwapo kwa notisi hiyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali hii ya CCM kutoa kauli rasmi mbele ya Bunge hili tukufu ni lini inatazamia kuwasilisha rufaa ambayo tayari imekwishaitolea notisi.
Mheshimiwa Spika,
Kuhusiana na Kesi ya Jackson s/o ole Nemeteni, Serikali haijatoa maelezo yoyote kwa nini haijatekeleza maelekezo ya kikatiba ya Mahakama Kuu kwa karibu miaka sita. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali itoe kauli rasmi kama, na lini, inatarajia kutekeleza maelekezo hayo ya Mahakama Kuu. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inahoji kama hii sio dharau ya Serikali hii ya CCM kwa Mahakama ya Tanzania ni kitu gani?
HITIMISHO
Mheshimiwa Spika,
Katika kuhitimisha maoni haya, napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza viongozi wakuu wa vyama vyetu vitatu vinavyounda Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa kufanya maamuzi ya kuendeleza ushirikiano ulioanzia ndani ya Bunge Maalum, kwenye Bunge lako tukufu. Kwa sababu ya maamuzi hayo, imewezekana kwa Naibu Waziri Kivuli wa Sheria na Katiba, Mheshimiwa Rashid Ali Abdallah, kushirikiana nami katika kuandaa na kuwasilisha Maoni haya. Naomba nitumie fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Rashid Abdallah kwa kuteuliwa kwenye nafasi hiyo na kumshukuru kwa ushirikiano wake katika kuandaa Maoni haya.
Mheshimiwa Spika,
Baada ya maelezo haya marefu, naomba kukushukuru na wewe binafsi na naomba kuwasilisha.


---------------------------------------------------------------
Tundu Antiphas Mughwai Lissu
MSEMAJI & WAZIRI KIVULI, WIZARA YA KATIBA NA SHERIA

No comments: