Sunday, June 15, 2014

CUF WATOA MAONI YAO KUHUSU BAJETI MWAKA HUU,LIPUMBA ASEMA IMEJAA ULAGHAI KWA WANANCHI-TAMKO LOTE LIKO HAPA

BAJETI, DEMOKRASIA NA UTAWALA BORA
Katika nchi yenye mfumo wa demokrasia ya kweli ambapo viongozi wa Serikali wanachaguliwa katika Chaguzi zilizo huru na za haki, sera ya maendeleo ya Taifa ni mkataba kati ya Serikali na wananchi. Serikali ikishindwa kutimiza mkataba huu, wananchi wanaiwajibisha Serikali katika uchaguzi kwa kuiondoa madarakani.

Bajeti ni nyenzo muhimu ya sera ya Serikali yeyote. Bajeti ni kielelezo cha maeneo ambayo Serikali inayapa kipaumbele. Bajeti ni kioo cha mapato na matumizi kinachoonesha maeneo ambayo Serikali inayapa kipaumbele.

Serikali yapaswa kukusanya mapato toka kwa walipa kodi kwa uadiifu na kupanga na kutumia mapato hayo kwa uangalifu katika maeneo yatakayotoa huduma bora kwa wananchi na kuchochea maendeleo.

Malengo ya uchumi mpana ni kukuza uchumi, matunda ya kukua kwa uchumi yawafikie wananchi wote, na uchumi usiyumbishwe kwa mfumko wa bei, ukosefu wa fedha za kigeni na thamani ya sarafu kuporomoka au kupanda sana. Uchumi unapoyumbishwa na mfumko mkubwa wa bei au thamani ya sarafu kubadilika badilika kwa kiasi kikubwa unapunguza motisha kwa sekta binafsi ikiwa ni pamoja na biashara ndogo na za kati kuwekeza na kwa hiyo kukuza uchumi wa kuongeza ajira.




Ili uchumi usiyumbe ni muhimu kuwa na nidhamu katika sera za mapato na matumizi ya sekta ya fedha za umma.


Madhumuni ya sera bora ya matumizi ya fedha za umma ni kuwa na nidhamu katika matumizi (fiscal discipline), kupanga na kutumia fedha kufuatana na vipaumbele vya sera na kuwa na usimamizi mzuri wa matumizi haya siku hadi siku.

Usimamizi mzuri wa siku hadi siku unasisitiza kuwepo kwa tija katika matumizi ya Serikali. Gharama za kununua bidhaa na huduma ziwe za chini huku ukizingatia ubora wa bidhaa na huduma zenyewe. Matumizi ya Serikali yafanikishe malengo ya sera kwa mfano fedha zilizotengwa katika sekta ya elimu zifanikishe watoto wapate elimu iliyo bora.


Nidhamu katika mapato na matuizi kunategemea makadirio mazuri ya mapato na matumizi.


Bajeti isiyotabirika inahujumu vipaumbele vya sera na matokeo ya matumizi ya Serikali. Ikiwa fedha za kununulia madawa  hazipatikani kwa wakati malengo ya kuendeleza na kuboresha afya za wananchi hayawezi kufikiwa.

Uwajibikaji wa kweli unasehemu mbili. Sehemu ya kwanza ya uwajibikaji na wajibu wa kutoa maelezo ya utekelezaji wa mambo muhimu uliyopewa kwa wadhifa ulionao. Viongozi wa Wizara, Idara za Serikali na Mashirika ya Umma wanawajibika kutoa maelezo ya matumizi ya fedha ya Serikali katika maeneo yao na malengo gani yamefikiwa katika matumizi hayo. Sehemu ya pili ya uwajibikaji ni kuwepo na motisha wa kutambuliwa kwa utekelezaji na matumizi mazuri ya fedha za Umma na kufikia malengo na kibano kwa utekelezaji mbovu na kutofikia malengo. 

    Hapawezi kuwa na uwajibikaji wa kweli bila kuwepo na motisha na kibano kufuatilia tathmini na uhakiki wa matumizi ya fedha na malengo yaliyofikiwa.

Uwajibikaji unahitaji kupata maoni ya wananchi wanaotumia huduma za Serikali kuhusu ubora wa huduma hizo ikiwa  ni pamoja na huduma ya miundo mbinu kama vile barabara, maji, umeme na kadhalika na huduma za jamii kama vile elimu na huduma za afya.

Katika shuguli za bajeti utekelezaji wa majukumu utakuwa umefanikiwa ikiwa malengo yaliyowekwa yamefanikiwa kwa mafungu ya fedha zilizotengwa bila kuathiri ubora wa malengo yenyewe na kuheshimu taratibu na sheria zilizowekwa.

Usimamizi wa matumizi ya fedha za Umma ulenge katika kupanga na kuyapima matokeo ya matumizi ya fedha hizo.

Ufisadi ni tatizo katika matumizi ya fedha za Umma. Lengo moja la kuboresha  matumizi ya fedha za umma ni kupunguza mianya ya rushwa na inapotokea kuhakikisha wanaohusika wanachukuliwa hatua kali. Pamoja na kuporomosha maadili ya nchi, ufisadi unadhoofisha nidhamu katika matumizi ya fedha za Umma, unaharibu mgao wa fedha za umma katika sekta na maeneo mbali mbali ya matumizi na unapunguza tija na ufikiwaji wa malengo ya matumizi ya fedha za umma. Ufisadi ni matumizi mabaya ya wadhifa uliopewa kwa manufaa binafsi.


MISINGI MIZURI YA BAJETI
Bajeti ya Serikali ijumlishe mapato na matumizi yote ya Serikali bila kujali taratibu maalum za kuendesha baadhi ya miradi na programmu, taratibu za kuidhinisha matumizi na vyanzo vya mapato.

Kwa ujumla mapato yote yakusanywe na matumizi kupangwa bila kujali chanzo cha mapato. ikiwa kuna mahusiano ya karibu kati ya mapato na wanaonufaika na matumizi ya mapato hayo, hoja ya mapato husika  kulipia matumizi ya huduma inakubalika.

Maamuzi ya Serikali na viongozi ambayo yanahitaji matumizi ya fedha za Serikali katika mwaka wa bajeti au miaka ijayo yawekwe wazi na kuchambuliwa.

Utayarishaji wa bajeti uzingatie:-
i)             Kufikia malengo ya uchumi mpana. Ukuaji wa pato la taifa, mfumko wa bei, akiba ya fedha za kigeni, thamani ya sarafu.
ii)           Matumizi yagawiwe kulingana na malengo ya sera ya taifa.
iii)         Kujenga mazingira ya utekelezaji mzuri wa bajeti.

Jambo linaloathiri sera, utayarishaji na utekelezaji wa bajeti bora ni uanzishaji wa sera na utamkaji wa ahadi katika majukwaa ya siasa ambao hayaendani na vipaumbele vilivyotumiwa kuandaa bajeti.

Bajeti ni kioo cha sera za Serikali. Ni muhimu kwa bajeti kuwa na mahusiano na sera. Ili kuwa na bajeti nzuri ya nchi ni muhimu:-
i.             Kuratibu vizuri uanzishaji wa sera
ii.           Kushirikisha umma katika kuanzisha sera
iii.         Kuwa na utaratibu mzuri wa kupitia na kutathmini sera na bajeti za Serikali katika bunge.
iv.         Uchambuzi wa kina wa mahitaji ya fedha na rasilimali nyingine ya mapendekezo ya bajeti na kuhakikisha kuwa bajeti ndiyo inayoshika hatamu katika mapato na matumizi ya Serikali.

Maandalizi ya bajeti yazingatie hali halisi ya uchumi. Ni muhimu kuwa na makadirio sahihi ya mapato na kuyatambua matumizi yote ya lazima.

Uandaaji wa bajeti uanze kwa kutambua mapato yatakayopatikana katika kipindi cha bajeti. Wizara na idara zijulishwe mapema viwango vya juu vya matumizi katika maeneo yao. Wizara na Idara zikadirie gharama za matumizi yao kufikia malengo yaliyowekwa huku wakizingatia ukomo wa matumizi yaliyowekwa.

Mfumo wetu wa Bunge tumeurithi toka Uingereza. Mamlaka na madaraka ya Bunge katika masuala ya bajeti ni mdogo sana. Madaraka ya Bunge ni kutathmini utekelezaji kama ulifuata bajeti iliyopita. Bunge halina mamlaka ya kuandaa Bajeti. bunge halina madaraka ya kuanzisha muswada wowote utakaohitaji matumizi ya fedha za Serikali.

Hali halisi ya Tanzania ni kwamba utayarishaji wa bajeti unategemea kikundi kidogo cha wataalamu wa Tanzania katika Wizara ya Fedha na Benki Kuu, na Wataalamu wa Mashirika ya misaada hasa Benki ya Dunia, Shirika la Fedha na kimataifa, na mashirika toka nchi za Jumuiya ya Ulaya. Bunge na Kamati zake hazina mamlaka ya kubadilisha bajeti ya Serikali.

TATHMINI YA MALENGO MAKUU YA SERA ZA SERIKALI

Kila bajeti, Serikali inaeleza katika hotuba ya bajeti kuwa Misingi na shabaha ya Bajeti imezingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025 ambayo inalenga kuwa Tanzania iwe ni nchi yenye kiwango cha kati cha mapato (middle income country) na hali bora ya maisha kwa wananchi; Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2010; MKUKUTA, Mpango wa Maendeleo ya miaka 5 na Malengo ya Maendeleo ya Milenia. Hata hivyo Waziri hafanyi uchambuzi wa kina kuonyesha jinsi sera za bajeti na matumizi ya serikali yanatekeleza mikakati hiyo, mafanikio yaliyofikiwa, vikwazo vilivyopo na vinavyokabiliwa na serikali.

Kwa mfano Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya CCM iliahidi kujenga kituo cha kufua umeme wa MW 300 Mnazi Bay Mtwara. Kwa kuzingatia Ilani ya CCM, Rais Kikwete ambaye ndiye Mwenyekiti wa Tume ya Mipango aliwaeleza Watanzania katika hotuba yake yakuukaribisha mwaka mpya tarehe 31 Desemba 2010 aliwaeleza Watanzania kuwa na ninanukuu “Kwa kushirikiana na sekta binafsi pia, ndani ya miezi 36 ijayo TANESCO wanatarajia kukamilisha ujenzi wa vituo vya umeme huko Kinyerezi (MW 240) Somanga Fungu (MW 230) na Mtwara (MW 300). Inatarajiwa pia kwamba katika kipindi hicho mradi wa kuzalisha MW 200 pale Kiwira utakamilika.” 

     Sasa ni miezi 42 toka Rais Kikwete atamke maneno hayo Bajeti inayotekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM imeifikisha wapi miradi hii? Wananchi wa Mtwara walipouliza mradi wa kufua umeme Mtwara umefikia wapi? Majibu ya CCM ilikuwa kuwapiga na kuwawekea utawala wa kijeshi. Ni vyema Mawaziri wakawa waungwana kama alivyokuwa Rais Mkapa mwaka 1996 alipoeleza kuwa Ilani ya Uchaguzi ya CCM haitekelezeki.

       MKUKUTA uliweka lengo la kufikia ukuaji wa uchumi wa asilimia 10 kwa mwaka. Hotuba za bajeti zinaeleza kuwa Bajeti inazingatia malengo ya MKUKUTA lakina hakuna uchambuzi unaoeleza kwa nini lengo la kukuza uchumi kwa asilimia 10 halijafikiwa.

Waziri ameeleza kuwa Bajeti hii imelenga kupunguza gharama za maisha ya wanachi kwa kuendelea na jitihada za kudhibiti na kupunguza mfumuko wa bei. Wananchi wengi wanaona kuwa gharama za maisha zinapanda kwa kasi ya juu kuliko takwimu zinazotolewa na serikali. 

         Takwimu za fahirisi ya bei zinaonyesha kuwa kati ya 2007 na 2012 bei zimeongezeka kwa  asilimia 70.5 lakini Hosehold Budget Survey ya mwaka 2012 ukilinganisha na ya 2007 zinaonyesha kuwa bei zimeongezeka zaidi ya mara 2. Gharama za maisha zinaongezeka kwa kasi kubwa na Watanzania wengi wanahisi kuwa serikali inawakejeli inapojigamba kuwa inadhibiti gharama za maisha.

Misamaha ya kodi

       Mwaka 2011/12 serikali ilipoteza mapato ya shilingi bilioni 1800 kwa sababu ya misamaha ya kodi. Mwaka 2013/14 mapato ya zaidi ya shilingi bilioni 2100 hayakuingia katika mfuko wa serikali kwa sababu ya misamaha ya kodi. Ninaunga mkono uamuzi wa Serikali kuwa na utaratibu wa kutoa tarifa ya misamaha ya kodi kila robo mwaka kwa kuwatangaza walionufaika na misamaha kwenye Tovuti ya Wizara ya Fedha. 

          Utaratibu huu ulianzishwa katika uongozi wa Rais Mkapa na Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete – wakati huo akiwa Waziri wa Mambo ya Nje, alikuwa miongoni mwa watu walioorodheshwa kunufaika na misamaha ya kodi baada ya kuingiza nchini magari ya kifahari. Serikali ya wawmu ya nne iliposhika hatamu za uongozi mwaka 2005 ilifuta utaratibu wa kuorodhesha, wananchi, kampuni na taasisi zilizosamehewa kodi. Kuweka wazi misamaha ya kodi kunaweza kusaidia kudhibiti misamaha ya kodi na kutawawezesha wananchi kuwa na taarifa za misamaha na kuweza kudai kwa sauti kubwa kufutwa kwa misamaha ya kodi

       Ili kujenga utamaduni wa kulipa kodi kuwa ni ishara ya uzalendo ni muhimu misamaha ya kodi ya viongozi wa serikali wakiwemo Wabunge, Mawaziri na Rais iondolewe. Ni vigumu kwa viongozi ambao hawalipi kodi kuwahamasisha wananchi kuwa Wazalendo na kulipa kodi.
Hatua ya Waziri kuondoa mamlaka yake ya kutoa misamaha ya kodi ni jambo jema.

Serikali inaandaa Muswada wa Sheria ya Bajeti na utakamilika kabla ya  mwisho wa mwaka 2014/15. Sheria hii inalenga kuongeza nidhamu ya matumizi na uwajibikaji kwa wadau wote wanaotekeleza Bajeti ya Serikali. Sheria hii ilipaswa kuandaliwa mapema katika uongozi wa Rais Kikwete. Ni vigumu kuwa na sheria nzuri ya bajeti katika mwaka wa mwisho wa uongozi wa Rais aliyeko madarakani ambayo kimsingi sheria hiyo itabidi itekelezwe na serikali inayokuja. Ili sheria nzuri ya bajeti itekelezwe ni muhimu kuacha utaratibu wa cash budget.

Utekelezaji wa miradi chini ya viwango.
Serikali imetambua tatizo la utekelezaji wa miradi chini ya viwango. Waziri ameeleza kuwa “Katika kuhakikihsa kuwa thamani ya fedha inawiana na uwekezaji katika miradi husika, Serikali imenunua vifaa vya kuhakiki ubora wa miradi ya maendeleo.” 

      Hata hivyo haikuelezwa utaratibu gani uliotumiwa kuamua kununua vifaa hivyo na taasisi gani itakayotumiwa kuhakiki ubora wa miundombinu. Miundombinu ni ya aina nyingi. Kuna barabara, bandari, majengo, mabomba ya maji, mabomba la gesi, mabwawa, mashine za aina mbalimbali. Vifaa gani vinavyoweza kuhakiki aina mbalimbali za miundombinu. Kuna tatizo la baadhi ya watendaji serikalini kuchangamkia ununuzi wa vifaa kwa mategemeo ya kupata commission kuliko malengo ya kuongeza ufanisi.

        Waziri kaeleza kuwa “Serikali imeamua kuzingatia ununuzi wa pamoja (bulk procurement) kutoka kwa wazalishaji badala ya wakala kama ilivyo sasa na hatua imeanza kuchukuliwa ili ununuzi wa mgari na vyombo vya TEHEMA ufuate utaratibu huo” Siku za nyuma serikali iliamua kununua mafuta ya petroli na dizeli kwa pamoja - bulk procurement, lakini Waziri hajaeleza utaratibu huu umefikia wapi na tumejifunza nini?

        Waziri amependekeza hatua nyingine ya kudhibiti matumizi ya umma kwa kuunganisha matumizi yote ya wizara, idara za Serikali zinazojitegemea, sekretarieti za mikoa, mamlaka za serikali za mitaa na wakala na taasisi za Serikali chini ya mfumo mmoja wa udhibiti wa fedha za Serikali unaosimamiwa na Mlipaji Mkuu wa Serikali. Utaratibu wa Single Treasury Account kusimamia matumizi ya serikali ni jambo zuri lakini linahitaji maandalizi ikiwa ni pamoja na kufunga akaunti nyingi zinazotumiwa na wizara, idara na asasi nyingine za serikali. Wizara na Idara nyingi zimeendelea kufungua akaunti mpya. Kuna wizara zinazopinga Hazina kusimamia ulipaji wa makandarasi wanaotekeleza miradi ya maendeleo. 

         Utekelezaji wa Treasury Single Account unahitaji kuungwa mkono kikamilifu na Rais. Hata ofisi ya Rais itumie utaratibu unaosimamiwa na Mlipaji Mkuu wa Serikali. Waziri ana uhakika wa kuwepo na utashi wa kisiasa wa kutekeleza utaratibu unaopendekezwa?

Bajeti ya 2013/14
Tatizo la msingi la bajeti ya 2013/14 ni kuwa makadirio ya mapato ya ndani na misaada na mikopo ya nje yalikuwa makubwa kuliko hali halisi ilivyojitokeza. Matumizi yote yalikadiriwa kuwa shilingi bilioni 1824.9. Lakini kwa sababu ya upungufu wa mapato matumizi yote yanatarajiwa kufikia shilingi bilioni 17097.7. Matumizi halisi ni kidogo kuliko bajeti kwa shilingi bilioni 1152.2 sawa na asilimia 6.3 ya bajeti iliyoidhinishwa na Bunge.

     Bunge liliidhinisha ukusanyaji wa mapato ya ndani ufikie shilingi bilioni 11154.1. Mpaka ifikapo Juni 30 2014 serikali inatarajia kukusanya shilingi bilioni 10098.7 ambazo ni shilingi bilioni 1055.4 sawa na asilimia 9.5 chini ya makadirio ya bajeti. Misaada na mikopo ya bajeti ilikadiriwa kuwa shilingi bilioni 11631.3 lakini serikali inatarajia kupata shilingi bilioni 988.7 ambazo ni shilingi bilioni 174.5 sawa na asilimia 15 chini ya bajeti. Serikali ilikadiria kupata shilingi bilioni 1796.9 kama misaada na mikopo ya miradi. Fedha ya misaada na mikopo ya miradi iliyopatikana kwa mwaka wa bajeti wa 2013/14  ni shilingi bilioni 922.3 ambazo ni shilingi bilioni 874.6 sawa na asilimia 48.7chini ya bajeti.

        Bajeti ya 2013/14 ilipanga kutumia shilingi bilioni 12574.9 kama matumizi ya kawaida. Matumizi halisi ya kawaida yanatarajiwa kuwa shilingi bilioni 12085.2 ambayo ni chini ya makadirio ya bajeti kwa shilingi bilioni 489.7 sawa na asilimia 3.9.

      Takwimu za jumla za bajeti ya kawaida hazioneshi picha halisi ya matatizo ya bajeti. Mfuko wa CFS ambao hutengewa fedha za kulipia madeni na matumizi ya pensheni na hifadhi ya jamii ulikadiriwa shilingi bilioni 3319.2 lakini matumizi halisi ya mfuko huu yalikuwa shilingi bilioni 4251.5 ambalo ni ongezeko la shilingi bilioni 932.4 sawa na asilimia 28.1 ya makadirio ya bajeti. Katika mfuko huu wa CFS fedha iliyotengwa kulipia madeni ilikuwa shilingi bilioni 2535.7 lakini fedha iliyotumiwa kulipia madeni ilikuwa shilingi bilioni 3223.1 ongezeko la shilingi bilioni 687.4 sawa na ongezeko la asilimia 27.1 ukilinganisha na bajeti. Madeni ya serikali yanayostahiki kulipwa hujulikani vizuri wakati bajeti inaandaliwa. 

        Hakuna ulipaji wa dharura wa madeni. Inakuwaje wakati matumizi mengine yanapunguzwa, ulipaji wa madeni unaongezeka kwa kiwango kikubwa kuliko makadirio ya bajeti. Mwaka wa fedha wa 2012/13 CFS ilitengewa shilingi bilioni 2735.9 lakini matumizi halisi yalikuwa shilingi bilioni 3341.7 sawa na asilimia 22.1 zaidi ya makadirio.

         Malipo mengine ya CFS yalikadiriwa kuwa shilingi bilioni 783.5 lakini serikali imetumia shiling bilioni 1028.5 ambalo ni ongezeko la shilingi bilioni 245 sawa na asilimia 31.3 ya makadirio ya bajeti. Sehemu kubwa ya matumizi mengine ya CFS ni malipo ya pensheni na mchango wa serikali katika mfuko wa hifadhi ya jamii ya wafanyakazi wa serikali ambayo makadirio ya bajeti yake yanapaswa kuwa ya uhakika. Ni vyema Mdhibitina mkaguzi wa serikali afanye ukaguzi maalum (special audit) wa mfuko wa CFS.

         Ulipaji wa mishahara ulikuwa mkubwa kuliko makadirio ya bajeti kwa shilingi bilioni 120 sawa na asilimia 2.5.
Matumizi mengine – Other Charges – ndiyo yaliyopunguzwa kwa kiasi kikubwa. Matumizi mengine ndiyo yanayogharamia vitendea kazi vya siku hadi siku katika wizara na idara za serikali. Ikiwa vitendea kazi hivyo havipo wafanyakazi wa serikali hawawezi kutimiza wajibu wao. Bajeti ya matumizi mengine ilikadiriwa kuwa shilingi bilioni 4109.1 lakini matumizi halisi yanatarajiwa kuwa shilingi bilioni 2682.1, upungufu wa shilingi bilioni 1427.1 sawa na asilimia 34.7 ya bajeti. 

      Wizara na idara zisizokuwa na nguvu za kisiasa zilitengewa fedha kidogo sana za Matumizi Mengine. Wafanyakazi wa serikali wanaenda kazini lakini hakuna kazi wanayoifanya kwa kukosa vitendea kazi, zahanati na hospitali hazina dawa, shule hazina vitabu na vifaa vingine vya kufundishia. Wanachi hawapati huduma za serikali.
Serikali ilikadiria shilingi 5674.0 kama bajeti ya maendeleo lakini fedha iliyotelewa ni shilingi bilioni 5011.6. Upungufu wa shilingi bilioni 662.5 sawa na asilimia 11.7 ya makadirio ya bajeti.

Bajeti ya Mandeleo inayoidhinishwa ni tofauti na bajeti halisi inayotekelezwa. Serikali bado haijatoa takwimu za bajeti halisi kwa kila wizara, idara na taasisi za serikali kwa 2013/14. Takwimu zilizopo ni za mwaka 2012/13. Mwaka wa bajeti wa 2012/13 Wizara ya Kilimo ilitengewa bajeti ya Maendeleo ya shilingi bilioni121.1 lakini fedha iliyopewa ilikuwa shilingi bilioni 67.1 sawa na asilimia 55.4 ya makadirio ya bajeti. Wizara ya elimu ilitengewa shilingi bilioni 92.6 kama bajeti ya maendeleo lakini ikapewa shilingi bilioni 59.5 sawa na asilimia 64.3 ya bajeti iliyoidhinishwa na Bunge.

Bajeti ya Maendeleo ya Wizara ya Maji ilikuwa shilingi bilioni 465.8 lakini ikapewa shilingi bilioni 229.3 sawa na asilimia 49.2. Wizara ya Afya ilitengewa shilingi bilioni 283.5 lakini ikapewa shillingi bilioni 220.2 sawa na asilimia 77.7. Wizara ya ardhi na Makazi ilitengewa shilingi bilioni 71 lakini ikapewa shilingi bilioni4 sawa na asilimia 5.6
Katika hali hii bajeti siyo mwongozo wa utekelezaji wa sera za serikali.

Bajeti ya 2014/15

Bajeti ya 2014/15 imekadiria kukusanya mapato na kutumia shilingi bilioni 19853.3 ukilinganisha na bajeti ya 2013/14 ya shilingi 18249.0 Matumizi halisi ya mwaka 2013/14 yanatarajiwa kuwa shilingi 17096.8 Ongezeko halisi la bajeti ya 2014/15 ni asilimia 16.1.

       Mapato ya ndani yanakadiriwa kuwa shilingi bilioni 12178.0. Mwaka 2013/14 serikali ilikadiria kukusanya shilingi 11154.1 lakini inatarajia kukusanya shilingi 10098.7. Je serikali hii itaweza mwaka huu kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa asilimia 20.6 ukilinganisha na ukusanyaji wa mwaka jana?

       Halmashauri zilikadiriwa kukusanya shilingi bilioni 383.5 mwaka 2013/14. Hata hivyo matarajio ni kuwa zitakusanya shilingi bilioni 268.4. Bajeti ya 2014/15 inakadiria Halmashauri zikusanye shilingi bilioni 458.5, ongezeko la asilimia 70.8 la mapato halisi ya 2013/14
Misaada na mikopo ya miradi ilikadiriwa kuchangia shilingi bilioni 1796.9 lakini zilizopatikana ni shilingi bilioni 922.3 tu. Hata hivyo serikali inakadiria kuwa mwaka 2014/15 misaada na mikopo ya miradi itakawa shilingi bilioni 1745.3 ongezeko la asilimia 89.2 ya fedha iliyopatikana mwaka 2013/14.

       Kwa uchambuzi wa takwimu hizi bajeti ya 2014/15 haitekelezeki kama ilivyokuwa kwa bajeti ya 20143/14. Huduma za serikali zilidorora sana kwa kukosa kupangiwa matumizi ya vitendea kazi zitaendelea kudorora kwani matumizi mengine yanakadiriwa kutengewa shilingi bilioni 2650.3 tu mwaka 2014/15 ukilinganisha na makadirio ya shilingi bilioni 4109.1 na matumizi halisi ya shilingi bilioni 2682.1.

      Bajeti ya serikali bado haitoi kipaumbele kwenye miradi ya maendeleo. Makadirio ya matumizi ya kawaida ni shilingi bilioni 13408.2 ambayo ni makubwa kuliko makadirio ya mapato ya ndani ambayo ni shilingi bilioni 12178.0. Kimsingi serikali haichangii bajeti ya maendeleo. Bajeti inayojikita kuchochea maendeleo mapato ya ndani yanakuwa makubwa kuliko matumizi ya kawaida na ziada inahamishiwa kwenye bajeti ya maendeleo. Bajeti ya maendeleo ya Tanzania inategemea misaada toka nje na mikopo ya ndani na nje.

Bajeti Mbadala ijikite katika ukusanyaji wa mapato makini na matumizi mazuri ya fedha za umma. Kwa kuondoa misamaha holela ya kodi tunaweza kukusanya asilimia 22-25 ya pato la taifa kama mapato ya serikali. Matumizi ya serikali yagawiwe kisekta kama ifuatavyo asilimia 25 elimu, asilimia 10 kilimo, asilimia 15 afya, asilimia 25 miundombinu, asilimia 25 ulinzi, usalama, utawala na mengine.

Watanzania tunahitaji tutafakari hali halisi tuliyonayo na tubuni sera na mikakati ya pamoja ya kujikwamua toka dimbwi la umaskini. Misingi muhimu ya sera na mikakati hiyo iwe:-

·        Kuitumia vizuri mali ya asili ya Tanzania kwa manufaa ya wananchi wote huku tukilinda mazingira yetu
·        Kuwekeza kwenye afya ya watoto wa Tanzania toka wakiwa katika mimba za mama zao kwa kuhakikisha kina mama waja wazito na watoto wachanga wanapata lishe bora
·        Kuwekeza katika elimu ya watoto wa Tanzania toka shule za chekechea na kuendelea. Kuweka msisitizo maalum katika elimu ya hesabu, sayansi na teknolojia
·        Kuwekeza katika kilimo hasa cha chakula kama vile mahindi, mpunga, maharage, jamii ya kunde na mbegu za mafuta kukidhi mahitaji ya ndani na kuuza masoko ya nje hasa nchi za jirani na hususan Congo
·        Kuwekeza katika miundombinu ya barabara, umeme, maji na mawasiliano
Kuweka mkakati madhubuti wa kuanzisha na kuendeleza viwanda vinavyotumia malighafi ya ndani na kuajiri watu wengi kama vile viwanda vya nguo na mavazi, viatu na bidhaa za ngozi, vifaa vya matumizi ya nyumbani na vifaa vya umeme na electroniki.

Serikali ya CCM haina utashi wa kisiasa ya kuandaa bajeti inayotekelezeka yenye maslahi ya mwananchi wa kawaida. Katika kipindi hiki kuelekea 2015 tuna wajibu wa kuandaa na kukamilisha mpango na bajeti inayotekelezeka itakayojenga misingi ya maendeleo ya kweli kwa wananchi wote.

Ibrahim Haruna Lipumba
Mwenyekiti wa CUF (Taifa)

15 JUNI, 2014




No comments: