Wednesday, September 24, 2014

HIKI NDICHO ALICHOKIFANYA BAKHRESA KWA WAANDISHI WA HABARI ZA MICHEZO TANZANIA LEO

Meneja Mkuu wa SSB, Sheikh Said Muhammad (kushoto) akikabidhi mfano wa hundi ya Sh. milioni 10 kwa Mwenyekiti wa TASWA, Juma Pinto (kulia). Wanaoshuhudia ni viongozi wengine wa TASWA kutoka kushoto Shijja Richard (Mweka Hazina), Amir Mhando (Katibu Mkuu) na Egbert Mkoko (Makamu Mwenyekiti).

KAMPUNI ya Said Salim Bakhresa Group Limited, leo imetoa kiasi cha Sh. Milioni 10 kwa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) kwa ajili ya tuzo za Wanamichezo Bora nchini, zilizopangwa kufanyika Desemba 12, mwaka huu.


  Akikabidhi fedha hizo, Meneja Mkuu wa SSB Limited, Sheikh Said Muhammad Said katika ukumbi wa City Sports Lounge, Mtaa wa Samora, Dar es Salaam, amesema kwamba wanatoa mchango huo ili kuwezesha zoezi hilo lifanikiwe.
“Kwanza nasema naomba nitoe shukrani zangu za dhati kwa niaba ya kampuni kwa TASWA kutufuata kutuomba tuchangie tuzo hizi. Sisi tupo mstari wa mbele katika kuunga mkono harakati zote za kimaendelea katika sekta ya michezo nchini,”amesema.Sheikh Said amesema kwamba SSB inajivunia kuwa sehemu ya shughuli hiyo na inawatakia kila la heri TASWA ili wafanikishe mchakato huo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TASWA, Juma Abbas Pinto amesema kwamba wanashukuru kwa mchango huo wa SSB, ambao unafungua mfuko wa fedha za kuendehea zoezi hilo unaohitaji Sh. Milioni 120.

“Tumejiwekea utaratibu kwamba baada ya kufanya mazungumzo na watu mbalimbali na kutukubalia kutusaidia zoezi hili, tutakuwa tunawatangaza mmoja baada ya mwingine na kiwango wanachotoa,”.
“Kwa leo tunaanza na SSB, lakini tutarajie kama si Jumapili basi Jumatatu tutakutana tena hapa hapa kwa ajili ya kumtangaza mdhamini mwingine,” amesema Pinto.
Katibu wa TASWA, Amir Mhando kwa upande wake amesema maandalizi yanaendelea vizuri na ameomba ushirikiano wa kutosha baina ya Waandishi wa Habari nchini, ili zoezi hilo lifane.
Tuzo za wanamichezo Bora nchini, mwaka jana zilishindwa kufanyika baada ya waliokuwa wadhamini wake, Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) kujitoa dakika za mwishoni.

No comments: