Sunday, May 10, 2015

DRFA YACHEKELEA TIMU ZAKE KUMALIZA TATU BORA LIGI KUU.





Chama cha soka mkoa wa Dar es salaam kimeonesha furaha yake baada ya timu tatu zilizo katika himaya yake, kumaliza katika nafasi za juu kwenye ligi kuu Tanzania bara iliyomalizika jumamosi mei 9,2015.


Kamati ya utendaji ya DRFA chini ya mwenyekiti wake Almas Kasongo,imesema ni jambo la kufurahisha kuona mkoa wa Dar es salaam unafanya vizuri kisoka na kuwa mfano wa kuigwa kwa mikoa mingine.
Timu hizo zimepongezwa kutokana matayarisho waliyoyafanya tangu kuanza kwa msimu,ambapo mabenchi ya ufundi yameonesha kuwa na nia ya dhati kuleta ushindani katika ligi.


Yanga SC na Azam Fc ndizo zitakazoiwakilisha nchi katika michuano ya vilabu barani afrika,ambapo Yanga itakwenda huko kuwania kombe la klabu bingwa baada ya kutwaa uchampioni,huku Azam ikiwania kombe la shirikisho baada kumaliza katika nafasi ya pili,wakati Simba imemaliza katika nafasi ya tatu.


Aidha DRFA imeipongeza Tff na kamati ya bodi ya ligi kwa usimamizi mzuri wa ligi msimu huu licha ya kuwepo na changamoto ndogondogo kwa vilabu kulalamikia miundombinu ya vyumba vya kubadilishia nguo viwanjani,na uonevu wa baadhi ya waamuzi.


Hata hivyo imeishauri Tff kuangalia kwa kina na kuzifanyia kazi changamoto hizo zilizojitokeza msimu huu ili zisijirudie tena katika msimu ujao,kwa lengo la kuiboresha ligi ya Tanzania,ambayo kuanzia msimu ujao itakuwa na jumla ya timu 16.


Pamoja na hayo DRFA imezishauri Yanga na Azam kujipanga vizuri kwaajili ya mashindano ya vilabu afrika msimu ujao, ili kuandika historia na kuleta vikombe hivyo kwa mara ya kwanza hapa nyumbani.

No comments: