Tuesday, October 28, 2014

HIVI NDIVYO MSANII CHID BENZ ALIVYOPANDISHWA KIZIMBANI KWA KOSA LA KUDAKWA NA UNGA

 Msanii wa Hip Hop, Rshid Makwiro ‘Chidi Benzi’ akisindikizwa na askari Polisi wakati akiingia katika chumba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini leo Dar es Salaam kujibu mashtaka matatu likiwemo la kukutwa na dawa za kulevya kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam. (Picha na Francis Dande)

MSANII
wa Muziki wa Kizazi Kipya (bongo fleva), Rashidi Abdallah Makwaro (29),
maarufa kama Chid Benz, amefikishwa mahakamani akikabiliwa na mashitaka
matatu ikiwemo kukutwa na Dawa za kulevya aina ya Heroin yenye thamani
ya Sh. 38,638, bangi ya Sh. 1,720 na vifaa ya kuvutia dawa hizo kijiko
na kigae.

Chid Benz amefikishwa  mapema leo
saa 3:00 asubuhi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es
Salaam kwa ajili ya kusomewa mashitaka yake. Saa 7:50 mchana alifikishwa
mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Warialwande Lema aliyepangiwa kusikiliza
kesi hiyo.


Hata
hivyo, hakimu aliamuru msanii huyo kutolewa nje ili akave vizuri nguo
baada ya suruali aliyokuwa amevaa mlegezo maarufu kama kata kei
kuonyesha nguo yake ya ndani.


“Kwanza mtoeni nje aende akavae nguo hizo zinazodondoka…” aliamuru Hakimu.

Saa
7:54 alirejeshwa ndani ya chumba cha mahakama upande wa Jamhuri
ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mwanaamina Kombakono akisaidiana na
Inspekta Jackson Chidunda, ulimsomea mashitaka yake.


Wakili
Kombakono alidai kuwa Oktoba 24, mwaka huu katika uwanja wa Ndege wa
Julius Nyerere, uliopo Ilala jijini Dar es Salaam, mshtakiwa alikutwa
dawa za kulevya aina ya heroin isivyo halali zenye uzito wa gramu 0.85.


Katika shitaka la pili, ilidaiwa kuwa siku na eneo la tukio la kwanza, mshtakiwa alikutwa na gramu 1.72 za bangi isivyo halali.

Wakili
huyo wa serikali alidai kuwa, siku na eneo la tukio la kwanza na la
pili, mshtakiwa alikutwa akiwa na vifaa vinavyotumika kuvua dawa za
kulevya aina ya heroin, kigae na kijiko huku akijua ni kosa.


Mshtakiwa alikana mashitaka yote na upande wa Jamhuri ulidai kuwa hauna pingamizi na dhamana dhidi ya mshtakiwa.

Hakimu
Lema alisema mshtakiwa atakuwa nje kwa dhamana kwa masharti ya kuwa na
wadhamini wawili wanaotoka kwenye taasisi zinazoamini na siyo walimu na
dhamana ya Sh. Milioni moja.


Hata hivyo, mshtakiwa alishindwa kutimiza masharti hayo na amepelekwa mahabusu hadi Novemba 11, kesi hiyo itakapotajwa.

No comments: