Monday, September 1, 2014

STORY NZIMA YA MGOMO WA WAFANYABIASHARA HAPA KARIAKOO IPO HAPA LIVE

Na Karoli Vinsent


      SIKU moja kupita baada ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kutoa onyo kwa wafanyabiashara juu ya uhakiki wa mashine za Kielektroniki EFDs, wafanyabiashara wa maduka Kariakoo wamegoma kufungua maduka  huku wakiishinikiza serikali kuwapunguzia kodi.


          Wafanyabiashara hao walifikia hatua hiyo, baada ya kupata taarifa kutoka TRA ya kwamba watafanyiwa ukaguzi endelevu na kuchukuliwa hatua za kisheria kwa wale watakaokutwa hawatumii mashine hizo na wale wanaohamasisha kuwarubuni wengine wasitumie mashine hizo.



      Wakizungumza na Mtandao huu jijini Dar es Salaam kwa nyakati tofauti, wafanyabiashara hao walipinga kuwa, hakuna mtu aliyewashawishi kufunga maduka yao, isipokuwa kutokana na kukatwa kodi kubwa inayowakosesha maslahi ndio imewafanya wafikie uamuzi huo.


      Nicco Saga, mmiliki wa duka la nguo, alisema wameamua kufanya hivyo lengo likiwa ni kukwepa kufanyiwa uhakiki wa TRA, ambapo tangu waanze kutumia mashine hizo wanaingiza hasara kutoka kana na kodi ya asilimia 18 wanayokatwa.


      “Kilio chetu tunataka punguzo la kodi, kwani kodi ikiwa kubwa faida inakuwa ndogo ndio maana mnaona hali hii…inaendelea, kama walivyosema ni zoezi endelevu na sisi tutafunga endelevu halafu tuone watatoa wapi kodi na nani atatumia mashine zao” alisema.


     Saga alitaja sababu nyingine za kufunga maduka hayo kwamba, suala la elimu bado limekuwa kigugumizi kwani asilimia kubwa ya wafanyabiashara hao hawajui kusoma wala kuandika, jambo linalowafanya wakimbie kufanyiwa uhakiki.


      Halima Bakary mjasiliamali katika eneo hilo, alisema kuwa, mfumo wa serikali katika utoaji kodi ni mkubwa sana, hali inayowafanya watumie njia nyingine za kujipatia kipato.


     “Sisi hatuijagoma kutumia mashine hizi, isipokuwa kodi ni kubwa mno mwisho wa siku faida hatuioni, ndio maana unaona tunatumia njia mbalimbali za kupata faida ikiwemo kugoma ili tufikie muhafaka” alisema.


       Priscus Tarimo ambaye ni kibarua anayejishughulisha katika maeneo hayo, alisema kuna baadhi ya wamiliki wa maduka hayo wamekuwa wakikwepa kodi kwa kutotumia mashine hizo na wengine wanaendelea kutumia stakabadhi za zamani ambazo teyari zimepigwa marufuku.


        “Nimeathirika sana, maana kwa siku naingiza 10000, lakini nimekuja nimekuta tajiri wangu kafunga duka wakati mashine anayo, hivyo nashindwa kufahamu sababu iliyomfanya achukue uhamuzi huo hali ya kuwa ameinunua kihalali” alisema.


         Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi, Richard Kayombo, alisema kuwa, kwasasa wafanyabiashara hao hawana pakukimbilia kwani sababu wanazozitoa hazina tija ya kuwafanya wasitumie mashine hizo.


     “Hakuna sababu za kueleweka juu ya mgomo wao, tuliwaita tuak

awafundisha matumizi ya mashine hizo, lakini cha kushangaza bado wanaendelea kukaidi agizo tulilokubaliana, pia tuliwaita ili wazungumze na waandishi wa habari wakagoma sasa wanataka serikali iwafanyie nini” alihoji Kayombo.


        Alisema, kutokana na mgomo huo kuna athari za kiuchumi zinazoweza kujitokeza kwa upande wao kama kujijkoshesha kipato cha kila siku, hali ya kuwa wengi wao wanaishi kwa mikopo, pia wanapoteza wateja wao  kutoka maeneo ya mbalimbali.


      “Hili zoezi litakuwa endelevu wasijidanye kwamba tutawaonea huruma kwa udanganyifu wanaoufanya, kwanza kuna wengine wanatumia mashine bandia, wengine hawana kabisa na wengine wanazitumia pale wanapofanyiwa ukaguzi jambo ambalo sio sahihi” alisisitiza Kayombo.


       Aliongeza kuwa, katika operesheni iliyofanyika jijini Dar es Salaam, maduka 70 yalibainika hayatumii stskabadhi na kati yao 11 yamefungiwa kabisa.


      “Hili zoezi lina nia nzuri kwa wafanyabiashara kwa kurahisisha utunzaji wa kumbukumbu, hivyo kupunguza au kuondoa misuguano wakati wa ukokotoaji wa kodi na kuleta uwazi bila ya mtu yoyote kuonewa”.


       Pia alitoa wito kwa wananchi kuwa makini na kudai stakabadhi sahihi kwa kiwango cha fedha walichotoa kila wanunuapo bidhaa.

No comments: