Saturday, November 22, 2014

MADUDU MENGINE HAYA HAPA--MWAKYEMBE SASA KITANZINI AHUSISHWA NA UFISADI HUU,SOMA HAPA



*Wajiandaa kuuza haki za kuiendesha kwa bei ya kutupa
*Wathamanisha ardhi, maji Sh milioni 246 kwa miaka 33
*Thamani halisi ni Sh bilioni 85, ni mkataba hatari kwa usalama
*Mwekezaji anapewa ‘bure’, TPA kukopa mtaji Sh bilioni 306
*Dk. Mwakyembe ahusishwa, Kigogo adaiwa kuhongwa bilioni 1

Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imeingia katika kashfa nyingine nzito kutokana na mpango wake wa siri inaoukamilisha wa kubinafsisha mlango wa Bandari ya Dar es Salaam katika eneo liitwalo Gerezani Creek kwa miaka 33 kuanzia mwaka huu.

Mpango huo unaosukwa kwa siri kubwa chini ya mkataba unaopendekezwa; imebainika kuwa kisheria ni mbovu, hauna maslahi kwa taifa na unahatarisha usalama wa Tanzania.

Mkataba huo ulipaswa kutiwa saini Septemba 6, mwaka huu, lakini inaelezwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Joseph Simbakalia, ambaye ni Mjumbe wa Bodi ya TPA, ameukataa.

lilipowasiliana na Simbakalia, alisema: "Ahaaaa, ahaaaa ahaaa, bwana, hayo mambo ya Bandari sitaki kuyazungumzia, ongea na Mwenyekiti au Kaimu Mkurugenzi wa Bandari. Sitaki swali zaidi." Akakata simu.


pichani niKaimu mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA),Mzee Maden Kipande



Inaelezwa kuwa Simbakalia aliwashawishi wajumbe wengine wa Bodi waukatae mkataba huo kutokana na ubovu wake. Mkataba husika uliandaliwa kwa siri jijini Geneva, Uswisi na baadhi ya vikao kufanyika Nairobi nchini Kenya, kisha ukaletwa nchini kwa nia ya kutiwa saini bila kubadilishwa kwa njia yoyote.

Eneo ‘linalogawiwa’ kwa Mzungu mwekezaji, ni pamoja na Bandari ilikojenga jengo jipya la ghorofa 35, ingawa wengine wanasema mchoro wa awali umebadilishwa na sasa litakuwa na ghorofa 40.

Mpango ulivyosukwa
Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, inadaiwa kwa kushikiana na Kaimu Mkurugenzi wa Bandari, Mzee Madeni Kipande, walianzisha kwa siri mchakato wa kubinafsisha mlango wa Bandari ya Dar es Salaam, kuanzia eneo zinakotia nanga ‘boti za kasi’ ziendazo Zanzibar hadi eneo yanakopakuliwa magari kutoka ng’ambo.
Habari za uchunguzi zinaonesha kuwa kampuni inayodaiwa kuwa inataka kubinafsishiwa eneo hili la Bandari kwa miaka 33 imesajiliwa miezi michache iliyopita na hadi Jumamosi Oktoba 18, mwaka huu kampuni hii ilikuwa haijaingizwa kwenye orodha iliyopo kwenye tovuti ya Msajili wa Kampuni (Brela).

Mkataba unaitaja kampuni ya Impala Terminals Tanzania Limited kuwa inamilikiwa na Kampuni ya Vullstar Limited ya Bahamas, lakini uchunguzi uliofanywa na Chanzo chetu, kampuni ya Vullstar haina wavuti na wala haionekani kwenye mtandao wowote.
Visiwa vya Bahamas vinasifika duniani kwa kuwa na kampuni feki, na hivi karibuni vilikuwa na kashfa ya kuwa na nyumba moja inayoonekana kuwa ni ofisi ya kampuni zaidi ya 3,000; nyumba hiyo ikiwa na vyumba visivyozidi sita.

Ukiacha utata wa kampuni mpya ya Impala kumilikiwa na Kampuni ya Vullstar isiyokuwapo kwenye mtandao wa intaneti, kampuni ya Impala Terminals Tanzania Limited anwani ya msingi inayoitumia hapa nchini ni ya simu ya mkononi ya airtel (namba inahifadhiwa), ambayo inapokewa na mtu asiyejitambulisha kwa jina ila ndiye ametajwa kama Mkurugenzi wa kampuni hiyo kwenye mkataba unaokusudiwa kusainiwa.

Alhamisi (Oktoba 16, 2014) Chanzo hicho kilipowasiliana na Mkurugenzi huyo, asiyetajwa jina ila yupo kwenye mkataba ambao Bandari inapaswa kukopa dola milioni 180 (Sh bilioni 306) kuendesha mradi huu, alihoji: "Umeupata wapi mkataba huu? Huu ni mkataba wa siri, uniambie aliyekupa mkataba huu ndipo nikujibu." Mwandishi alipomwambia kuwa taaluma hairuhusu kutaja majina ya waliompa mkataba, Mkurugenzi huyo akasema: "Andika maswali unitumie kwenye barua pepe."

Mwandishi alimsomea anwani za barua pepe zilizoko kwenye mkataba, naye akakiri kuwa ndizo; na akataka maswali yatumwe kupitia barua pepe hizo.
Mwandishi aliandika maswali 11 na kumpelekea barua pepe mbili zilizopo kwenye mkataba, ambazo nazo ni za kampuni nyingine iitwayo Impala Terminals, na badala ya maswali kujibiwa; huyo Mkurugenzi mwenye namba ya airtel, Ijumaa Chanz chetu haijaapata majibu kutoka kwa mtu mwingine kabisa aliyeko Geneva, Uswisi akisema:
"Mpendwa Bwana Balile, asante kwa maswali yako kwa Impala. [Huwa] hatuzungumzii uvumi au hisia. Salaam za upendo, Victoria Dix."

Huyu Victoria Dix kwa mujibu wa mtandao wa www.impalaterminals.com ni Mkuu wa Idara ya Uhusiano upande wa mashirika wa kampuni ambayo ina makao yake Geneva, Uswisi.

Mkataba unachotaka
Mkataba huo wenye shinikizo kubwa kutoka kwa kigogo mmoja ndani ya Wizara ya Uchukuzi, ambaye inadaiwa amehongwa dola 800,000 za Marekani (Sh bilioni 1.36) akamalizia ununuzi wa kiwanja kutoka kwa Mjerumani mmoja karibu na eneo la Bahari Beach Hotel, Dar es Salaam; unatajwa kuwa utahatarisha usalama wa taifa.

Masharti inayotoa kampuni ya Impala Terminals Tanzania Limited, ni kuwa lazima Bandari ikubali kuingia ubia na kampuni hiyo kwa kuunda kampuni ya pamoja inayotajwa kwa Kiingereza na lugha ya kisheria kama Joint Venture Company (JVC), ambayo kwa sasa haijasajiliwa kwa nia ya kuendesha Bandari chini ya Ushirikiano wa Serikali na Sekta Binafsi (PPP).

Mtaji wa vitabuni, inaelezwa kuwa kampuni itakayoundwa itakuwa na mtaji wa vitabuni wenye thamani ya dola milioni 27 za Marekani utakaogawanywa katika hisa 10,000 kwa maana kuwa kila hisa itakuwa na thamani ya dola 2.7.

Kampuni ya Impala Terminals Tanzania limited inajinadi kuwa itabuni, itaendeleza, itatoa mtaji na kuendesha Bandari ya Dar es Salaam kwa kujenga gati mbili katika eneo la Gerezani Creek, ila wanatumia ujanja kwa kudai kuwa ni uwekezaji wa pamoja na TPA.

Mbali na ujenzi wa gati mbili, kampuni ya Impala inajinadi kuwa itatoa ajira kwa Watanzania na kuleta nchini ujuzi wa uendeshaji bora wa bandari. Hata hivyo, kati ya maswali waliyoulizwa na kukataa kuyajibu ni pamoja na ukweli kwamba kampuni hii au Vullstar inaelezwa kuwa haijawahi kuendesha bandari yoyote duniani na hivyo haina uwezo inaotamba kuwa nao.

Kampuni nyingine wanayotumia anwani ya barua pepe zake, impalaterminals.com, kwenye mtandao inajinadi kuwa inao uzoefu mkubwa katika sehemu mbalimbali duniani wa kutuza maghala (warehouses) na si kuendesha bandari. JAMHURI haikuweza kufahamu uhusiano uliopo kati ya Impala Terminals, Vullstar na Impala Terminals Tanzania Limited.

Wakati mkataba huo unaizuia Bandari kuhamishia hisa zake kwa mwekezaji mwingine wakati wote wa uhai wa mkataba, yaani miaka 33; Impala wao wanaruhusiwa kuhamisha hisa zao kwenda kampuni ya Vullstar bila kulazimika kuomba ruhusa kwa TPA.

Gharama ya mradi
Gharama ya mradi atakaopewa mwekezaji huyu chini ya mkataba ni dola milioni180 za Marekani. Hata hivyo, mkataba huu umeandikwa kwa ujanja wa hali ya juu. Kifungu cha 5.2.1 cha mkataba kinahamishia jukumu la kukopa mtaji kwa TPA na si kwa mwekezaji kama ilivyoelezwa awali.

Kifungu hiki kinasema: "Bandari ina wajibu wa kutoa asilimia 30 ya hisa kama mchango wake wa ardhi na matumizi ya maji na mkopo wote wa wanahisa unaohitajika kwa ajili ya kampuni (JVC) ambao si zaidi ya Mtaji wa Kuanzishia Mradi (dola milioni 180) na inaweza pia kulipia hisa asilimia 19 kwa njia ya fedha kama mchango wake kwa JVC."

Kifungu cha 5.1.1 kinasema Impala Tanzania Terminals Limited yenyewe itamiliki hisa asilimia 51 na wanatumia maneno kuwa itatafuta mkopo kwa ajili ya hisa hizo na nyingine kadri itakavyohitajika. Maana yake ni kwamba Impala haitawekeza kitu na bado itamiliki asilimia 51 ya hisa kwenye kampuni hii kwani Mtaji wa Kuanzia ambao ni dola milioni 180 za Marekani umetajwa wazi kuwa utakopwa na TPA.

Thamani ya hisa na ardhi
Maajabu mengine katika mkataba huo, thamani ya hisa zinazopendekezwa kumilikiwa na Bandari bei yake iko chini ukilinganisha na zinazopendekezwa kumilikiwa na Impala.
Bandari wanatajwa kuwa watapewa ‘bure’ asilimia 30 ya hisa; sawa na hisa 55 kama mchango wao wa haki ya kumiliki ardhi na maji ilipo Bandari ya Dar es Salaam, kisha watapaswa kulipia hisa 36 kwa gharama ya dola 95,000 za Marekani kwa hisa zitakazotolewa na JVC. Wao impala watachukua hisa 94 kwenye JVC kwa gharama ya dola 255,000 za Marekani.

Sambamba na malipo hayo, Bandari pia watapaswa kutoa mkopo wa dola 855,000 za Marekani huku Impala mkataba ukiwataka watoe mkopo wa dola 2,295,000 za Marekani kwa nia ya kuijengea uwezo wa kifedha kampuni itakayoundwa.

Maajabu yanayotokea ni kuwa hisa zilizotolewa kwa Bandari thamani yake inakuwa dola 2,638.88 za Marekani kwa kila hisa, wakati hisa zilizotolewa kwa Impala thamani yake ni dola 2,684.21 za Marekani kwa kila hisa. Utofauti huu wa thamani ya hisa haukuelezwa umetokana na nini. Kwa mantiki hiyo, asilimia 30 ya hisa zilizotolewa kwa Bandari kwa njia ya ardhi ina maana ardhi hiyo imethamanishwa kuwa ni dola 145,000 (Sh milioni 246).

Suala la ardhi ndio kilio cha wataalam. Vyanzo vya kuaminika kutoka Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi, vimeliambia JAMHURI kuwa thamani ya eneo la Bandari wanalopanga kubinafsisha ni zaidi ya dola milioni 50 za Marekani (Sh bilioni 85), hivyo kulitoa kwa thamani ya Sh milioni 246 ni kuhujumu uchumi wa nchi.

Impala yatoa masharti magumu
Pamoja na kwamba haijasaini mkataba huu, Impala imetoa masharti magumu kwa Serikali. Kupitia mkataba huu inajipa mamlaka ya kuchunguza uwezo wa TPA kifedha na haki zote zilizopata kutolewa kupitia mikataba mingine, na kupitia Kifungu cha 3 chote hakuna mahala ambako Bandari inapaswa kuichunguza Impala kuona kama inao uwezo kifedha.

Kampuni hii inataka kukagua masharti ya usafirishaji kati ya Bandari na TAZARA. Pia TPA inapaswa kuikabidhi Impala nyaraka zilizotolewa na mamlaka halali zikiisamehe kodi Impala. Inaitaka Bodi ya Wakurugenzi ya TPA kukasimisha madaraka yake kwa Impala kwa maandishi juu ya uendeshaji wa Bandari kwa miaka yote 33 kuwa haitaingilia utendaji wake wakati wowote.

Mkataba unataka Waziri wa Fedha akabidhi barua ya kujifunga kuwa atahakikisha mkataba kati ya TPA na Impala unatelekezwa bila kubadilishwa kwa kipindi chote cha miaka 33 na TPA kuikabidhi barua ya kuthibitisha kuwa Bandari haitabadilisha matumizi ya ardhi au kuingia mkataba na mwendeshaji mwingine kwa muda wote wa miaka 33 ya mkataba.

Masharti magumu yanahitimishwa kwa kifungu cha 3.5 chenye kusema kuwa ikiwa TPA itashindwa kutimiza masharti hayo ndani ya miezi mitatu tangu siku ya kusainiwa kwa mkataba, basi mkataba utakuwa umevunjika. Ingawa kwenye eneo hili wanasema hakuna atakayedaiwa gharama za kuvunjwa kwa mkataba, kiujanja chini ya kifungu cha 22.1.1 kinaelekeza TPA idaiwe.

Kifungu hiki na kinachofuata cha 22.1.2 vyote vinasema ikiwa mkataba huu utavunjika iwe makosa yamefanywa na Impala au Bandari, basi TPA ndiye atakayelipa gharama za kuvunjika kwa mkataba huu kwa Impala. Mbaya zaidi, mkataba unasema ikiwa Bandari itashindwa kulipa, basi Serikali ndio itapaswa kulipa deni husika au mali za Serikali zitakamatwa kokote duniani.

Kundoshwa kwa mamlaka ya dola (waver of sovereignty immunity)
Mkataba unapendekeza chini ya Kifungu cha 34 kwa tafsiri isiyo rasimu unasema: "[Bandari] inaridhia kwa ujumla suala lolote kuhusu mashitaka au nafuu inayotolewa [kwa Impala] dhidi yake [TPA] kwa njia ya zuio au amri ya kutekeleza jambo maalum au kupata kitu chochote kiwacho na mali zake kuwa wazi kwa ajili ya utekelezaji wa amri au hukumu au mchakato unaoendeshwa kuhusu mali yoyote [ya TPA au Serikali].

"Kinga inaondolewa kwa ujumla wake bila haki ya kuirejesha dhidi ya mashitaka na mwenendo wake na utekelezaji au kukamata mali (ikiwa ni pamoja na hukumu za awali na ukamataji kwa msaada) ambako kuanzia sasa haki hii inaweza kurejeshwa tu kwa mujibu wa sheria za mamlaka yoyote na inatamkwa kwamba kundolewa kwa kinga ya mashitaka kutatekelezwa kwa kiwango kinachoruhusiwa na sheria."

Kuna taratibu za kisheria mtu au taasisi yoyote inapotaka kuishitaki Serikali, lakini kwa mkataba huu, Impala inataka Serikali iwe wazi kushitakiwa wakati wowote itakapojisikia kufanya hivyo bila kuomba kibali chochote. Kwa sasa kuishitaki Serikali inapaswa kutolewa notisi ya siku 90, kitu wasichokitaka Impala.

Nafasi ya Watanzania
Katika mkataba huo, Watanzania wanapewa kazi za ukiranja. Mkataba unapendekeza Bodi ya Wakurugenzi Watano, na Impala ambaye hakukopa mtaji ndiye awe na Wakurugenzi watatu, huku Bandari waliokopa mtaji na kutoa haki ya kutumia ardhi na maji wakitakiwa kuwa na wakurugenzi wawili kwenye Bodi hiyo.

Katika nafasi za utendaji, inapendekezwa Afisa Mtendaji Mkuu atoke kwa Impala, Afisa Fedha Mkuu atoke Impala na Afisa Uendeshaji Mkuu naye atoke Impala. Kwa upande wa Tanzania inapendekezwa Mtanzania awe Naibu Mtendaji Mkuu (anayeshughulikia uhusiano) na mwingine awe Afisa Utumishi na Rasilimali Watu.
Mkataba huu unaopendekezwa una upungufu mkubwa, likiwamo pendekezo kwamba mbia atakayeshindwa kulipia hisa, zilipiwe na mwenzake na hivyo kuhamisha umiliki wa hisa kama ilivyotokea kwa Benki ya NBC ambako mwekezaji sasa anaimiliki karibu kwa asilimia 100.

Mwakyembe, Kipande wakaa kimya
Waziri wa Uchukuzi, Dk. Mwakyembe pamoja na kupelekewa maswali ofisini kwake na kupelekewa ujumbe wa simu ya mkononi, hakujibu.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Madeni Kipande amegoma kuruhusu mwandishi kuingia ofisini kwake na hata alipopigiwa simu hakupokea, lakini alipotumiwa ujumbe mfupi wa simu akajibu kwa kusema: "Tutawasiliana baada ya kesi kukamilika."

Mwaka huu, Kipande alilifungulia JAMHURI kesi Mahakama Kuu ya Tanzania na kupata hukumu ya awali inayolizuia gazeti hili kuandika habari zisizo za kweli dhidi ya Kipande hadi kesi ya msingi iishe. Kati ya mambo aliyolalamikia Kipande katika kesi hiyo ni pamoja na habari kwamba Bandari ya Dar es Salaam haina kamera za usalama (CCTV).

Ikiwa mkataba huu utapitishwa, basi Serikali haitakuwa na uwezo wa kuingia katika eneo la Bandari bila ruhusa ya Impala au kubadili matumizi kwa miaka 33 hadi Impala iwe imeridhia mabadiliko hayo iwapo tu yanatimiza masilahi ya kampuni hiyo.

Chanzo: GAZETI LA JAMHURI

No comments: