Tuesday, December 30, 2014

URAIS CCM RUSHWA WAZI WAZI ,SOMA MAKALA HII ILIYOJICHUKULIA UMAARUFU LEO

Picha na maktaba,MAKALA HII MEANDKWA NA GAZETI LA MWANACHI 
 Ikiwa imebaki miezi 10 tu kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu mwakani, CCM kinaonekana kuteswa na tuhuma za rushwa inayodaiwa kutolewa na makada wake wanaotajwa kutaka kuwania nafasi mbalimbali ukiwamo urais.
Hali hiyo inabainishwa na kauli za baadhi ya makada wa chama hicho katika ngazi mbalimbali ambao wameamua kulalamika waziwazi ama kupitia vyombo vya habari au kwenye mitandao ya kijamii.
Moja ya kauli hizo ni ile iliyotolewa juzi na Mbunge wa Bukoba Mjini, Balozi Khamis Kagasheki kwenye akaunti yake ya Twitter akisema: “Mgawo wa Xmass na Mwaka Mpya kwa wajumbe husika wa CCM ni kucheza na ugumu wa maisha uliopo. Ni ununuzi wa nafasi na si uwezo wa uongozi. Aibu.”
Alipotakiwa kufafanua kauli yake, Kagasheki alisema kwenye maoni yake hakutaja mtu licha ya kwamba wapo wengi wanaotoa zawadi, lakini baada ya kuandika katika mtandao ameandamwa na baadhi ya watu huku wengine wakimtolea lugha chafu.
“Hii ni line yangu ninaitumia kutoa mawazo siku zote, lakini nimeshangaa leo watu wameshikia kidedea maoni hayo mpaka wengine wanatumia lugha kali... sijamtaja mtu kwa sababu najua wapo watu wengi wanaotoa zawadi,” alisema Balozi Kagasheki aliyewahi kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii huku akisisitiza kuwa hayo ni mawazo huru ambayo anayaamini.
Waliyonena kuhusu rushwa
Kauli ya Kagasheki haina tofauti na zile zilizowahi kutolewa na makada wengine, akiwamo mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete na wengine waliowahi kushika nyadhifa za juu ndani ya chama hicho na Serikali yake juu ya kukithiri kwa rushwa katika kusaka madaraka.
Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula alimwambia mwandishi wetu jana kuwa suala hilo linafuatiliwa kwa karibu na dawa yake itaiva Februari baada ya kamati yake ya maadili iliyofuatilia kutoa tathmini yake.
“Tulipotangaza kuwafungia, tuliunda kamati ya ufuatiliaji harakati za kila mmoja kuona je, yale tuliyomtaka kutoyafanya ametekeleza? Sisi tunaheshimu vikao vyetu, hivyo tunasubiri kamati hiyo itakapotuletea taarifa yake.
“Katika tathmini hiyo kama watakuwapo wa kusamehewa watasamehewa na kama watakuwapo wa kuongezewa adhabu wataongezewa.”
Kauli ya Mangula ilikuwa inafafanua makada wa chama hicho waliopewa onyo kali kwa kufanya kampeni mapema na kujihusisha na vitendo vinavyokiuka maadili ndani ya chama na ndani ya jamii.
Mangula alisema hayo wakati kukiwa na madai kuwa baadhi ya wanachama wake kudaiwa kugawa fedha kwa wajumbe wa mkutano mkuu na Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) Zanzibar na maeneo mengine ya nchi.
Mangula jana alikaririwa na gazeti la CCM, Uhuru, akijibu madai hayo kuwa, “hakuna mwanachama aliye juu ya katiba, kanuni na miongozo ya chama na hivyo hakitamvumilia mtu yeyote atakayebainika kutumia fedha.”
Kwa mujibu wa madai hayo, kada mmoja wa CCM anadaiwa kugawa kati ya Sh1 milioni na Sh500,000 kama zawadi ya sikukuu ya Krismasi kwa wajumbe wa vikao vya chama visiwani humo.
Mangula alisema kutokana na malalamiko hayo, CCM itapeleka timu ya uchunguzi kupitia kitengo cha usalama na maadili kuchunguza tuhuma hizo.
Oktoba 25, mwaka jana Rais Kikwete alisema endapo rushwa haitakomeshwa ndani ya CCM, kitaanguka vibaya katika Uchaguzi Mkuu 2015 na iwapo kitanusurika hakitapita mwaka 2020.
Kauli hiyo pia inaungwa mkono na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye aliyewahi kuliambia gazeti hili kuwa iwapo misingi ya uchaguzi ndani ya CCM itaendelea kulalia kwenye rushwa, hataendelea kuwa sehemu yake na kuonya kuwa tatizo hilo limefikia pabaya na litakiangusha chama hicho.
Mwaka 2011, Rais Kikwete alitangaza mkakati wa ‘kujivua gamba’ akiwataka makada wa chama hicho wanaotuhumiwa kwa ufisadi kutafakari na kujiondoa ndani ya siku 90, lakini hata baada ya muda huo kumalizika, mkakati huo uliyeyuka na viongozi wakaanza kubadili maudhui yake.
Waliopigwa ‘stop’
Vigogo waliopewa adhabu hiyo ni Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wasira, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba na aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja.
Wanavyoitazama CCM
Wachambuzi waliozungumza na gazeti hili walisema CCM hakiwezi kupambana na rushwa kwa sababu baadhi ya viongozi wake ni walarushwa na wamekiondoa katika misingi ya kuwatumikia wananchi.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), Bashiru Ally alisema: “Chama hakiongozwi kwa makaripio, mkakati wa kujivua gamba na matamko katika vyombo vya habari. Kinaongozwa kwa mifumo imara, fikra sahihi, dira na historia yake nzuri.
“Ndiyo maana wanachama wa CCM wamekuwa wakitenda mambo kinyume na katiba ya chama chao na hakuna wa kuwachukulia hatua. Kolimba (marehemu) aliwahi kusema kuwa CCM haina dira wala mwelekeo. Hilo linaonekana sasa, kimeshindwa kukemea rushwa.”
Alisema ni vigumu kwa CCM kuikataa rushwa wakati baadhi ya wanachama wake, tena wenye nyadhifa za juu ndani ya chama hicho wakituhumiwa kwa rushwa.
“Mchawi yupo ndani ya CCM yenyewe. Profesa Tibaijuka ni mjumbe wa Kamati Kuu na amepewa mgawo wa escrow lakini chama kipo kimya. Jimbo la Bukoba Vijijini limegawanyika kwa sababu ya rushwa inayotolewa na wanaotaka ubunge, hayo yote CCM hawayaoni na kukimbilia yanayotokea Zanzibar,” alisema. Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam, Dk Benson Bana alisema: “CCM ni chama ambacho kinajibu mapigo ila hakitoi mapigo. Kinachotokea sasa ni dalili mbaya kwake kwani kimekuwa dhaifu katika kuwashughulikia wanachama wake wasio waadilifu.”
Alisema matamko mengi ya chama hicho ni ya kisiasa zaidi na mengi huishia katika vyombo vya habari. “Hayo yanamaanisha kuwa uwezo wa CCM umepungua. Mfano ni Chadema kwa sasa kinatoa mapigo na si kujibu mapigo pekee. Hiyo ndiyo inatakiwa kufanywa na chama cha siasa,” alisema.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alisema Mangula alipotangazwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM aliahidi kupambana na rushwa na mpaka leo kashindwA

No comments: