Monday, October 13, 2014

BADO MTOTO WA KIKE TANZANIA HAYUPO SALAMA IMEELEZWA

Mwenyekiti wa mtandao wa kupinga ndoa za utotoni TCEMN  ambaye pia ni mkurugenzi mtendaji wa KIWOHEDE JUSTA MWAITUKA akizungumza wakati akitoa tamko la mtandao huo juu ya siku ya mtoto wa kike ambayo imeadhimishwa leo ndani ya ofisi za KIWOHEDE Jijini Dar es salaam
Pamoja na jitihada zinazofanywa na serikali  na mashirika yasiyo ya kiserikali kuhakikisha kuwa haki za mtoto wa kike  zinalindwa imeelezwa kuwa bado nchini Tanzania mtoto wa kike amekuwa akikabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo kukosa fursa ya kupata elimu sawa na wanaume,kubaguliwa katika ngazi ya familia,pamoja na tatizo la ndoa za utotoni ambalo limeonekana kuendelea kukua miongoni mwa jamii za kitanzania.

       Hayo yamesemwa leo jijini dare s salaam na mkurugenzi mtendaji wa  KIWOHEDE ambaye pia ni mwenyekiti wa mtandao wa mashirika ya  kupinga ndoa za utotoni  (TCEMN) Bi JUSTA MWAITUKA wakati maadhimisho ya siku ya mtoto wa kike yaliyoadhimishwa na mashirika hayo,ambapo amesema kuwa inasikitisha sana kuona bado ndani ya jamii za Tanzania bado kuna watu wanaamini kuwa mtoto wa kike hana haki ya kupata elimu sawa na mwanaume jambo ambalo amesema kuwa linahitaji kupigwa vita kwa nguvu kwani ni mila potofu nay a kuwagandamiza watoto wa kike.

Picha tatu zikionyesha watoto wa KOWOHEDE wakiwa katika shamra shamra za kuwahamasisha watanzania kuacha kumkandamiza mtoto wa kike na badala yake kumlinda,kumtunza na kuhakikisha kuwa wanampa haki zote za msingi kama mtoto wa kike




Amesema kuwa kwa mujibu wa shirika la UNICEF takriban watoto wa kike 8000 hapa Tanzania kwa mwaka hukatisha masomo yao kwa sababu za ujauzito huku idadi kubwa pia ya watoto wa kike wakishindwa kuendelezwa na elimu baada ya ile ya msingi na kujikuta wanaingia katika ndoa za umri mdogo.

     Bi MWAITUKA anasema kuwa pamoja na changamoto hiyo kumekuwa na tatizo la watoto wa kike wengi kusafirishwa kutoka vijijini kuja mijini kwa ahadi kuwa wanakuja kupatiwa ajira na wengine elimu na mwisho wake huishia kufanyishwa kazi za ndani bila malipo na  kuteseka hali inayowafanya wengi kuanza kukaa mitaani na baadae kujiingiza katika mambo machafu kama biashara ya ngono na utapeli.

          Aidha anaongeza kuwa changamoto nyingine inayowakumba watoto wa kike Tanzania ni swala la ukeketaji ambapo pamoja na kelele nyingi zinazopigwa na mashirika mbalimbali na serikali bado takwimu zinaonyesha tatizo la ukeketaji nchini ni kubwa ambapo kwa mujibu wa takwimu za viashiria vya idadi ya watu na afya 2010,asilimia 14.6 ya wanawake nchini Tanzania wamekeketwa na wengi wao ni watoto wa kike.
Utafiti unaonyesha kuwa mbinu mpya ya ukeketeji imeibuliwa ambapo watoto hukeketwa mara tu wanapozaliwa huku report ya mwaka 2013 ya haki za binadamu inayotolewa na kituo cha sheria na haki za binadamu ikionyesha ongezeko la kila mwaka la matukio ya ukatili kwa watoto hasa watoto wa kike.

            Kufwatia hali hii mtandao wa mashirika yanayopinga ndoa za utotoni (TCEMN)  wameitaka serikali kuhakikisha kuwa sheria zilizopo zinasimamiwa na zinatekelezwa pale zinapovunjwa kwa kuweka mifumo iliyo wazo na rahisi ya kupata na kufwatilia haki vile vile kubadilisha sheria ambazo bado zimekuwa ni kandamizi kwa motto wa kike hasa ukizingatia kuwa Tanzania ipo katika kipindi cha uandishi wa katiba mpya.

Mkurugenzi mtendaji wa kituo cha sheria na haki za binadamu LHRC naye pia alikuwepo kama washiriki wakubwa wa kulinda haki za watoto wa kike ambapo na yeye alisisitiza kuhakikisha wahusika kuhakikisha wanakaa katika nafasi yao katika kumtetea mtoto wa kike ili apate haki zake 
Aidha wameitaka jamii kuwajibika katika kuwalinda watoto wa kike dhidi ya vitendo vyote vya ukatili ikiwa ni pamoja na kuthamini nafasi ya kila mtoto na kuona mtoto wa mwezako ni wako na kutoa taarifa pale unapoona kuwa kuna mtoto wa kike ananyimwa haki yake ya msingi.


      Siku ya mtoto wa kike duniani imeadhimishwa leo jijini Dar es salaam na mtandao unaopinga ndoa za utotoni (TCEMN)  ambao unaundwa na mashirika zaidi ya 35 mtandao ambao ulianzishwa mwaka 2012 kwa lengo kukuza uelewa juu ya haki za motto wa kike na umuhimu wa kupewa fursa zaidi. 

No comments: