Sunday, November 16, 2014

BUNDI WA MIGOGORO ALIYETUA CHAMA KIPYA CHA ACT ATOWEKA KIAINA.MWENYEKITI ASEMA HALI NI SHWARI

Mwenyekiti wa chama hicho ndugu LUCAS LIMBU KADAWI akizungumzaa na wanahabari muda huu jijini Dar es salaam
          Mgogoro uliokuwa unafukuta ndani ya chama kipya kabisa katika siasa  za Tanzania chama cha ACT mgogoro uliopelekea baadhi ya wanaojiita waasisi wa chama hicho kutangaza kumtimua katibu mkuu wa chama hicho SAMSON MWIGAMBA umezimwa kiaina na uongozi  wa chama hicho baaada ya kukutana na upande wa walioanzisha mgogoro huo.

        Akizungumza na wanahabari muda huu makao makuu ya ACT jijini Dar es salaam mwenyekiti wa chama hicho ndugu LUCAS LIMBU KADAWI amesema kuwa chama hicho kimekutana na wanachama wawili ambao ndio waliotangaza kumtimua katibu mkuu ambao ni bwana GREYSON NYAKARUNGU na LEOPARD MAHONA na kuwasikilia malalamiko yao ambapo mwisho wakafikia muafaka wa kupatana na kuendelea kukijenga chama.

Bwana KADAWI amesema kuwa swala hilo limekwisha na hakuna mgogoro tena ndani ya chama chao na wanaendelea kukijenga chama chao huku akiwataka wanachama wa chama hicho kuondoa mashaka na chama hicho na badala yake waendelee kukiamini.

Mapema wiki iliyopita watu wawili ambao wamejivisha joho la uasisi wa chama walijitokeza mbele ya wanahabari na kudai kuchoshwa na mambo anayoyafaya katibu mkuu wa chama hicho ndugu SAMSON MWIGAMBA kwa kile walichoita ni kwenda kinyume na makubaliano wakati wa kuanzisha chama hicho ambapo walitangaza kumfukuza katibu huyo huku wakitoa onyo kali kwa viongozi wengine wakuu wa chama hicho.
Kushoto kabisa ni GREYSON NYAKARUNGU na kulia kabisa ni LEOPARD MAHONA ambao ndio waliotangaza kumfukuza katibu mkuu wa chama hicho ambapo leo wamerejea na kuungana na viongozi hao wa chama hicho na kuumaliza mgogoro huo
 TAMKO NZIMA LIPO CHINI HAPO


TAARIFA KWA UMMA KUHUSU ‘KUTIMULIWA’ KWA KATIBU MKUU WA ACT-TANZANIA
  1. Mnamo tarehe 11 Novemba 2014 kuliripotiwa na vyombo vya habari kwamba Katibu Mkuu wa ACT-Tanzania Ndugu Samson Mwigamba alikuwa ‘ametimuliwa’ katika nafasi yake na vijana waliojiita waasisi wa chama, ambao ni Ndugu Greyson Nyakarungu na Ndugu Leopold Mahona. Tunakiri kwamba Ndugu Greyson Nyakarungu na Ndugu Leopold Mahona ni wajumbe katika Kamati ya muda ya Uongozi ya chama. Ndugu Leopold Mahona ni Naibu Katibu Mkuu (Bara) wakati Ndugu Greyson Nyakarungu ni Mjumbe wa Kamati.
  2. Kwa utamaduni wa chama cha ACT-Tanzania, tangazo la vijana hawa lilichukuliwa kama kiashiria cha tatizo linalohitaji kutatuliwa, na ambalo lilielekea kuchafua hali ya kisiasa na amani ndani ya chama. Kwa sababu hiyo, Kamati ya Uongozi ilikutana kwa muda wa siku mbili Jijini Dar es Salaam na kujadili kwa kina dukuduku walizokuwa nazo Ndugu Mahona na Ndugu Nyakarungu.
  3. Kwa kuwa chama chetu kinaamini katika uhuru kamili wa maoni ambayo yanaweza kutolewa kwa njia mbalimbali ikiwemo mikutano na waandishi wa habari, Kamati ya Uongozi ilipokea taarifa iliyosambazwa katika vyombo vya habari na Ndugu Nyakarungu na Ndugu Mahona kwa tahadhari kubwa katika kulinda misingi ya chama na haki ya viongozi na wanachama kutoa maoni yao chanya na hasi kwa uwazi.
  4. Baada ya majadiliano marefu na tafakuri ya kina, viongozi tumekubaliana:
    1. kujenga utamaduni wa kuwasiliana mara kwa mara na tabia ya kutoa dukuduku zetu ndani ya vikao vya chama
    2. Pale ambapo ni muhimu kutumia vyombo vya habari kutoa dukuduku zetu kuhusu mwenendo wa viongozi wenzetu ni vizuri kufanya hivyo katika namna ambayo italinda misingi ya chama na kuendeleza udugu, umoja na amani ndani ya chama chetu na jamii kwa ujumla.
  5. Tunatoa wito kwa viongozi wetu na wanachama kwa ujumla kuendelea na maandalizi ya uchaguzi wa serikali za mitaa. Tunawakikishia kwamba viongozi wenu wote katika ngazi ya kitaifa tupo pamoja na tunaendelea kuchapa kazi kama kawaida.
Kadawi Lucas Limbu, Mwenyekiti wa Taifa.


No comments: